Kabla mkulima hajavuna mazao yake, ni vyema akatambua namna ya kuyahifadhi kwa lengo la kuhakikisha zao linabaki katika ubora wake kwa muda mrefu.
Kwa nini kuhifadhi
Mazao yanapovunwa, ni vyema kuhifadhiwa ili kuhakikisha usalama wa chakula katika kaya na taifa kwa ujumla. Kuweka akiba kwa matumizi ya baadaye au kuhifadhi kwa ajili ya matumizi ya mbegu. Mikunde huhifadhiwa kwenye maghala ya aina tofauti na yanaweza kuwa ya jingo au chombo chochote kilicho imara.
Wakulima wengi hupenda kuhifadhi mazao ya mikunde kwa kutumia njia za asili kama vile vilindo, madebe, mitungi au vibuyu. Njia hizi ni duni na husababisha upotevu wa mikunde kwa kiasi kikubwa na pia hazikidhi mahitaji ya kaya. Ili kuepuka upotevu wa mazao wakati wa kuhifadhi, ni muhimu kutumia maghala bora.
Ghala bora
Ghala bora ni chombo chochote kile au jengo lolote lililo imara na lenye sifa zifuatazo;
- Liwe na uwezo wa kuzuia wadudu, panya, mvua na unyevu kutoka chini.
- Liwe na nafasi ya kutosha kuweka mazao, kukagua na kutoa.
- Liwe na uwezo wa kuhifadhi mazao yaliyokusudiwa
Aina ya maghala bora
- Kihenge
Hii hujengwa kwa kutumia vifaa kama vile matete, mianzi, miti au fito nyembamba na kusiribwa ndani na nje kwa udongo, sementi na samadi. Paa la kihenge huezekwa kwa kutumia nyasi, makuti au bati.
Sifa za kihenge
- Kiwe kimeinuliwa juu kwa zaidi ya mita moja kuzuia unyevu kutoka ardhini.
- Kiwe na vizuizi vya panya, na kiwe na mfuniko na mlango wa kutolea nafaka.
- Kihenge bora hudumu kwa muda wa miaka mitano hadi kumi kumi na tano
- Sailo au bini
Haya ni maghala yanayojengwa kwa dhana ya kutokuwepo na mzunguko wa kawaida wa hewa ndani ya nafaka iliyohifadhiwa na kusababisha wadudu waharibifu na vimelea vya magonjwa kutoweza kusitawi na kuharibu nafaka.
Ghala hili hujengwa kwa kutumia bati la chuma au matofali ya kuchoma au ya sementi. Salio za bati hazifai kutumia kujengea hasa katika maeneo ambayo mabadiliko yavipindi vya joto na baridi ni vikubwa kwasababu wakati wa joto bati linapata joto kwa haraka.
Aidha, wakati wa baridi, bati hupoa kwa haraka pia na kupata unyevu kwa ndani, jambo ambalo linasababisha nafaka au mikunde iliyohifadhiwa kupata unyevu na kuoza.
Matofali ya kuchoma au ya sementi hayapitishi joto au baridi kwa hiyo hakuna unyevu unaoweza kutokea ndani ya ghala na kusababisha mazao kuoza. Mazao yanayohifadhiwa ndani ya maghala ya aina hii hayahitaji kufungashwa (kichele) na yanapaswa kuwa na unyevu ulioshauriwa ili kuepuka kuoza.
Sifa ya salio au bini
- Maghala haya yana uwezo mkubwa wa kuzuia unyevu kutoka ardhini kwani huwekwa karatasi maalumu wakati wa kujenga msingi.
- Yana uwezo wa kuzuia uingiaji wa takataka na panya.
- Maghala haya yana mlango wa kutolea nafaka kwa chini na hivyo hurahisisha kazi ya kutoa nafaka wakati wa mahitaji.
- Yana uwezo wa kuhifadhi kulingana na mahitaji; Sailo ina uwezo wa kuhifadhi magunia kati ya 10 hadi 30, na Bini ina uwezo wa kuhifadhi magunia kati ya 10 hadi 50.
- Mapipa
Mapipa yenye mifuniko imara hutumika kuhifadhi nafaka kwa dhana ya kutokuwa na hewa ndani ya nafaka. Pipa likijazwa nafaka na kufungwa sawasawa hakuna hewa inayoingia na hakuna mdudu anayeweza kuishi ndani yake, na hata punje za nafaka hufa baada ya kuhifadhiwa kwa muda hivyo inashauriwa kuwa nafaka inayotegemewa kwa ajili ya mbegu isihifadhiwe ndani ya pipa.
- Maghala ya nyumba
Hifadhi ya mikunde hufanyika katika chumba au nyumba maalumu na maghala haya huhifadhi mazao yaliyofungashwa kwenye magunia. Uwezo wa kuhifadhi hutegemea wingi wa mazao.
Mambo ya kuzingatia kuhifadhi mikunde
- Matayarisho kabla ya kuhifadhia
Hii hujumuisha uandaaji wa vifungashio safi na vya kutosha, kuhakikisha hazina wadudu wala magonjwa kwa kuchemsha au kuweka dawa za kuhifadhia, kuandaa maghala hayo kwa kusafisha, kukarabati, kunyunyizia dawa au kujenga, na kuondoa mabaki ya mazao ya zamani kabla ya kuweka mapya.
- Jinsi ya kupanga magunia yenye mikunde
Panga magunia katika safu juu ya chaga ili kuepuka mikunde kuoza kutokana na unyevu wa sakafu. Panga kwa safu zinazopishana ili kuruhusu mzunguko wa hewa kati ya gunia na gunia pamoja na kuimarisha safu za magunia (hii hujumuisha pia kupanga magunia kwa kuacha nafasi ya mita moja kutoka ukutani ili kurahisisha kazi ya ukaguzi ndani ya gunia). Upangaji wa safu hurahisisha kazi ya kufukiza ambapo dawa hupenya katika kila gunia.
- Ukaguzi wa maghala
Ni lazima kufanyike kwa ukaguzi wa maghala na punje za mikunde kila baada ya wiki moja ili kuweza kugundua kama kuna mashambulizi yeyote ya wadudu, panya, unyevu na kujua hali ya ghala kwa ujumla. Wakati wa kukagua ni muhimu kuzingatia yafuatayo;
- Hali ya ghala: Ni vyema kujua hali ya ghala kwa ujumla kama bado ni imara na halivuji, kuziba nyufa kama zimejitokeza pamoja na kusafisha ndani ya ghala na nje.
- Halia ya mazao: Ukaguzi pia uangalie hali ya mazao kujua kama kuna dalili za kushambuliwa na wadudu waharibifu, magonjwa ua panya.