Sera ya soko huria iliyoanza kutekelezwa toka miaka ya 1990 imefungua fursa kwa wawekezaji kuwekeza kwa wingi kwenye maeneo mbali mbali ya kibiashara.
Kwa muda mrefu, Kilimo kimewavuta wawekezaji ambao wamekuwa wakijishughulisha na mashamba makubwa ili kukudhi madhumuni ya biashara ya kuzalisha kwa wingi kupunguza gharama ya kuzalisha kwa kiasi kidogo. Pamoja na kutekelezwa kwa makubaliano baina ya wawekezaji na kijiji wanakofanya shughuli za kilimo, kumekuwa na manunguniko mengi kuhusu wawekezaji kuchukua maeneo makubwa na ardhi ikianza kupungua kutokana na kuongezeka kwa watu na wahamiaji hasa wafugaji.
Ili kupungumza manunguniko ya wakulima inabidi wakulima watayarishwe, ili waweze kuzungumza lugha ya biashara ambayo inalingana na ya wawekezaji.
Ni muhimu wakulima wakaelimishwa na kufahamu kwa undani kuhusu kilimo biashara. Hii itawasaidia wakulima kutimiza nia ya kufanya kilimo biashara na kupata kipato kikubwa. Ili kufikia lengo hilo inabidi wakulima wafanye mambo yafuatayo;
- Walime kwa kiasi cha kutosha.
- Wasindike wenyewe na
- Watafute soko na kuuza bidhaa zilizoongezwa thamani badala ya kuuza mali ghafi.
Mkulima anayeuza bidhaa zilizoongezewa thamani anakuwa na fursa ya kushiriki kupanga bei badala ya kupangiwa bei kitendo ambacho kinampa fursa ya kupata faida kubwa. Wawekezaji wanahamasishwa kuchukua mali ghafi kwa wakulima na kusindika kwa niaba ya wakulima na kuwaunganisha na masoko ya bidhaa wakitumia teknolojia za kisasa ambazo mkulima mdogo hawezi kuzipata kutokana na kuwa na mtaji midogo.
Kuna faida wakulima wadogo kujiunga na wawekezaji wanaofanya shughuli za kilimo kwa kiwango kikubwa. Moja wapo ya faida hizo ni pamoja na mkulima mdogo kuunganishwa na soko ambalo humpatia mkulima midogo faida.
Halikadhalika humuwezesha mkulima mdogo kuongeza uwezo wa kupanua shamba, kupata kipato kikubwa na kupunguza manunguniko. Mkulima ambaye anauza mazao yaliyoongezewa thamani anaweza kupanua kilimo chake na kuongeza idadi ya mazao ambayo anaweza kulima, kusindika na kuongezea thamani.
Vipi kuhusu wafugaji?
Wafugaji wanaweza kutumia eneo dogo la ardhi ikiwa wanafuga ndani badala ya kuchunga na kuwa na mkakati wa kutenga maeneo ambayo yataoteshwa malisho kwa ajili ya mifugo.
Kwa kufanya hivyo pia itapunguza migogoro ambayo inatokea kati ya wakulima na wafugaji kwa baadhi ya maeneo kwa sababu ya wafugaji kupenda kuchunga badala ya kufuga ndani.
Kwa kufanya ufugaji wa ndani, itawawezesha pia wafugaji kuuza mifugo iliyoongezwa thamani, kwa mfano kunenepesha mifugo na kuongeza tija ya kupunguza kiasi cha mifugo badala ya kuwa na mifugo mingi isiyokuwa na tija. Mfugaji anaweza kuwa na mifugo michache yenye faida. Kwa maelezo zaidi juu ya mnyororo wa ongezeko la thamani, unaweza kuwasiliana na Herment A. Mrema kutoka Africa Rural Development Support Initiative (ARUDESI) kwa simu +255 752 110 290, Barua pepe: machomingi@yahoo.com