Usafi shambani
Ni vyema kuhakikisha kwamba shamba ni safi, haina magugu ambayo yanaweza kushindana na mimea kupata lishe na maji. Inashauriwa kufanya palizi ya mara kwa mara. Pia, Panda mimea ya msimu ikifuatana na mimea ya msimu mfupi. Kwa, mfano, baada ya kupanda mahindi, unaweza kupanda viazi vitamu ambavyo vitasaidia kufunika udongo na kuhakisha upotevu mdogo wa maji.

Tumia wadudu rafiki dhidi ya wadudu waharibifu
Kuna baadi ya mimea kama vile nyanya ambayo wakulima wamekuwa wakitegemea sana kwa ajili ya kujipatia kipato wakati wakisubiria mazao yanayochukua muda mrefu kama vile, mahindi na mengineyo. Kwa bahati mbaya nyanya ni moja ya mazao ambayo ni rahisi sana kushambuliwa na wadudu katika mzunguko wake wa uzalishaji.
Mbali na nyanya mazao mengine ambayo ni rahisi kushambuliwa ni viazi mviringo, maharagwe, sukuma wiki, hoho, spinachi na kabichi. Madhara zaidi hutokea kunapokuwepo na upungufu mkubwa wa wadudu rafiki. Mkulima anapotumia kemikali kuulia wadudu, sumu hizo haziui wadudu waharibifu tu ila pia huuwa na wadudu rafiki ambao hutumika kudhibiti wadudu waharibifu kwa njia ya asili. Hii ndiyo sababu wadudu waharibifu wamekuwa wengi mashambani.
Tumia dawa za asili
Mojawapo ya wadudu ambao huwa wakulima hupata shida kuwadhibiti, ni inzi weupe, vithiripi, buibui wekundu, na vidukari. Wadudu hawa huharibu kati ya asilimia 2030 ya mazao na kuendelea. Wadudu kama vithiripi na inzi weupe ni vigumu sana kuwadhibiti kwa kuwa huzaliana kwenye mazao yanayokua. Hivyo, njia moja wapo ni kutumia njia ya kujihami badala ya wakulima kutumia kemikali, wanaweza kutumia dawa za asili ambazo haziui wadudu rafiki na ambazo pia husaidia mimea kujijengea kinga dhidi ya magonjwa.




