Kilimo kimekuwepo tangu zama za mababu zetu. Binadamu wa kwanza walipata chakula chao kwenye mazingira yanayowazunguka na kwa juhudi kama uwindaji kabla ya kuanza kulima ardhi, kupanda mazao na kufuga mifugo kama vyanzo vya lishe. Hii ni pamoja na nafaka, mazao ya mizizi, karanga, matunda, nyama, maziwa, na hata mayai. Kilimo kimebadilisha maisha na maisha pia yamebadilisha muundo wa kilimo.
Kwa sasa, kilimo ni muhimu sana na umuhimu huu hauwezi kupungua katika miaka ya karibuni. Maadamu watu wanaishi, ni lazima wakule na wakulima wataendelea kulima!
Nini kinafanya kilimo kuonekana muhimu zaidi? Nini hufanya wakulima kutumia muda wao mwingi mashambani; kwenye jua kali, wakivuta vumbi toka kwenye ardhi iliyokauka wakati wa maandalizi ya msimu wa mvua, n ahata kuloa wakati wa mvua za rasharasha wakijaribu kupata thamani zaidi?
Watu wengi hawajawahi kufikiri kwa nini kilimo ni muhimu sana, hata wakulima wenyewe hawajiulizi hili. Tunafanya kilimo kama desturi tu, na tukijaribu kueleza kwa nini tunafanya tunachofanya, tunashindwa kujieleza au tunaeleza bila kuwa na uhakika.