- Mifugo

Maji moto (weaver’s ant) wadudu rafiki wanaowezesha kilimo hai

Sambaza chapisho hili

Maji Moto au Sangara ni aina ya wadudu, ambao ni rafiki kwa mkulima yeyote anayefanya shughuli zake kwa kuzingatia misingi ya kilimo hai. Ni wadudu wadogo sana ambao huishi katika miti ya mikorosho pamoja na miembe. Mara nyingine hupatikana pia katika pamba.

Ikumbukwe kuwa tangu kuumbwa dunia, kila kitu kilikuwa kiasili, watu walikula vyakula na matunda ambayo yalikuwa katika mfumo wa asili bila kuwa na matumizi ya madawa ya viwandani. Wadudu kama ilivyo kwa maji moto na wengineo, walitumika kudhiti wadudu waharibifu.

Kwa kuona umuhimu na mahitaji ya mazao yanayotokana na kilimo hai, shirika la maendeleo la Waswis (SDC) linatoa kipaumbele na kufadhili miradi ya kilimo hai. Moja wapo ni huu mradi wa kutafiti na kutumia maji moto kama njia ya kudhibiti wadudu waharibu wa zao la korosho bila kutumia dawa za kemikali.

Maisha ya maji moto

Wadudu hawa huishi kijamaa katika miti waliyochagua wao. Hupendelea kuishi kwa ukoo katika mti mmoja na mara nyingine hupigana na koo kugawanyika hivyo kuwafanya kuwa katika miti mingi zaidi, jambo ambalo ni faida kwa mkulima anayefanya kilimo hai.

Huishi katika viota ambavyo hutengeneza kwa kutumia majani ya miti yaliyokomaa na huunganisha kwa kutumia ute unaotoka katika miili yao wenyewe.

Katika viota hivyo  huishi malkia ambaye huzaliana zaidi na zaidi, huku wengine wakifanya kazi ya kutafuta chakula na kula ndani ya viota hivyo. Chakula ambacho ni wadudu wengine wasiokuwa wa jamii yao kama vile mbu wa mikorosho na mbu wa minazi.

Rafiki wa mkulima awa kilimo hai

Hawaogopi

Wadudu hawa pamoja na kuwa wadogo sana, lakini ni jasiri, na hupambana na adui yoyote anayeingia katika himaya yao. Wana nguvu sana kwani muda wote utawaona wakipanda na kushuka bila kupumzika huku wakifanya shughuli zao. Wana harufu ya pekee sana, inayowasaidia kuwasiliana. Ukimgusa mmoja tu haraka sana wengine wote wanafahamu kuwa kuna jambo linatokea na hivyo wanashambulia kwa ukali.

Malkia

Katika kila kiota cha maji moto, utakuta kuna malkia mmoja. Hata hivyo mara nyingine katika majira ya kiangazi au vuli, unaweza kukuta malkia zaidi ya mmoja katika kiota. Ni rahisi sana kumtambua malkia kwa kuwa ana umbo la tofauti na wenzake. Yeye ana umbo kubwa, rangi ya kijani au udhurungi, na huwa na tumbo kubwa kwa ajili ya kuzalisha mayai.

Dume

Madume huwa na umbo dogo kuliko malkia na huwa na rangi nyeusi. Kazi yao ni kumpanda malkia ambapo hata hivyo hufa mara baada ya kufanya hivyo. Mara nyingi hufa baada ya wiki moja.

Wafanyakazi wadogo

Hawa huwa kama bibi, wao kazi yao kubwa ni kukaa kwenye kiota na kutunza maji moto wachanga.

Wafanya kazi wakubwa

Hawa hufanya kazi kwa pamoja na wana kazi ya kutekeleza majukumu yote katika kundi lao. Wanalinda kundi lao dhidi ya maadui, kukusanya na kuleta chakula kwenye kundi, na kutengeneza kiota. Siyo hivyo tu, lakini pia inapotokea kiota chao kuharibiwa au kusumbuliwa wana kazi ya kuhamisha maji moto wadogo kutoka kwenye kiota na kuhakikisha wako mahali salama.

Maji moto hupendelea kujenga viota vyao katika mimea yenye majani mapana yaliyokomaa au yenye majani mengi, na ambayo haidondoshi majani yake yote wakati wa kiangazi ili kuepuka usumbufu.

Wanafanyaje kazi katika kilimo hai

Wadudu hawa kama nilivyotangulia kusema, ni wajanja sana na hawaruhusu adui kuingia katika himaya yao. Kwa mantiki hiyo hushambulia aina nyingine yoyote ya wadudu wanaojaribu kuingia eneo ambalo ni makazi hayo.

Kuna wadudu kama mbu wa mikorosho na mbu wa minazi ambao huharibu matunda ya korosho na maembe kwa kutoboa. Mbu hawa ni chakula kikubwa cha maji moto ambapo huwakamata na kuwaingiza katika viota vyao na kuwala.

Kutokana na hali hiyo inakuwa ni vigumu sana  kwa mbu hao kupata nafasi ya kuharibu korosho au maembe, na kufanya uzalishaji kuongezeka bila ya kutumia kemikali.

Mfano katika zao la korosho, wakulima ambao wamekuwa wakitumia maji moto kudhibiti wadudu hawa, wamepata ongezeko la uzalisha kwa kila mkorosho mpaka kufikia kiasi cha asilimi sabini na tano (75%).

Mbali na ongezeko la uzalishaji kwa mikorosho yenye maji moto, pia wakulima wanaozalisha katika misingi ya kilimo hai, wamekuwa wakipata pato zaidi kwa kuwa bei ya mazao yanayozalishwa kiasili yana bei kubwa zaidi kuliko ilivyo kwa uzalishaji wa aina nyingine.

Mfano,kilo moja ya korosho iliyozalishwa kwa kufuata misingi ya kilimo hai kwa msimu uliopita, mkulima aliweza kuuza kwa shilingi 1,750 za Tanzania, na ambayo haikuzalishwa kwa njia ya kilimo hai, iliuzwa kwa shilingi 1,500 za Tanzania. Hivyo unaweza kuona ni kwa namna gani anaefanya kilimo hai anaweza kupata faida zaidi.

Hali kadhalika wakulima waliokubali kujiunga katika vikundi na kufanya kilimo hai ni rahisi kupata misaada ya kuwezesha shughuli zao kama shirika la maendeleo la waswis (SDC) linavyofanya kwa wakulima wa korosho eneo la masasi mkoani Mtwara, ambapo pia ni rahisi kupata soko wanapokuwa katika vikundi.

Utunzaji na usambazaji wa maji moto shambani

Unaweza kusambaza maji moto katika miti mingine kwa kufunga kamba (interconnection) kutoka mti mmoja kwenda mwingine. Hii husaidia maji moto kuwa katika miti mingi zaidi shambani na kuongeza ufanisi.

Ili kufanya wadudu hawa kuendelea kuwepo na kustawi, mkulima anashauriwa kuzingatia yafuatayo:

  • Kutopuliza dawa za kemikali shambani mwake.
  • Kutochoma moto shamba.
  • Kuchukua maji moto kutoka katika aina nyingine ya miti na kuwasambaza shambani mwake.
  • Kuweka matandazo shambani ili wadudu maadui wa maji moto wasipande juu ya miti kuwashambulia.

Zingatia kuwa maji moto hukabiliana na mbu wa mikorosho na minazi tu, hivyo endapo kutaibuka aina nyingine ya ugonjwa hawawezi kukabiliana nao, hivyo ni vyema kukagua mazao yako mara kwa mara na kutumia dawa za asili kukabiliana na aina hiyo ya ugonjwa au wadudu.

Kwa sasa, utafiri zaidi juu ya namna maji moto wanavyoweza kutumika kuleta ufanisi zaidi katika kilimo hai unaendelea katika chuo kikuu cha Sokoine (SUA) na katika kituo cha utafiti wa kilimo Naliandele mkoani Mtwara.

Ukiwa na swali zaidi juu ya maji moto, unaweza kuwasiliana na bwana Yuda John kwa simu namba +255 686 164 194

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *