Upatikanaji wa mazao bora hutegemea matumizi ya aina na ubora wa mbegu za mazao husika. Baadhi ya wakulima nchini Tanzania wamesahau matumizi ya mbegu za asili na kujikita zaidi katika mbegu za kisasa.
Mbegu ni nini?
Mbegu ni sehemu ya mmea ambayo mmea mpya unaweza kuota.
Kuna makundi makuu mawili ya mbegu ambayo ni;
Punje: Kama vile nafaka au mbegu za matunda, ambazo kawaida huzalishwa kwa uchavushaji, na zina kiini na chakula chake huhifadhiwa ndani ya ganda gumu la mbegu.
Shina/mizizi: Kama vile mihogo na viazi.
Upatikanaji wa mbegu
Mbegu hupatikana katika mfumo rasmi na mfumo wa asili (yaani mfumo usio rasmi). Aidha, mifumo hii hutegemeana kwani yote ni muhimu sana kwa masuala yanayaohusu upatikanaji, uhakika na usalama wa mbegu.
- Mfumo rasmi wa uzalishaji mbegu hutumia mbegu zilizozalishwa na mfumo wa asili wakati wa kuboresha viini asilia kisayansi.
- Mfumo usio rasmi yaani mfumo wa asili wa uzalishaji mbegu wenyewe hutegemea mbegu zilizochaguliwa kwa uangalifu mkubwa sana na mkulima kutokana na mavuno yaliyo tangulia, alizopewa na Jirani yake ama zile zilizozalishwa na wakulima wadogo wanaozalisha mbegu.
Mbegu za asili
Hizi ni mbegu za mazao zilizokuwepo Mbegu za asili Hizi ni mbegu za mazao zilizokuwepo tangu awali. Mbegu hizi hutegemewa sana na wakulima wadogo hasa vijijini. Mbegu hizi zinaundwa na viini asilia vinavyoziwezesha kuendelea kuzaliana na kuhimili mazingira, tabia na namna tofauti kwa wakati tofauti.
Kwa mujibu wa sensa ya kilimo Tanzania ya mwaka 2007/2008, mfumo wa uzalishaji wa mbegu kwa njia asilia huchangia kiasi cha asilimia 83 ya upatikanaji wa mbegu kwa wakulima wadogo wa Tanzania. Aidha, mfumo huu umewezakudumisha na kuendeleza teknolojia na ubunifu wa kuzizalisha, kuzitumia na kuzitunza mbegu hizi kutoka familia moja na nyingine na kizazi kimoja hadi kingine.
Faida za kutumia mbegu za asili
Kuna faida nyingi za kutumia mbegu za asili kwa mkulima mmoja mmoja na hata kwa jamii nzima. Hizi ni pamoja na;
- Mbegu za asili hupatikana kwa urahisi kwani hupatikana kwa wakulima wenyewe.
- Mbegu za asili zinaweza kutumika kwa misimu mingine ya mbele, iwapo itachambulliwa na kutunzwa vizuri kwani zina uwezo wa kuzalisha mazao mengi hata kwa misimu mingine. Tofauti na mbegu za kisasa ambazo zikitumika msimu mmoja, msimu unaofuata mavuno hupungua kwa kiasi kikubwa. Hivyo, inamgharimu mkulima kununua mbegu mpya kwa kila msimu.
- Mbegu za asili hutumia pembejeo kidogo na za asili ukilinganisha na mbegu za kisasa. Hii ni kutokana na uwezo wake wa kumudu changamoto za kilimo.
- Mbegu za asili huhimili mabadiliko ya tabia nchi, magonjwa na wadudu washambuliao mazao.
- Wakati mwingine mazao yanayotokana na mbegu za asili hutumika kupambana na magonjwa mbalimbali. Kwa kwa mfano, maharage ya jesca yanasaidia katika kurudisha kumbukumbu akilini.
- Mazao ya mbegu nyingi za asili huwa na soko na bei yake pia ni nzuri.
- Mbegu nyingi za asili zikitumiwa kama chakula huwa na ladha nzuri kutokana na uasili wake.
Haki za wakulima katika kutunza mbegu za asili
- Kwa vizazi vingi na miaka mingi kote duniani, wakulima wamekuwa wakitunza mbegu zao kupitia njia na mbinu mbalimbali ambazo ziliwawezesha kuwa na uhakika wa mbegu kwa msimu unaofuata.
- Njia na mbimu hizo ni pamoja na kuzizalisha, kutunza kwa njia za asili, kubadilishana au kuuza.
- Mbinu na utamaduni huu umerithishwa kutoka kizazi hadi kizazi kwa lengo la kutunza mbegu hizo kwa uendelevu. Hivyo, wakulima wana haki ya kutunza mbegu zao za asili ili kulinda chaguo la wakulima, kudumisha anuai za kilimo, kudumisha bioanuai asili.
Kwa maelezo zaidi wasiliana na Daudi Manongi Mtaalamu wa mbegu asili kutoka Tanzania Biodiversity Alliance Organisaion (TABIO) kwa namba 0769 86 10 63