Siafu
Siafu ni miongoni mwa wadudu wanaoshambulia nyuki wanaozalisha asali. Ni wadudu wapole wasiokuwa na shida lakini huvamia mzinga na kuwauwa nyuki. Kutokana na uharibifu huo, humuumiza na kumvunja moyo mfugaji, na mara nyingine wanaweza kuuma na kusababisha maumivu.
Kuweka mizinga sehemu yenye siafu inaweza kusababisha utunzaji kuwa mgumu. Kukiwa na kundi dhaifu la nyuki linaweza kusababisha nyuki kuondoka, na hii ni njia moja wapo ya nyuki kujilinda dhidi ya uvamizi wa mara kwa mara wa siafu. Kwa ujumla imekuwa ikiripotiwa kuwa siafu husababisha uharibifu kwa wafugaji wa nyuki wa asili na hata wa kisasa.
Udhibiti
Njia ambayo imeonekana kuwa na ufanisi katika kuwadhibiti siafu ni kutafuta kiota chao sehemu ya kufugia nyuki, kisha kuharibu kiota hicho kwa kuchoma. Njia bora inayopendekezwa ya kudhibiti siafu kwenye eneo la ufugaji wa nyuki ni kuondoa masega ya asali kwenye eneo hilo baada ya kuvuna, kuondoa miti iliyo oza, pamoja na kufyeka majani kutoka katika eneo hilo.
Kwa ujumla njia bora ya kudhibiti siafu ni kuweka mzinga juu ya nguzo zenye urefu wa sentimita 30-50 na kuzipaka mafuta machafu ya kulainisha mashine (oil chafu) au grisi. Ukaguzi wa mara kwa mara na kurudia kupaka oil chafu au grisi ni muhimu.
Njia nyingine ambayo ni ya kutegemewa zaidi ni kuweka nguzo kwenye debe au ndoo ya plastiki iliyojazwa maji au oil chafu.
Usafi wa mara kwa mara katika eneo la mizinga ni muhimu ili kuepusha kuwepo daraja linaloweza kuwawezesha siafu kufikia mizinga, pia maji yaliyomo kwenye ndoo yabadilishwe mara kwa mara.
Nyigu
Nyigu ni moja ya maadui wakubwa wa nyuki wanaozalisha asali. Nyigu hukamata na kuwaua nyuki ambao hawakimbii wakati wa kuruka, na mara nyingi hushambulia kundi lililodhaifu. Uvamizi wa nyigu katika mizinga ya nyuki huwasababisha nyuki kuhama.
Nyigu pia wanaweza kusababisha uharibifu wa vyanzo vya asali. Kwa kawaida uharibifu huu hutokea kwa msimu. Inashauriwa wafugaji kujifunza kutokana na mazingira yao, ni kipindi kipi cha mwaka ambacho uharibifu huu unaosababishwa na nyigu hutokea.
Udhibiti
Wafugaji wa nyuki wanashauriwa kutumia mitego inayoweza kunasa nyigu, au kutumia kitambaa chenye matundu ambayo nyigu hawawezi kupenya kuingia kwenye mzinga, lakini ambacho hakizuii nyuki kuendelea na shughuli zao.
Angalia sehemu nyigu walipojenga na uharibu viota vyao, ingawa inahitaji muda na mara nyingine njia hii haifanikiwi sana. Wafugaji wa nyuki ni lazima pia wawe makini sana na eneo la kuweka mizinga.
Weka mizinga katika eneo lililo salama na kuhakikisha kuwa vitundu vya nyuki kuingilia kwenye mzinga ni vidogo ili kutokuruhusu aina nyingine ya wadudu kuweza kuingia kwenye mzinga.
Mende
Kuna aina tofauti ya mende wanaoishi sehemu inakotengenezwa asali. Hata hivyo, mende hawa wanaweza tu kuishi penye kundi dhaifu la nyuki. A i n a nyingi za mende hawana madhara k w a nyuki, japo hula asali au poleni. Pia mende huvamia koloni la nyuki wakati wa shughuli muhimu kama vile wakati wa kutengeneza asali.
Mende wadogo wanaoishi kwenye mzinga, huzaliana na kuongezeka. Mende hawa huweka viota vyao vya mayai sehemu ambayo nyuki hawawezi kufikia. Viluwiluwi wa mende hupendelea zaidi kuishi penye poleni au mazega ya asali. Viluwiluwi wakubwa huondoka kwenye mzinga na kwenda kuishi nje ili waweze kukuwa na kuwa mende kamili.
Mende na lava wa mende wanaweza kuathiri uzalishaji wa asali ndani ya mzinga na nje ya mzinga. Katika eneo hilo huanzisha ulaji wa malighafi za asali au zilizoko kwenye asali na hivyo kusababisha asali kuanza kuvunda. Viluwiluwi wa mende na kinyesi chake husababisha asali kubadili rangi na ladha yake.
Udhibiti
Njia pekee ya udhibiti wa mende kwenye mizinga na eneo la uzalishaji wa asali ni kuwa na koloni ambalo liko imara, na kuondoa lile linaloonekana kuwa dhaifu. Tatizo la wadudu hawa ni kwamba wanaweza kuzaliana na kuongezeka hata wakiwa nje ya mzinga, hasa pale kunapokuwepo matunda yaliyo oza mfano apple na ndizi – ambapo hufanya sehemu hizo kama sehemu za viota vyao.
Hali hii ndiyo inayowasaidia kuweza kuvamia mizinga ya nyuki. Mende wanauwezo mkubwa wa kukimbia kwa haraka na hata kuruka. Hii huwasaidia kuweza kuenea kwa haraka kwenye koloni la nyuki, na hata katika maeneo yanayofaa kwa uzalishaji wa asali.