- Kilimo

Mnyororo wa Kilimo Ikolojia

Sambaza chapisho hili

Kilimo ikolojia ni mfumo wa ukuzaji wa mimea au mifugo kwa njia jumuishi inayowezesha kufikia ustawi wa kijamii kimahitaji, kimazingira na kiuchumi. Inatafuta kuboresha mwingiliano kati ya mimea, wanyama, binadamu na mazingira.

Kupitia mfumo huu wa kilimo ikolojia, jamii inajihakikishia usalama wa chakula na utunzaji wa mazingira. Mfumo huu licha ya kuhakikisha usafi na usalama wa vyakula lakini pia unatusaidia katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi. Hivyo kupitia mfumo wa kilimo ikolojia tunalenga kulinda na kuhifadhi maziringa na kuongeza ufanisi katika uzalishaji kwa kutumia rasilimali zinazomzunguka mkulima kwa gharama nafuu hivyo kuboresha kipato na ustawi wa mkulima.

Mbinu zinazotumika katika kutekeleza kilimo ikolojia

  • Mzunguko wa mazao: Mbinu hii hutumia kukabiliana na magonjwa na wadudu au visumbufu vya mimea na kuimarisha afya ya udongo. Kwa kutumia mbinu hii mkulima hatahitaji kupuliza viuatilifu hatarisha kwa mimea na mazingira kwa ujumla na hivyo kujihakikishia usafi na usalama wa chakula kwa wote.
  • Kilimo mesto: Mbinu hii ya kulima mazao au mimea mbalimbali kwenye shamba moja ili kuongeza bayoanuai, kipato kwa mkulima, kuthibiti wadudu na kuimarisha au kuongeza virutubisho kwenye udongo. Mfano kuchanganya mahindi na maharage au mbaazi. Kwa kutumia mbinu hii, inaleta uhimilivu wa kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
  • Udhibiti wa magugu kwa njia za asili: Mfumo wa kilimo ikolojia inahimiza sana kutumia mbinu za asili kwenye kudhibiti magugu mashambani. Mkulima anaweza kupalilia kwa mkono, kutumia matandazo ya asili kama vile nyasi au masalia ya mimea au kutumia mazao funika ambayo huzuia ukuaji wa magugu. Mkulima unaweza kutumia mazao funika kama vile fiwi.
  • Matumizi ya mbolea za asili: Kilimo ikolojia kinajikita katika kujenga afya ya udongo kwa uzalishaji endelevu. Mbolea za asili ni kama vile samadi, mboji na mbolea ya kijani.
  • Matumizi ya wadudu rafiki wenye manufaa na mimea yenye kufukuza wadudu kwa harufu: Kilimo ikolojia ni mfumo uliojitosheleza, hutunza bioanuai hivyo kukuza na kulinda uwepo wa wadudu wenye manufaa ambao husaidia kukabilina na wadudu waharibifu. Pia mkulima anaweza kutumia mimea kama vile bangi pori, mchaichai na baadhi ya viungo kufukuza wadudu kwenye bustani yake na kupata mbogamboga salama.
  • Matumizi ya viuatilifu vya asili: Mbinu hii hutumiwa na wakulima kwenye mapambano ya magonjwa na wadudu waharibifu. Mkulima anaweza kutengeneza dawa ya asili ya kupuliza shambani kwake kwa kutumia rasilimali zinazomzunguka. Mfano kuchanganya majani ya mti wa mwarobaini, alizeti pori na kitunguu swaumu.
  • Uhifadhi wa maji na udongo: Sote tunafahamu umuhimu wa maji kwenye ukuaji wa mazao au mimea mbalimbali. Kilimo ikolojia inahimiza kutumia mbinu za kuhifadhi au uvunaji maji mashambani kwa kutumia makingamaji ya fanya juu na fanya chini. Pia mkulima anaweza kutumia mfumo wa umwagiliaji kwa njia ya matone ambao huongeza ufanisi na tija kwenye kilimo. Mbinu hii inasaidia kupunguza mmomonyoko wa udongo na kudhibiti upotevu wa rubuta mashambani.

