Wakulima wengi hutumia dawa za kemikali kudhibiti magonjwa na wadudu waharibifu shambani. Hata hivyo, tatizo moja kubwa la kutumia dawa za kudhibiti wadudu na magonjwa kwa kiasi kikubwa ni kuwa wadudu hao huwa sugu baada ya muda mfupi.
Hii inapelekea wakulima wengine kubuni njia hatari za kudhibiti wadudu na magonjwa. Baadhi yao hutumia dawa ya kuulia kupe kwa ajili ya kuua wadudu kama vile inzi weupe, vithiripi, utitiri na buibui. Hii ni hatari sana kwani dawa hii inaruhusiwa kutumika kwa ajili ya kuogeshea wanyama tu lakini si kwenye mboga ambazo zinauzwa kwa walaji. Hali hii inahatarisha afya ya walaji.

Pia, kuna aina nyingine za dawa ambazo ni hatari na zimepigwa marufuku na serikali, lakini maduka mengine ya pembejeo bado yanaziuza na wakulima wanatumia. Aina hizi za kemikali ni hatari sana kwa afya Picha:IN ya binadamu hasa zinapojikusanya kwa kiasi kikubwa mwilini. Baada ya muda mrefu inaweza kuwa sugu na kusababisha magonjwa kama saratani, ukuaji usiokuwa wa kawaida, kisukari na magonjwa ya mzio.
Mbali na madhara kwa afya ya binadamu, pia sumu hizo hupenya na kwenda kwenye maji yaliyomo ardhini na kuyachafua. Sumu hizo huathiri na kuuwa wadudu muhimu waliomo ardhini ambao huboresha udongo, kuuwa wadudu muhimu ambao hufanya ushavushaji kwenye mazao, na wadudu wengineo ambao hudhibiti wadudu waharibifu kwenye mazao na mazingira yetu. Hivyo, inashauriwa wakulima kutumia mbinu endelevu za kudhibiti wadudu na magonjwa.
Uchunguzi wa mara mara
Ni vyema mkulima kutembelea shamba lake mara kwa mara na kuangalia hali ya mimea yake. Hii inasaidia kutambua kama mimea imepata maambukizi ya magonjwa na kujua vile atapambana na hali hiyo. Huenda vijidudu vimeanza kuvamia mimea ili hali mkulima hajatambua. IKiwa mkulima atatembelea na kutazama mimea yake, basi huenda akaepukana na magonjwa na pia kuhakikisha kwamba anazuia na kutibu mimea yake kwa wakati unaofaa.
Kawaida huwa tunashauri mkulima kuwa na uhusiano na afisa wa kilimo kata. Afisa anaweza kutoa ushauri kuhusu usimamizi mzuri wa mimea na pia mipango thabiti ili kuhakikisha uzalishaji wa hali ya juu.




