Rose Rafael Mollel (35) nina Watoto wanne. Mimi ni mfugaji wa kuku wa kienyeji.
Nilianza na kuku 10 tu ambao walinipa changamoto kuwafuga kwani kuku watatu walikufa kwa ugonjwa wa kideri. Nikajiuliza nitafanyaje sasa na
sipendi kutumia madawa ya kemikali!
Nikabuni chanjo ya kienyeji: tangawizi nikaisaga, matone ya myaa na chumvi kidogo nikakoroga nikawapa vijiko vitatu asubuhi na vitatu jioni. Tangu kipindi hicho kuku wangu hawajawahi kunisumbua tena na ugonjwa wa kideri sasa wameongezeka nina kuku 27. Navuna mayai na kuuza kijijini.
Nilipokutana na watu wa Mkulima Mbunifu walipokuja kutembelea kikundi cha jirani, walinipatia kitabu cha ufugaji wa kuku chenye maarifa zaidi. Kuna magonjwa na jinsi ya
kutibu, chakula bora kwa kuku na jinsi ya kujenga banda bora la kuku.
Nimefurahi kwani nitapanua mradi wangu na nitapata mafanikio zaidi.