Hivyo mkulima yeyote anaweza kufuata mbinu hizo za kilimo ikolojia katika uzalishaji wake. Ili mkulima aweze kutekeleza mbinu hizo ni dhahiri kuwa lazima kuwepo na uhusiano wa moja kwa moja baina ya shughuli za kilimo na ufugaji na kutegemeana.

Siyo lazima mkulima awe na shamba kubwa ili aweze kutekeleza, bali hata kwenye shamba dogo mkulima anaweza kujipatia chakula safi na salama.

Kwenye mahusiano haya mkulima atakusanya na kupeleka mbolea kutoka kwa wanyama shambani ili kuongeza rutuba ya udongo, uzalishaji. Mifugo hutegemea malisho kutoka shambani (mabaki ya mazao kama vile mabua na majani), Mkulima hupata chakula safi na salama kutoka shambani hivyo kunakuwa na mnyororo wa kutegemeana.

Kwanini mnyororo wa kilimo ikolojia

Katika kilimo ikolojia, tunazungumzia wanyama, mimea, binadamu, na mazingira. Hivyo huu ni mnyororo mzima unaotegemeana kwa namna ifuatayo;

  • Binadamu: Mkulima anapozalisha mazao na kufuga, anategemea kupata lishe kamili itokanayo na mazao yote ya mifugo na kilimo kama nyama, mayai, mboga, nafaka. Hii ataipata tu endapo atafanya kilimo ikolojia itakayompa mazao bora, mengi na salama kwa ajili ya afya yake.
  • Wanyama: Wanyama wanaofugwa na hata wasiofugwa wanategemea kupata lishe kamili kama majani, maji safi na salama hivyo kupitia kilimo ambacho binadamu anafanya ataweza kuzalisha chakula cha kutosha kwa ajili ya mifugo yake.
  • Mazingira: Tunapozungumzia mazingira tunajumuisha kwanza udongo ambao ndiyo kiini cha uzalishaji na ili kuwa na udongo wenye rutuba tunategemea mbolea kutoka kwa wanyama, masalia ya mimea pamoja na masalia ya taka za nyumbani zinazozalishwa na binadamu.
  • Mimea: Ili kuzalisha mimea bora na salama ni lazima kuhakikisha kunakuwepo na binadamu ambaye ndiye mzalishaji na upatikanaji wa udongo wenye rutuba ambao unategemea mbolea za wanyama, pamoja na masalia ambayo hutengeneza mboji. Hii ina maanisha kuwa ni lazima vitu vyote hivi vitegemeane katika kilimo ikolojia na ndiyo ikolojia yenyewe.

Kwa kuhitimisha kilimo ikolojia kina faida mbalimbali kwa mkulima na jamii kwa ujumla kama ifuatavyo;

  • Kukuza kipato cha mkulima: Mbinu hizi za kilimo cha kiikolojia kuhuza kipato cha mkulima kwa namna mbalimbali. Mkulima atazalisha kwa gharama ndogo na kupata faida kubwa kutoka kwenye shughuli za kilimo na ufugaji anaofanya. Kipato cha ziada mkulima anaweza kutumia kusomesha watoto, kujenga nyumba bora na kuanzisha miradi mbalimbali.
  • Uhifadhi wa mazingira: Kilimo ikolojia kinatekelezwa kwa kujali mazingira ya uzalishaji kwa kutokutumia viwatilifu vya kikemikali, lakini kudhibiti mmomonyoko wa aridhi na kuhifadhi rutuba ya udongo ili uwezeshe uzalishaji’
  • Kulinda Afya ya binadamu: Kutokutumia dawa za kemikali katika shughuli za uzalishaji na uhifadhi wa mazao mfano kupalilia, kufukuza wadudu na kukabiliana na magonjwa lakini hata kuhifadhi mazao baada ya mavuno. Vyakula vinavyozalishwa kwa mfumo huu wa kiikolojia ni safi na salama kwa afya za walaji hivyo kupunguza gharama za matibabu na kuwa wa nguvu kazi itakayotumia kwenye shughuli zingine za uzalishaji.

Kwa mawasiliano zaidi wasiliana na MVIWA Arusha kwa simu namba 0754 818 355.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *