Maziwa ni bidhaa ya chakula ambayo kila mtu anahitaji. Ni moja ya lishe bora yenye protini nyingi za hali ya juu, kalsiamu na vitamin B12. Aidha kuongezeka kwa wafugaji na wazalishaji maziwa kumeibua changamoto kwa baadhi yao ambao wamekuwa wakiuza maziwa na kuyagandisha na mengine kubaki.
Hali hii imewafanya baadhi ya wafugaji kupata hasara kutokana na maziwa kuharibika. Lakini maziwa makavu ya unga ambayo sawa na mabichi pia yana virutubisho vingi yanaweza kuokoa pesa na rahisi kuyatumia na kuhifadhiwa kwa muda mrefu. Hivyo leo tunakufundisha namna ya kusindika maziwa mabichi ili kuwa unga.
Kwa nini utengeneze maziwa ya unga?
Kuna faida nyingi ya kutengeneza maziwa ya unga nyumbani kwa sababu inakusaidia kuokoa gharama kwa kupunguza upotevu wa maziwa. Tambua maziwa haya ya unga unaweza kuyahifadhi muda mrefu na yana virutubisho kama maziwa mabichi.
Kuna njia kadhaa za kutengeneza maziwa ya unga nyumbani moja ikiwa ni kuyakausha kwa kutumia dehydrator ya chakula. (Hii ni chombo cha kielektroniki kilichoundwa kuhifadhi matunda, mboga mboga, mimea, nyama na samaki kwa kuondoa unyevu au kuvikausha).
Kwa kutumia Dehydrator;
- Weka maziwa yako kikombe kimoja au viwili kulingana na ukubwa wa trei ya dehydrator kwa kila trei.
- Weka kipunguza maji kwa kipimo cha 130 ° F – 135 ° ili kayakausha maziwa. Itachukua takriban saa 12 kwa maziwa kukauka.
- Baada ya maziwa kukauka kabisa na kutengeneza kipande au vipande, vunja vipande vipande na uviweke kwenye blender saga hadi iwe unga.
- Chukua unga wako na hifadhi.
Njia nyingine ya kuyatengeneza maziwa mabichi kuwa unga ni kuyachemsha maziwa kwa saa kadhaa hadi maji yakauke;
- Washa jiko lako la gesi au stovu hakikisha linawaka moto wa wastani na siyo mkali.
- Mimina maziwa kwenye sufuria kubwa kisha, yatenge kwenye jiko ili yachemke huku ukikoroga taratibu kuzuia yasimwagike mpaka yatakapoanza kukaukia na kutengeneza mgando wa vipande.
- Chukua vipande hivyo baada ya kupoa na visage kwenye blender ili kufanya viwe unga.
- Mpaka hapo tayari utakuwa umebadili maziwa yako mabichi kuwa unga.
Vidokezo vya kukumbuka:
- Ili kupata kilo 1 ya unga wa maziwa unahitaji lita 8.5 za maziwa.
- Ikiwa unatengeneza maziwa ya unga kwa dehydrator, hakikisha unatumia trei mbili tu badala ya zote kwa wakati mmoja ili kuangalia ikiwa mpangilio wa halijoto unafanya kazi kukausha maziwa.
- Maziwa yaliyopungukiwa na maji yanapaswa kuwa kavu kabisa, ikiwa sio makavu yanaweza kusumbua kusaga na unga wake kuharibika.
Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana +255 622 642620.