Mahindi ni zao la kwanza katika mazao makuu ya nafaka hapa nchini. Huzalishwa kwa wastani wa tani 2393000 kwa mwaka ambayo ni sawa na asilimia 63 ya mazao yote ya nafaka nchini.
Zao la mahindi hulimwa karibu katika mikoa yote, lakini hulimwa zaidi katika mikoa ya Rukwa, Ruvuma, Iringa, Mbeya, Morogoro, Dodoma, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Tanga, Mwanza na Shinyanga.
Licha ya kuwa zao hili ni la chakula, vilevile hutumika kama zao la kibiashara.
Katika kipindi hiki cha mavuno, wakulima hawana budi kuwa makini sana na kutambua ni kwa namna gani watavuna mazao yao na kuyahifadhi ili kuondokana na upotevu ambao mara nyingi hufikia hadi asilimia 20 hadi 30 ya mavuno.
Nini husababisha upotevu wa mavuno
Upotevu huu unasadikika kutokana na wakulima wengi kuyaacha sehemu ya mazao shambani kutokana na kushindwa kuyadhibiti na wakati mwingine kupotea njiani wakati wa kupeleka au wakati wa kuhifadhi.
Aidha, upotevu mwingine hutokea wakati wa kuhifadhi kulingana na aina ya vifaa vinavyotumika kuhifadhia kuwa na urahisi wa kuharibiwa na wadudu na mengine kuoza kutokana na unyevu.
Wakati mwingine wakulima huvuna mazao yakiwa bado hayajakomaa vizuri hivyo kukosa ujazo mzuri unaoshauriwa kitaalamu katika uhifadhi wa zao hili.
Maandalizi kabla ya kuhifadhi
Kabla ya kuvuna ni muhimu kuandaa vifaa vya kuvuna na kukagua shamba ili kujua kama mahindi yamekomaa vizuri. Kwa kawaida mahindi hukomaa kati ya miezi 3 hadi 8 kutegemeana na aina na hali ya hewa. Unyevu katika punje huwa kati ya asilimia 23 hadi 28.
Dalili za mahindi yaliyokomaa
- Rangi ya majani ya mmea wa mhindi na maganda ya gunzi hugeuka kutoka ukijani na kuwa ya kaki.
- Sehemu iliyounganisha punje na gunzi huwa nyeusi na punje ya mhindi hung’ara
Matayarisho kabla ya kuvuna
Vifaa vya kuvunia na kubebea mahindi ni pamoja na Vikapu, Matenga, Mapanga, Magunia, Mashine (combine harvest) kwa wakulima wenye mashamba makubwa.
Vyombo vya usafiri
Mkulima ni lazima kuandaa vyombo kwa ajili ya kusafirishia mahindi kutoka shambani hadi nyumbani/ghalani. Vyombo vya kusafirishia ni kama mikokoteni inayokokotwa na wanyamakazi au ya kusukumwa/kuvutwa na mikono, matela ya trekta pamoja na magari.
Vifaa na sehemu ya kukaushia
Hivi ni pamoja na kichanja bora/chekeche, mikeka, maturubai, sakafu safi, na ghala safi la kuhifadhia.
Kuvuna
Ni muhimu kuvuna mapema ili kuepuka upotevu wa mahindi unaoweza kusababishwa na waduduna wanyama waharibifu, moto, wezi na mvua.
Njia za kuvuna
Njia zinazotumika kuvuna mahindi ni kwa kutumia mikono au mashine.
Kuvuna kwa mikono: Hii njia hutumiwa na wakulima ambao wana mashamba madogo na uwezo wao kupata mashine ni mdogo pia. Mashina ya mahindiyaliyokomaa hukatwa kwa paanga, na kurundikwa mahali pamoja kisha magunzi ya mahindi huondolewa kwenye mashina kwa kutumia mikono.
Kuvuna kwa mashine: Njia hii hutumiwa na wakulima wenye uwezo na mashamba yao ni makubwa. Mashine hukata mashina ya mahindi yaliyokauka, kuyamenya na kupukuchuwa kwa wakati mmoja. Punje za mahindi humiminwa kwenye chombo tayari kwa kusafirishwa hadi sehemu ya kusafisha na kufungasha.
Kusafirisha
Mahindi husafirishwa kutoka shambani hadi sehemu ya kukaushia kwa kutumia, matoroli, kubeba kichwani, kutumia baiskeli, kutumia wanyamakazi kama punda, kutumia mikokoteni ya wanyamakazi, kutumia mateka ya trekta pamoja na magari.
Kukausha
Ili kupunguza upotevu na kudumisha ubora, ni muhimu kuzingatia njia bora za kukausha mahindi.
Hatua ya kwanza: Huu ni ukaushaji wa awali ambao hufanyika mara tu mahindi yanapotolewa shambani. Ukaushaji huu hufanyika kwa kuyaweka magunzi ya mahindi juu ya turubai, kichanja, sakafu, au kribu. Lengo la kukausha magunzi ni kupunguza unyevu na kurahisisha upukuchuaji.
Upukuchuaji
Hatua hii hujumuisha upukuchuaji wa mahindi kabla ya kufungasha au kuhifadhi. Mahindi ambayo hayajapukuchuliwahushambuliwa zaidi na wadudu waharibifu hasa dumuzi kuliko yaliyopukuchuliwa. Pia si rahisi kufahamu kiwango cha mahindi ambacho mkulima anacho yakiwa kwenye magunzi.
Kabla ya kuanza kupukuchua, ni muhimu kuchunguza na kutoa mahindi ambayo tayari yameshaanza kuoza au kuwa na wadudu. Mahindi yanaweza kupukuchuliwa kwa kutumia mikono, mashine, kichanja maalum, au kutumia magunia kisha kupiga.
