- Mifugo

Hifadhi vyakula kuepuka njaa wakati wa ukame

Sambaza chapisho hili

Hifadhi mazao ili uweze kuwa na chakula kwa muda mrefu bila kuharibika. Utunzaji pia husababisha vibaki na ubora pamoja na kurahisisha upatikanaji muda mwingi kwa ajili ya chakula.

Mara nyingi wakulima hupambana shambani kwa ajili ya kuzalisha chakula ambacho pasi na shaka ndio hulisha watu wote waliopo vijijini na mijini. Pamoja na kujishughulisha huko hujikuta wanabaki bila akiba ya chakula hasa katika kipindi cha kiangazi ambapo mashamba mengi hayazalishi vyakula.

Ili kukabiliana na tatizo hilo katika kipindi hiki tunapoelekea kwenye kiangazi, tumekuandalia makala hii kwa ufupi namna unavyoweza kuhifadhi vyakula hasa jamii ya mizizi ili kukukimu katika kipindi kigumu

Ili kukidhi matakwa ya makala hii na kwa kuzingatia mazao ambayo mara nyingi hutumika kama mazao ya kiangazi au yanayotumika zaidi kukabiliana na njaa, tutazungumzia zaidi mazao ya mizizi hasa mihogo na viazi.

Mazao ya Mihogo na viazi vikiwa na kiwango kikubwa cha unyevu huaribika haraka joto linapoongezeka.

Ni nini husababisha upotevu!

Mara nyingi mazao yanapokuwa na wadudu huaribika kwa urahisi zaidi. Hii inatokana na kupumua kwa wadudu kunaongeza unyevu. Binadamu na wanyama husababisha upotevu, kuvuna mazao yasiyokomaa, uvunaji mbaya na mengineyo yanayofanana husababisha upotevu wa mazao.

Uwepo wa Kemikali

Mabadiliko ya rangi kwa upande wa viazi endapo vitamenywa kwa kuwekwa kwenye chombo kisicho na maji maji au viazi vya kuhifadhi endapo vitamenywa bila ya kuanikwa vinabadilika rangi na kuwa vya kahawia.

Namna ya kuhifadhi

Mazao ya mizizi (muhogo/viazi) yana unyevu mwingi ambao unafikia asilimia 14. Unyevunyevu huo husababisha mihogo kuharibika haraka sana endapo haitahifadhiwa ipasavyo.

Ili kuepuka uharibifu na upotevu, zingatia mambo yafuatayo kwa ajili ya uhifadhi

  • Uvunaji bora.
  • Chambua viazi /mihogo ambayo haijashambuliwa na wadudu.
  • Kutumia vifungashio sahihi.

Hifadhi ya mazao ya mizizi imegawanyika katika sehemu kuu mbili

  • Hifadhi ya mihogo/ viazi vibichi
  • Hifadhi ya mihogo/ viazi vikavu

Hifadhi ya muhogo mbichi

Kuna njia nyingi za kuhifadhi mihogo mbichi zinazotumiwa na wakulima

kwa lengo la kuhifadhi unyevu uliomo kwenye mihogo usipotee. Hata hivyo njia hii ya uhifadhi ni ya muda mfupi.

Hifadhi mihogo mibichi kwenye viroba

Hii ni teknolojia ya kuhifadhi mihogo ambayo haitahifadhiwa kwa muda mrefu. Njia hii inafaa zaidi kwa mihogo inyohifadhiwa kwa ajili ya chakula na biashara. Njia hii inaweza kuhifadhi muhogo kwa muda wa siku 1 hadi 2.

Jinsi ya kuhifadhi

  • Chagua mihogo isiyo na jeraha.
  • Osha kwa maji safi ili kuondoa udongo na uchafu mwingine.
  • Tumbukiza kwenye maji kwa muda wa dakika moja.
  • Weka mihogo kwenye kiroba kwa kuipanga vizuri.
  • Funga kwa usahihi kwa kutumia kamba imara.
  • Panga viroba vyenye mihogo kwenye kichanja.
  • Hakikisha kichanja kipo ndani ya stoo, nyumba au sehemu yenye paa madhubuti.

Hifadhi ya mihogo mibichi kwenye makasha ya mbao

Hii ni aina ya uhifadhi wa mihogo inayoweza kudumu kwa muda wa miezi 2 bila ya kuharibika.

Namna ya kuhifadhi

Ni muhimu mkulima akazingatia mambo yafuatayo kabla ya kuhifadhi mihogo kwa kutumia njia hii ya makasha.

  • Tandika karatasi ya nailoni kuzunguka kuta ndani ya kasha.
  • Weka maranda ya mbao au masago.
  • Nyunyiza maji kidogo katika maranda.
  • Panga mihogo na uhakikishe haigusani kwa kuweka Maranda katikati ya muhogo na muhogo.
  • Endelea kupanga kwa mtindo huo hadi lijae.
  • Funika kwa kutumia Maranda au masago yenye unyevu.
  • malizia kwa kufunika na karatasi la nailoni.
  • Hifadhi makasha ndani ya nyumba juu ya kichanja.

ZINGATIA: Faida za Maranda au masago ni kuhifadhi unyevu

kwenye mihogo na kuzuia isibanane na kuchubuka, wakati Karatasi la nailoni linasaidia kuzuia unyevu uliopo kwenya maranda na mihogo usipotee.

Hifadhi ya viazi vitamu vibichi

Ili kuhifadhi viazi vitamu, hakikisha unazingatia mambo yafuatayo ili kuwa na ufanisi maridhawa.

Imarisha Ngozi

Kabla ya kuhifahdi viazi vibichi ni muhimu kuvianika kwa muda wa siku 1-2. Lengo la kuanika ni kuimarisha ngozi na kuzuia upotevu wa unyevu wa viazi na kuponyesha majeraha.

Hatua hii husababisha ngozi ya viazi kuwa imara na nene zaidi. Hali hii huvifanya viazi viweze kuhifadhiwa kwa muda mrefu zaidi na wakati huohuo huimarisha ubora.

Viazi hufunikwa kwa masago au magunia ili kupata hali ya joto na unyevu mwingi kwenye chumba vinapohifadhiwa. Kwa kawaida huhitaji hali hewa yenye nyuzijoto 27-34. Viazi huachwa muda wa siku 5 hadi 20.

Viazi vilivyoimarishwa ngozi havichubuki kwa urahisi na vichomozo huonekana kwa mbali. Aina hii ya uhifadhi ni kwa ajili ya muda mfupi na ni kwa ajili ya chakula na

biashara.

Uhifadhi wa viazi kwenye shimo

Aina hii ya uhifadhi ni moja ya njia bora ya kuhifadhi viazi vibichi kufunika kwenye shimo ,kwa kutumia ghala la majani. Kwa njia hii viazi vinaweza kuhifadhiwa kwa muda wa miezi mitatu bila kuharibika.

Jinsi ya kuhifadhi

  • Shimo lichimbwe sehemu isiyotuhamisha maji ili kuepuka viazi kupata unyevu au kuoza.
  • Shimo lichimbwe kulingana na wingi wa mazao.
  • Shimo lenye urefu wa mita mbili na upana wa mita moja na kina cha mita moja huweza kuhifadhi kilo 500.
  • Jenga paa la nyasi kufunika eneo lenye shimo.

Uhifadhi ya mihogo mikavu

Njia pekee na bora zaidi ya kuhifadi mihogo kwa muda mrefu ni kuhifadhi mihogo

Iliyokaushwa. Mihogo iliyokaushwa huweza kuhifadhiwa kwa muda wa miezi 6 hadi 12 bila kuharibika.

Makopa hushambuliwa sana na dumuzi. Ili kukabiliana na tatizo hilo inashauriwa kuhifadhi mihogo iliyoparuliwa na kukaushwa. Chagua mihogo ambavyo ipo katika hali ya ungaunga na kufanya mashambulizi ya dumuzi yapungue kabisa.

ZINGATIA: Mihogo haihifadhiwi kwa kutumia madawa ya viwandani. Hifadhi katika hali ya usafi na kukagua ghala kuona kama kuna mashambilizi ya panya. Chukua tahadhari kuepuka upotevu wa chakula hicho

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *