Mara nyingi wakulima wanapuuza maswala yanayohusiana na nafya ya mimea na kupata hasara kubwa. Ikiwa mkulima hatawekeza muda na rasilimali, atakuwa na mimea iliyodhoofika.
Ni nia ya kila mkulima kuwa na mimea yenye nguvu na afya, na yenye uwezo wa kutoa mapato ya hali ya juu. Ni lazima kuwa makini na kuzingatia mbinu zitakazowezesha kufikia lengo hili. Hivyo, swala zima la afya ya mimea huanzia kwenye utayarishaji wa shamba, kurutubisha udongo, kuchagua mbegu na kudhibiti wadudu waharibifu na magonjwa.
Haya ni baadhi ya mambo ya kuzingatia ili kuweka mimea kwenye hali ya afya na kuzalisha zaidi.
Tunza udongo ili kutunza mimea
Utunzaji wa udongo unategemeana kwa kiasi kikubwa na mazingira ya kibiolojia. Kazi kubwa ya baadhi ya viumbe hai waliomo kwenye udongo, ni kumeng’enya mabaki ya mimea na viumbe hai wengine. Mtiririko huu hufanya uwepo wa nguvu, virutubisho, na hewa ya kaboni, ambavyo kwa pamoja hutengeneza rutuba kwenye udongo.
Utunzaji wa rutuba ya udongo unaongozwa na filosofia hii ‘Lisha udongo ili nao ulishe mimea.’ Udongo wenye rutuba utazalisha mimea yenye afya inayoweza kukabiliana na magonjwa.
Uzalishaji wa mazao kwa njia za asili uhakikisha kunakuwepo uzalishaji wa kutosha bila ya kutumia pembejeo za ziada isipokuwa matandazo, mboji na bila kutifua udongo mara kwa mara. Ongezeko la malighafi za asili husaidia kuimarisha udongo na kufanya kuwepo kwa virutubisho vya kutosha.
Aina ya kilimo cha kisasa na kinachotumia kemikali hufanywa tofauti na ilivyo kwa kilimo hai. Katika aina hii ya kilimo; udongo hulimwa mara kwa mara jambo linalosababisha uharibifu wa muundo wa udongo, uwiano wa virutubisho, ambapo virutubisho huongezwa kwa kutumia mbolea za viwandani na matandazo hayazingatiwi.
Muundowa udongo unapobadi-lika, rutuba nayo hupungua, uwezo wa udongo kuhifadhi maji pamoja na viumbe hai kwenye udongo pia hupungua.
Kiwango cha udongo mzuri pia hupungua kwa kuwa hakuna tena viumbe hai wanaotengeneza udongo pia inapunguza mazao kila msimu. Kwa asili mzunguko huu huwa na matokeo yanayoishia kwenye afya ya mimea, na hapa wadudu huchukua nafasi inayowawezesha kufikia malengo yao.
Usafi shambani
Ni vyema kuhakikisha kwamba shamba ni safi, haina magugu ambayo yanaweza kushindana na mimea kupata lishe na maji. Inashauriwa kufanya palizi ya mara kwa mara. Pia, Panda mimea ya msimu ikifuatana na
mimea ya msimu mfupi. Kwa, mfano, baada ya kupanda mahindi, unaweza kupanda viazi vitamu ambavyo vitasaidia kufunika udongo na kuhakisha upotevu mdogo wa maji.
Tumia wadudu rafiki dhidi ya wadudu waharibifu
Kuna baadi ya mimea kama vile nyanya ambayo wakulima wamekuwa wakitegemea sana kwa ajili ya kujipatia kipato wakati wakisubiria mazao yanayochukua muda mrefu kama vile, mahindi na mengineyo. Kwa bahati mbaya nyanya ni moja ya mazao ambayo ni rahisi sana kushambuliwa na wadudu katika mzunguko wake wa uzalishaji.
Mbali na nyanya mazao mengine ambayo ni rahisi kushambuliwa ni viazi mviringo, maharagwe, sukuma wiki, hoho, spinachi na kabichi. Madhara zaidi hutokea kunapokuwepo na upungufu mkubwa wa wadudu rafiki. Mkulima anapotumia kemikali kuulia wadudu, sumu hizo haziui wadudu waharibifu tu ila pia huuwa na wadudu rafiki ambao hutumika kudhibiti wadudu waharibifu kwa njia ya asili. Hii ndiyo sababu wadudu waharibifu wamekuwa wengi mashambani.
Tumia dawa za asili
Mojawapo ya wadudu ambao huwa wakulima hupata shida kuwadhibiti, ni inzi weupe, vithiripi, buibui wekundu, na vidukari. Wadudu hawa huharibu kati ya asilimia 20- 30 ya mazao na kuendelea. Wadudu kama vithiripi na inzi weupe ni vigumu sana kuwadhibiti kwa kuwa huzaliana kwenye mazao yanayokua. Hivyo, njia moja wapo ni kutumia njia ya kujihami badala ya wakulima kutumia kemikali, wanaweza kutumia dawa za asili ambazo haziui wadudu rafiki na ambazo pia husaidia mimea kujijengea kinga dhidi ya magonjwa.
Punguza matumizi ya kemikali
Wakulima wengi hutumia dawa za kemikali kudhibiti magonjwa na wadudu waharibifu shambani. Hata hivyo, tatizo moja kubwa la kutumia dawa za kudhibiti wadudu na magonjwa kwa kiasi kikubwa ni kuwa wadudu hao huwa sugu baada ya muda mfupi.
Hii inapelekea wakulima wengine kubuni njia hatari za kudhibiti wadudu na magonjwa. Baadhi yao hutumia dawa ya kuulia kupe kwa ajili ya kuua wadudu kama vile inzi weupe, vithiripi, utitiri na buibui. Hii ni hatari sana kwani dawa hii inaruhusiwa kutumika kwa ajili ya kuogeshea wanyama tu lakini si kwenye mboga ambazo zinauzwa kwa walaji. Hali hii inahatarisha afya ya walaji.
Pia, kuna aina nyingine za dawa ambazo ni hatari na zimepigwa marufuku na serikali, lakini maduka mengine ya pembejeo bado yanaziuza na wakulima wanatumia. Aina hizi za kemikali ni hatari sana kwa afya ya binadamu hasa zinapojikusanya kwa kiasi kikubwa mwilini. Baada ya muda mrefu inaweza kuwa sugu na kusababisha magonjwa kama saratani, ukuaji usiokuwa wa kawaida, kisukari na magonjwa ya mzio.
Mbali na madhara kwa afya ya binadamu, pia sumu hizo hupenya na kwenda kwenye maji yaliyomo ardhini na kuyachafua. Sumu hizo huathiri na kuuwa wadudu muhimu waliomo ardhini ambao huboresha udongo, kuuwa wadudu muhimu ambao hufanya ushavushaji kwenye mazao, na wadudu wengineo ambao hudhibiti wadudu waharibifu kwenye mazao na mazingira yetu. Hivyo, inashauriwa wakulima kutumia mbinu endelevu za kudhibiti wadudu na magonjwa.
Uchunguzi wa mara mara
Ni vyema mkulima kutembelea shamba lake mara kwa mara na kuangalia hali ya mimea yake. Hii inasaidia kutambua kama mimea imepata maambukizi ya magonjwa na kujua vile atapambana na hali hiyo. Huenda vijidudu vimeanza kuvamia mimea ili hali mkulima hajatambua. IKiwa mkulima atatembelea na kutazama mimea yake, basi huenda akaepukana na magonjwa na pia kuhakikisha kwamba anazuia na kutibu mimea yake kwa wakati unaofaa.
Kawaida huwa tunashauri mkulima kuwa na uhusiano na afisa wa kilimo kata. Afisa anaweza kutoa ushauri kuhusu usimamizi mzuri wa mimea na pia mipango thabiti ili kuhakikisha uzalishaji wa hali ya juu.