Kupepeta na kupembua
Kazi ya kupepeta hufanyika ili kuondoa takataka kama vile magunzi, mawe, wadudu, punje zilizooza, kuharibika au kupasuka. Kazi hii inaweza kufanyika kwa kutumia mikono, chekeche mashine.
Hatua ya pili
Hatua hii hujumuisha ukaushaji wa pun je hadi kufikia unyevu unaokubalika kwa kuhifadhi salama ambao ni asilimia 13.5. Iwapo kiwango kitakuwa chini ya hapo, basi mahindi hushambuliwa kwa urahisi sana na vimelea vya ukungu, na kusababisha kuoza.
Ukaushaji huu hufanyika kwa kusambaza punje za mahindi kwenye sehemu yeyote iliyo safi ili kuhakikisha kuwa punje hizo zinakaukabila kuingiliwa na uchafu tena.
Jinsi ya kutambua punje za mahindi zilizokauka
Utambuzi huu unaweza kufanyika kwa kupima unyevu kwa njia kuu nne ambazo ni:
- Kung’ata punje: Huwa magumu na hukatika kwa mlio mkali.
- Kumimina kwenye chomboau sakafu: Hutoa mlio mkali kama wa kuumiza sikia.
- Kutumia chumvi: Changanya mahindi na chumvi kiasi kisha mimina kwenye jagi la kioo, na kama chumvi itang’ang’ania kwenye punje basi hazijakauka.
- Kutumia kipima unyevu : Kuonyesha unyevu wa asilima 13.5.
Kutayarisha mahindi kabla ya kuyahifadhi
Kabla ya kuweka mahindi kwenye vifungashio au kuhifadhi ghalani, inabidi kuchukua tahadhari ya kuzuia uharibifu utokanao na wadudu au wanyama kama panya ndani ya ghala.
Hakikisha gahala la kuhifadhia mahindi ni safi, lisilovuja na ikibidi changanya mahindi na viuwadudu. Viuwadudu hivyo vinaweza kuwa ni viwe vya asili vinavyotokana na mimea kwa mfano muwarobaini au pareto. Aidha ni muhimu kutenga kiasi cha mahindi yatakayotumika kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu baada ya kuvuna. Hii ni kwasababu katika kipindi hiki, mashambulizi ya wadudu huwa ni ya kiwango cha chini sana.
Kuchanganya kiuwadudu na nafaka
Wakati wa kuchanganya kiuwadudu na nafaka ni muhimu kuandaa vifaa kama vile, turubai isiyokuwa na matundu, sakafu safi ya sementi, debe la kupimia nafaka, beleshi au koleo, dawa ya kuhifadhia na kifaa au kitambaa safi cha kufunika pua na mdomo.
Hatua za kuchanganya
- Tandika turubai safi kwenye sakafu katika sehemu isiyokuwa na upepo.
- Pima nafaka kwa kutumia debe au kwa kutumia mizani ili kupata uzito wa kilogramu 100 (madebe sita)
- Weka nafaka kwenye turubai na funika pua na mdomo kwa kitambaa safi ili kuzuia dawa isiingie mwilini.
- Fungua pakiti ya gramu 200 ya dawa ya asili na mimina juu ya kilo 100 za nafaka.
- Anza kuchanganya dawa na mahindi kwa kutumia beleshi au koleo mpaka mahindi yote yatakapopata dawa.
- Fungasha kwenye magunia safi ya kilo 100 tayari kwa kuhifadhi ghalani au waweza kuhifadhi kwenye kihenge, silo au bini.
- Mahindi yapangwe kimadaraja kwenye ghala. (Maguniua yasiwekwe moja kwa moja sakafuni, mbao huweza kutangulizwa sakafuni kwanza).
Ghala bora la kuhifadhia mahindi
Ghala bora ni chombo chochote kile au jengo lolote lililo imara na lenye sifa zifuatazo;
- Liwe na uwezo wa kuzuia wadudu, panya, mvua na unyevu kutoka chini.
- Liwe na nafasi ya kutosha kuweka mazao, kukagua na kutoa.
- Liwe na uwezo wa kuhifadhi mazao yaliyokusudiwa.
Aina ya maghala bora
- Kihenge
Hii hujengwa kwa kutumia vifaa kama vile matete, mianzi, miti au fito nyembamba na kusiribwa ndani na nje kwa udongo, sementi na samadi. Paa la kihenge huezekwa kwa kutumia nyasi, makuti au bati.
- Sailo au bini
Haya ni maghala yanayojengwa kwa dhana ya kutokuwepo na mzunguko wa kawaida wa hewa ndani ya mahindi yaliyohifadhiwa na kusababisha wadudu waharibifu na vimelea vya magonjwa kutoweza kusitawi na kuharibu mahindi.
- Mapipa
Mapipa yenye mifuniko imara hutumika kuhifadhi mahindi kwa dhana ya kutokuwa na hewa ndani ya mahindi. Pipa likijazwa mahindi na kufungwa sawasawa hakuna hewa inayoingia na hakuna mdudu anayeweza kuishi ndani yake, na hata punje za mahindi hufa baada ya kuhifadhiwa kwa muda hivyo inashauriwa kuwa mahindi yanayotegemewa kwa ajili ya mbegu isihifadhiwe ndani ya pipa.
- Maghala ya nyumba
Hifadhi hii hufanyika katika chumba au nyumba maalumu na maghala haya huhifadhi mazao yaliyofungashwa kwenye magunia. Uwezo wa kuhifadhi hutegemea wingi wa mazao.
Hello
Habari,
Karibu sana Mkulima Mbunifu nasi tuko tayari kukuhudumia kwa maswali yeyote