Kuku wa asili ni aina ya kuku ambao wamekuwepo nchini kwa muda wa miaka mingi na damu au koo zao hazikuchanganywa na aina yeyote ya kuku wa kienyeji. Kuku hawa wana rangi na maumbo mbalimbali.
Kwa kawaida ufugaji wa kuku wa asili nchini Tanzania hufanywa na wafugaji wadogo wadogo wanaoishi kandokando ya miji na wale wanaoishi hasa vijijini.
Kuku hawa wa asili hufugwa kwa mtindo huria yaani hufungiwa ndani nyakati za usiku na hufunguliwa na kuachiwa huru asubuhi ili wajitafutie chakula.
Kuku wa asili hutoa mazao machache sana yaani nyama na mayai; Kwa mfano kuku mmoja wa asili hutaga kiasi cha mayai 40 hadi 60 kwa mwaka badala ya 100 hadi 150 iwapo atatunzwa vizuri.
Aidha, uzito wa kuku hai ni chini sana, wastani wa kilo 1.0 hadi 1.5 kati ya umri wa zaidi ya miezi 6 badala ya kilo 1.8 hadi 2.5 iwapo anapata matunzo vizuri.
Sifa za kuku wa asili
- Kuku wa asili ni wastahimilivu wa magonjwa, lakini ni muhimu wakikingwa na baadhi ya magonjwa ya kuku kama vile mdondo, ndui ya kuku na ikiwezekana wapewe kwa kuendeleza.
- Kuku wa asili wana uwezo wa kujitafutia chakula lakini ni muhimu kuwapa chakula bora na cha ziada.
- Kuku hawa wana uwezo wa kuhatamia mayai, kutotoa, kulea vifaranga na ustahimilivu wa mazingira magumu (ukame, baridi).
- Nyama na mayai ya kuku wa asili vina ladha nzuri sana kuliko kuku wa kisasa.
- Kwa kiasi fulani kuku wa asili wana uwezo wa kujilinda na maadui kama vile mwewe.
- Pamoja na sifa hizi ni muhimu sana kuku hawa wakapewa matunzo mazuri, wawekwe kwenye mabanda mazuri na imara, na pia wapewe maji na chakula cha kutosha.
Faida za ufugaji wa kuku wa asili
- Chakula; Kuku wa asili wanatupatia nyama na mayai ambayo hutumika kama chakula muhimu cha wanadamu, chenye protini.
- Chanzo cha kipato; Mkulima huweza kujipatia kipato kwa kuuza kuku au kuuza mayai.
- Chanzo cha ajira; Ufugaji wa kuku ni mojawapo ya ajiira kwa jamii.
- Kuku hutumika kwenye shughuli za ndoa kama vile kutoa mahari kwa baadhi ya makabila lakini pia ni kitoweo muhimu katika sherehe hizo.
- Gharama nafuu katika kuanzisha na kuendesha mradi huu.
- Kuku wa asili ni kitoweo rahisi na chepesi kwa wageni kuliko wanyama wakubwa kama ng’ombe au mbuzi na ni kitoweo kisichohitaji hifadhi kwani hutumika kwa mlo mmoja au miwili na kumalizika.
- Kuku na mayai pamoja hutumika pia kwa tiba za asili.
- Jogoo hutumika kama saa anapowika nyakati za alfajiri na katika majira mengine ya siku.
- Kuku hutuhabarisha iwapo kiumbe kingine kigeni au cha hatari kimeingia kwa mlio wake maalumu wa kuashiria hatari.
- Mbolea au kinyesi cha kuku kinaweza kutumika katika kurutubisha mashamba ya mazao na mabwawa ya samaki.
- Kuku wa asili pia hutumika katika kuendeleza kizazi cha kuku nchini.
- Soko la kuku wa asili lipo juu na la uhakika ukilinganisha na kuku wa kisasa kwani nyama na mayai yake hupendwa zaidi na walaji.
- Manyoya ya kuku wa asili hutumika kama mapambo na pia huweza kutumika kutengenezea mito ya kulalia na kukalia.
- Shughuli za utafiti zinaonyesha kuwa kuku wa asili wanatumika katika tafiti nyingi za baiolojia kama kutambua mambo ya lishe.
- Shughuli za viwandani; Mayai ya kuku wa asili yenye mbegu ya jogoo hutumika katika kutengenezea dawa za chanjo.
- Magamba ya mayai ya kuku wa asili yanweza kutumika katika kutengeneza vyakula vya wanyama.
- Kiini cha njano cha mayai ya kuku wa asili hutumika kutengenezea mafuta ya kuoshea nywele.
Mapungufu ya kuku wa asili
Kuku wa asili hutaga mayai madogo wastani wa gramu 47 ambapo kuku wa kisasa hutaga yai la wastani wa gramu 55.
Aidha, kuku wa asili hutaga mayai machache wastani wa mayai 60 kwa mwaka ambapo kuku wa kisasa huweza kutaga hadi mayai 300 kwa mwaka.
Kuku wa asili hukua taratibu kutokana na lishe duni. Kutokana na hali hii kuku huchukua muda mrefu (miezi sita) kufikia uzito wa kuchinja (kilo 1 hadi 1.5). Na hali hii pia hufanya faida ya ufugaji wa kuku wa asili kuchukua muda mrefu kupatikana.
Nyama ya kuku wa asili ni ngumu (huchukua muda mrefu kuiva) ikilinganishwa na nyama ya kuku wa kisasa.
Changamoto katika ufugaji wa kuku wa asili
Ukosefu wa mabanda yenye ubora, wezi, wanyama na ndege wengine hushambulia kuku.
Magonjwa kama vile mdondo na ndui huathiri ufugaji wa kuku.
Tabia ya miiko ya baadhi ya jamii au makabila hapa nchini ambayo huona ufugaji wa kuku kama ni kitu duni.
Upatikanaji haba wa chanjo za magonjwa kama vile mdondo, ndui na homa ya matumbo hasa katika maeneo ya vijijini.
Mifumo ya ufugaji wa kuku wa asili
Kuna mifumo mitatu ya ufugaji wa kuku wa asili inayotumika nchini Tanzania ambayo ni ufugaji huria, ufugaji nusu huria na ufugaji wa ndani na kila mfumo una faida na hasara zake.
Ni vyema mfugaji kujua mifumo yote na kisha kuchagua anaoona ni bora kulingana na mazingira yake. Hata hivyo katika kufanya uteuzi ni vyema kutilia maanani mfumo wenye faida zaidi na kuepuka mfumo wenye hasara nyingi.
Ufugaji huria
Katika mfumo huu kuku huachiwa kuanzia asubuhi wakitembea kujitafutia wenyewe chakula na maji na kufungiwa vibanda visivyo rasmi wakati wa usiku. Huu ni mfumo rahisi lakini si mzuri kwa mfugaji wa kuku wengi kwani atahitaji eneo kubwa la ardhi.
Faida za ufugaji huria
Ufugaji huu ni wa gharama ndogo kwani gharama za kujenga uzio hazihitajiki.
Gharama za chakula hupungua kwani kuku huokota wadudu na kujilia baadhi ya majani.
Hasara za mfumo huria
- Kuna uwezekano mkubwa wa kuku kuliwa na vicheChe, mwewe na wanyama wengine, kuibiwa mitaani au kukanyagwa hata na magari.
- Kuku hutaga popote na upotevu wa mayai huwa ni mkubwa.
- Katika mfumo huu kunakuwako na usimamizi hafifu wa kundi la kuku na pia ni rahisi kuku kuambukizwa magonjwa.
- Utagaji wa kuku unakuwa si mzuri kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa.
- Uwekaji wa kumbukumbu si mzuri na mara nyingi kumbukumbu si sahihi.
- Si rahisi kugundua kuku wagonjwa na utoaji wa tiba na kinga ni mgumu lakini pia vifaranga wengi huweza kufa na hata wakati mwingine kupotea.
Namna ya kuboresha mfumo huu
Kuku wajengewe banda kwa ajili ya kulala nyakati za usiku na liwasaidie wakati mwingine wowote kuwakinga na hali ya hewa inapokuwa si nzuri.
Kuku wapatiwe chakula cha ziada na maji lakini pia kuku waandaliwe viota maalumu kwa ajili ya kutagia.
Kuku 100 watumie eneo la ardhi a ekari moja ili kuwapa uwiano katika eneo.
Ufugaji nusu huria
Katika mfumo huu kuku hujengewa banda rasmi na banda hilo huzungushiwa wigo (uzio) na wigo huo hujengwa kwa mbele ambapo kuku hulala ndani ya banda nyakati za usiku na kushinda nje ya banda (ndani ya wigo)nyakati za mchana wakila chakula na kunywa maji humo.
Mfumo huu wa nusu huria ni ghali kiasi kuliko mfumo huria lakini huweza kumpatia mfugaji tija kubwa na kwa haraka sana.
Faida za mfumo huu
Sehemu ndogo ya kufugia hutumika kuliko sehemu inayotumika katika ufugaji huria na utunzaji wa kuku ni rahisi ukilinganisha na ule wa huria.
Ni rahisi kutibu na kukinga maradhi ya milipuko kama mdondo na upotevu wa kuku na mayai ni mdogo ukilinganisha na mfumo huria na pia uwekaji wa kumbukumbu ni rahisi.
Hasara zake
Mfumo huu unahitaji gharama za banda na uzio na pia gharama za chakula zitakuwa kubwa kidogo ukilinganisha na ufugaji huria.
Matumizi ya muda mrefu ya eneo husika laweza kuwa na minyoo au vimelea vingine vyovyote vya magonjwa.
Uboreshaji wa mfumo huu
Fanya usafi wa eneo husika na banda kila siku na ikiwezekana pia kuwe na mzunguko wa kutumia eneo hilo.
Muhimu: Ili mfugaji aweze kupata tija na mafanikio katika ufugaji wa kuku wa asili anashauriwa atumie mfumo huu.
Ufugaji wa ndani
Katika mfumo huu, kuku hujengewa banda rasmi na hufugwa wakiwa ndani huku wakipatiwa chakula, maji na kufanyiwa huduma nyingine muhimu wakiwa humo bandani kwa muda wote wa masha yao.
Kwa mfumo huu, kuku huwekwa kwenye mabanda ambayo sakafu hufunikwa kwa matandiko ya makapi ya mounga, takataka za mbao (randa), maganda ya karanga au majani makavu yaliyokatwakatwa.
Faida zake
- Mfumo huu unahitaji eneo dogo la kufugia hivyo ni mzuri kwenye maeneo yenye uhakika wa ardhi.
- Uangalizi wa kuku ni mzuri na rahisi na pia ni rahisi kuhakikisha ubora wa chakula.
- Hakuna haja ya kufagia vinyesi vya kuku kila siku
- Kuku wanakuwa wanakingwa na hali ya hewa na maadui wengine.
- Ni rahisi kukinga na kutibu maradhi ya kuku lakini pia uwekaji wa kumbukumbu ni rahisi.
- Ni rahisi kudhibiti upotevu wa kuku, vifaranga na mayai.
Hasara zake
- Uwezekano wa kuku kudonoana na kula mayai ni mkubwa kama utunzaji utakuwa duni
- Uwezekano wa kuku kuhatamia mayai bila mpangilio ni mkubwa
- Ujenzi wa mabanda na ulishaji una gharama kubwa na mahitaji makubwa ya nguvu kazi.
- Kuku watakosa mionzi ya jua ambayo ni muhimu sana kwa kuwapatia vitamin D.
- Ni rahisi ugonjwa kuenea haraka unapoingia kwenye kundi.
Muhimu: Kutokana na uwezo mdogo wa uzalishaji kimaumbile, kuku wa asili hawataleta tija kwa mfugaji iwapo atatumia mfumo huu.
Uboreshaji wa mfumo huu
Hakikisha utumzaji mzuri wa matandiko na usafi wa banda ili kupunguza unyevunyevu na joto kali ndani ya bandi.
Kuku wawe na nafasi ya kutosha, mita mraba moja hutosha kuku kuanzia 5 hadi 8.
Maandalizi ya ufugaji wa kuku wa asili
Ili kuweza kufuga kuku wa asili kwa faida, ni vyema kufanya maandalizi ya awali yatakayokuwezesha kuzalisha kuku walio bora.
Maandalizi hayo yanajumuisha utayarishaji wa banda kulingana na idadi ya kuku utakaowafuga, uchaguzi wa kuku bora na uandaaji wa vifaa vya kulisha na kutagia pamoja na uwiano wa kuku ndani ya banda.
Banda bora
Ni muhimu kuwajengea kuku banda bora ili wapate kujikinga na mvua, baridi, wezi na wanyama. Banda la kuku linaweza likajengwa kando kando au nyuma ya nyumba ya kuishi .
Eneo la banda la kuku liwe ni eneo ambalo; Linafikika kwa urahisi, lisituamishe maji na lisiwe na mwelekeo wa upepo mkali.
Banda la kuku linaweza kujengwa kwa kutumia rasilimali za misitu zinazopatikana kwa urahisi kwenye eneo husika. Vifaa muhimu katika ujenzi wa banda ni pamoja na miti, nyasi, mabati, makuti, fito, udongo, mabanzi, saruji na vifaa vingine mbalimbali vya ujenzi.
Kuchagua kuku wa kuendeleza kizazi
Mafanikio zaidi katika kuchagua kuku wa kuendeleza kizazi yatapatikana iwapo uchaguzi na uchambuzi wa kuku wanaozaliwa utafanywa mara kwa mara.
Sababu kubwa ya kufanya uchaguzi ni kupata kundi la kuku litakalofaa kwa sifa zote katika uzalishaji. Sifa hizo ni pamoja na kupevuka haraka, kutaga mayai mengi, kuwa na uzito mkubwa na nyama nyingi kwa umri mdogo.
Ufugaji bora utazingatia kuchagua kuku wenye sifa nzuri na kuwaacha waendelee na uzalishaji na wanaosalia wauzwe au wachinjwe waliwe.