- Kilimo

Unapata wapi matandazo kwa ajili ya kufunika ardhi yako

Sambaza chapisho hili

Matandazo kwa ajili ya kilimo katika msingi wa kilimo hai huweza kutokana na njia mbalimbali kama vile mazao funikizi, mabaki ya mazao, majani kutoka katika miti au vichaka na katika mimea mbalimbali.

Ikiwa matandazo yanategemewa kupatikana katika mazao funikizi, basi maandalizi ya eneo la kuoteshea na kukuzia mazao hayo ni lazima ufanyike.

Matandazo kutoka katika mazao funikizi

Baadhi ya mazao funikizi huzalisha na kuacha utando mwembamba wenye mabaki ya mimea hai na iliyokufa juu ya uso wa ardhi.

Kabla ya kuotesha zao jipya ni lazima kusafisha na kung’oa mimea hii ili kusaidia kuzuia ushindani wa virutubisho kati yake na zao utakaloliotesha.

Unaweza kuondoa mimea hii pia kwa kufyeka, kung’oa mashina kwa kutumia majembe ya kukokotwa na wanyama kazi na vifaa kama vile trekta na baadaye kuyatandaza juu ya uso wa ardhi kisha kuotesha zao jipya juu ya matandazo hayo.

 

Matandazo kutoka katika mabaki ya mazao

Mazao mbalimbali yanayooteshwa kwa msimu kama vile mahindi ni chanzo kikubwa cha matandazo mara baada ya kuvuna.

Kitu cha kufanya ni kuvuna kwa kukata mabua kisha kuyalaza chini kufunika udongo na ikiwa hukuotesha mazao funikizi mabua haya yanatosha kuwa chanzo kizuri cha kurutubisha udongo.

Katika maeneo ambayo ni kame na hayana maji ya kutosha kuotesha mazao funikizi hasa kipindi cha kiangazi, njia ya kuacha mabaki ya mazao mara baada ya kuvuna kama matandazo ndiyo pekee inayofaa katika maeneo haya.

Wakulima katika maeneo mbalimbali huondoa kabisa masalia a mabaki ya mazao baada ya kuvuna kwa ajili ya kulishia mifugo na wakati mwingine huruhusu mifugo kuingia katika shamba kwa ajili ya kujilia masalia hayo jambo ambalo hupelekea uharibifu katika ardhi.

Namna ya kulinda uharibifu wa ardhi

Mara baada ya kuvuna, jitahidi kuacha mabaki mengi ya mazao shambani kwa ajili ya kutumika kama matandazo na ikiwa utahitaji kwa ajili ya kulisha mifugo, basi chukua kiasi kidogo tu cha mabaki yenye ubora na acha mengine kwa ajili ya kufunika uso wa ardhi.

Zuia uchungaji wa mifugo katika shamba ili kusaidia kutokuharibu rutuba ya udongo pamoja na kuzuia kula mabaki yote ya mazao.

Tumia vyanzo vingine vya ulishaji wa mifugo kama kujitengea eneo maalumu kwa ajili ya kuotesha majani na kulisha mifugo yako.

Matandazo kutoka kwenye miti na vichaka

Miti na vichaka hutoa majani mengi ambayo huweza kutumika kama matandazo katika kilimo na wakati huo huo huweza kutumika kwa ajili ya kulishia mifugo.

Wakulima wanaweza katika miti au vichaka gani wanaweza kupata matandazo kwa ya kilimo na kufunika udongo. Kuna aina mbalimbali ya miti na vichaka vyenye kutoa matandazo yanayofaa kama yafuatayo;

Miti yenye matumizi mbalimbali; Baadhi ya miti huwa na matumizi mbalimbali kama vile kuzalisha mbao, matunda, lishe kwa wanyama na hata malazi.

Katika aina hii ya miti, mkulima anaweza kupunguza matawi au majani yake na kusambaza katika shamba lake kama matandazo.

Miti ya fensi; Miti hii ambayo huoteshwa kwa ajili ya kuweka uzio na ambayo mara nyingine hutumika kama malisho ya mifugo, kuni wakati huohuo huweza kupunguzwa na kutumika kama matandazo.

Vichaka jamii ya mikunde; Vichaka jamii ya mikunde kama vile gliricidia hutengeneza rutuba kwa kuongeza naitrojeni katika udongo na unaweza kupanda kwa mzunguko wa mahindi au mtama kisha kukata na kutumia katika matandazo.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *