- Kilimo

Vuruga biocide: Kiuatilifu cha asili sasa chapatikana kwa ruzuku

Sambaza chapisho hili

Hayawi hayawi sasa yamekua. Mvumilivu, hula mbivu. Ni muda wakulima wa kilimo hai wamekua wakilalamika upatikanaji wa bidhaa za kilimo hai kwa urahisi. Serikali ya Tanzania kupitia wizara ya kilimo imepitisha kiuatilifu hai kwa jina la Vuruga.

Kiuatilifu hai (VURUGA BIOCIDE) kimetengenezwa kwa vimelea asili vya fangas (A. oryzae) kwa ajili ya kudhibiti visumbufu vya mazao shambani hasa jamii ya vipepeo (Moth). Pia kimefanyiwa majaribio kwa muda mrefu katika mikoa mbalimbali Tanzania katika kudhibiti wadudu wasumbufu wengi ikiwemo; Kanitangaze, viwavi jeshi vamizi, viwavi wanaoharibu pamba, viwavi wanotoboa matunda (maembe) na mbogamboga kama mchicha, mnavu, chainizi, kabichi na pamba.

Kiuatilifu hiki pia kimetengenezwa katika mifumo mingi inayoweza kutatua changamoto za usugu wa visumbufu.

Vuruga Biocide (VB) inafaa kutumia katika mazao ya nyanya, viazi, mahindi na mboga mboga,maua na pamba kuanzia wiki ya tatu tangu mimea kuoteshwa.

Namna ya kutumia kiuatilifu cha vuruga

  • Pima mililita 2 changanya na lita 1 ya maji safi, nyunyiza kwenye majani, shina au matunda.
  • Pima kwanza maji nusu kwenye pampu kisha weka kiuatilifu katika uwiano unaostahili, malizia kiasi cha maji kilichobaki kukamilisha ujazo wa pampu.
  • Kisha nyunyiza kwenye majani machanga ya mimea au maua au matunda machanga ili kudhibiti wadudu wanaotarajia kuharibu matunda kabla ya kukomaa.
  • Nyunyiza kiuatilifu nyakati za jioni kuanzia saa 11 jioni kwa ufanisi wa hali ya juu. Nyunyiza kiuatilifu upande wa chini ya majani au kwenye funeli ya mhindi na tumia pampu sahihi yenye nozo ya wadudu yenye matundu madogo zaidi (inayotoa maji kama mvuke).
  • Hifadhi sehemu ya utulivu nyuzi joto isiyozidi 30, weka mbali na watoto na hifadhi mbali na jua/mwanga kwa matokeo mazuri zaidi.

Matokeo ya vuruga katika majaribio katika mazao

Kiuatilifu hiki (VURUGA BIOCIDE) kimefanyiwa majaribio tangu 2016 hadi sasa katika mikoa ya Mbeya, Arusha, Manyara, Morogoro, Manyara, Dar es salaam, Pwani, Iringa na Simiyu katika kudhibiti visumbufu jamii ya viwavi; Kanitangaze na viwavi jeshi vamizi, viwavi wa pamba, chawa jani nk.

Faida zake

  • Ni cha asili (Organic)
  • Hutengenezwa kwa malighafi zinazopatikana nchini
  • Ni salama kwa binadamu, wadudu rafiki na mazingira
  • Ina ufanisi kwa asilimia 90-100
  • Huangamiza visumbufu vingi sugu vya mazao hasa Kanitangaze, viwavijeshi, wadudu wa pamba, chawa jani, viwavi wa pamba nk.
  • Kinapatikana kwa gharama nafuu ukilinganisha na viuatifu vingine
  • Kinafanya kazi tatu kwa mpigo: mbolea, kiuatilifu na huvuta wadudu rafiki katika mimea
  • Si rahisi kujenga usugu kwa wadudu, ni suluhisho la kudumu (sustainable)

Katika jitihada za serikali kuhakikisha mkulima anazalisha mazao salama, ilikulinda afya ya mmea na mlaji, pia kuzingatia uendelevu kiuatilifu hiki sasa kinapatikana kwa ruzuku. Mkulima Mbunifu imeshuhudia ugawaji wa kiuatilifu hiki kwa wakulima wilayani Babati, Mkoani Manyara.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *