- Kilimo

Msomaji wa jarida la MkM atoa ushauri kwa wafugaji wa kuku

Sambaza chapisho hili

Moja ya kazi inayofanywa na Mkulima Mbunifu katika kufikisha elimu kwa wakulima, ni kutumia ujuzi na uzoefu wa wakulima na wafugajhi wengine katika kuelimisha na kushirikisha namna mbalimbali wanavyofanya na kufanikiwa katika kazi zao za uzalishaji.

MkM

Huu ni ushauri kutoka kwa mmoja wa wasomaji wa jarida la Mkulima Mbunifu kwa wafugaji wa kuku.

“Naitwa Nicodemus Nzenga, ni mmoja kati ya wasomaji wazuri wa jarida lenu. Nashukuru na kuwapongeza, kwani jarida linaelimisha na kutoa mbinu mbadala za kuinua maisha ya wakulima wadogo.

Mimi ni mfugaji mdogo wa kuku wa asili mwenye uzoefu wa kiasi wa shughuli hizi. Nadhani haitakuwa vibaya nikitumia muda huu kubadilishana mawazo na wafugaji wenzangu kuhusu vifo vya vifaranga na nini kisababishi?’’

Ufugaji holela: Vifaranga wanatumia muda mrefu kukimbizana na mama yao kutafuta chakula na hivyo kupata misukosuko mingi kama ajali, wanyama, ndege na hata kupotezana na mama yao.

Suluhisho: Wafungwe katika chumba maalumu au wapumzishwe kadri inavyowezekana kwani hata chakula wanachopata wanakitumia kutembea na kukimbizana na mama yao badala ya kujenga miili yao.

Magonjwa: Vifaranga wanapototolewa tu huambukizwa magonjwa kwani hukumbana na maeneo ambayo tayari yalishachafuliwa na kuku wakubwa. Mbaya zaidi ni kwamba kuna magonjwa ambayo wanaweza kutoka nayo katika yai hivyo huwachukua wiki mbili tu na kuanza kufa.

Suluhisho: Viranga wapewe antibiotics ndani ya siku saba za uhai wao ili kuepuka magonjwa ya bakteria.

Ikumbukwe kwamba uwezo wa kuku wakubwa kuvumilia magonjwa ni mkubwa kuliko wa vifaranga, hivyo wakifugwa pamoja vifo hutokea kwa magonjwa na hata kuuwawa na kuku wakubwa/majogoo wasiopenda vifaranga.

Suluhisho: Ni vyema viranga wakatengwa na kuku wakubwa.

Upungufu wa vitamin A: Hili ni tatizo kubwa hasa wakati wa kiangazi ambapo hakuna uoto wa kutosha na pia uwezo wa vifaranga kula majani ni mdogo hivyo vifo vingi vinatokea kwa upungufu wa vitamin A bila hata ya kuonyesha dalili yoyote.

Suluhisho: Vifaranga waanze kupewa Vitamin A siku ya kwanza kwa kufuata maelezo ya watengenezaji wa vitamin hiyo.

Wadudu: Utitiri, viroboto na wadudu wengine washambuliao kuku viranga hutotolewa na kukumbana na wadudu hao toka siku ya kwanza tu na unaweza ukakuta wengine wanashindwa kutoa hata sauti na vifo hutokea.

Suluhisho: Kuku wanapoanza kuhatamia waandaliwe kwa kuwekewa viota safi na dawa za kuua wadudu hao ili vifaranga watotolewe katika mazingira safi yasiyokuwa na wadudu hao.

Unyevu: Kuku anaweza akakumbatia vifaranga wake lakini chini kukawa na unyevu au baridi hivyo lengo la kuvipatia joto halitatimia.

Suluhisho: Hakikisha banda ni safi na halina unyevu wala uchafu wa aina yoyote ile.

Nicodemus Nzenga, Msimamizi wa Upendo nyuki group, niconzengatz2@gmail.com

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *