Mkulima ni mfanyabiashara, na mfanyabiashara yeyote analenga faida kubwa au hasara kidogo sana. Ni muhimu kwa mkulima kujua thamani ya mazao yake ili aweze kujua ni bei gani anayotakiwa kuuzia mazao yake lakini pia ajue bei ambayo akiuza kwayo itamletea hasara.
Unapoanzisha mradi wa kilimo biashara, unatarajia mwisho wa siku umalizike kwa kupata faida. Kuna mambo mawili makubwa miongoni mwa mambo kadha wa kadha unayotakiwa kuyajua kabla hujaanza mradi wowote wa kilimo. Mambo hayo ni;
- Mpango mkuu wa kilimo (Farming master-plan)
Katika kilimo biashara, hili ni jambo la kwanza na muhimu kulifahamu. Farming master-plan ni muongozo wa shughuli zote unazotakiwa kuzifanya katika kilimo tangu kuandaa shamba mpaka kuvuna.
Hatua hii ijumuishe shughuli kama kupanda, kudhibiti magugu, uwekaji wa mbolea na kudhibiti wadudu na magonjwa.
Kwa mfano uwekaji wa mbolea: wakati gani uweke? kiasi gani? uwekeje? Unatakiwa ufahamu haya yote kabla hujaanza mradi wa kilimo ili usipate usumbufu wakati wa utekelezaji.
- Makadirio ya gharama za uzalishaji na faida
Hili ni jambo muhimu sana. Unapofanya kilimo biashara hujaamua kulima ili ujifurahishe tu, unalima ili upate faida. Kwa mantiki hiyo unatakiwa ujue mradi wako utakugharimu kiasi gani katika utekelezaji wake na mwisho wa siku utakulipa kiasi gani?
Kwanini ni muhimu kufahamu mambo haya?
- Kufahamu mahitaji muhimu unayotakiwa kuwa nayo kabla hujaanza mradi wa kilimo
- Kupata fursa ya kufuatilia mradi wako katika hatua mbalimbali hata kabla hujauanzisha
- Utaweza kujua makadirio ya gharama za uzalishaji na faida tarajiwa
Mambo ya ziada yanayoweza kusaidia kukuza kilimo biashara
Tunza kumbukumbu:“Mali bila daftari hupotea bila habari”. Mkulima unatakiwa uwe na daftari la kutunzia kumbukumbu za shughuli zote za shamba. Tunza kumbukumbu za gharama zote ulizozitumia katika kilimo chako.
Mfano; Kama ulikodi shamba au ulinunua, ulilima kwa trekta, ukaajiri watu wa kupanda, ukanunua pembejeo na kama uliajiri watu katika hatua tofauti za kilimo n.k gharama zote ulizotumia katika shughuli hizi zihifadhiwe kwani hii ndio dira yako.
Pima mavuno: Kiasi cha mavuno unaweza kukipima kwa idadi ya magunia au matunda, kwa uzito (Kg) au ujazo (lita au debe). Inapendekezwa kupima kwa gunia, au kilo au/na idadi ya matunda kwa sababu ndio vipimo vinavyotumika kuuza bidhaa sokoni.
Tambua thamani ya mazao: Katika hatua hii gawanya jumla ya gharama za uzalishaji kwa kiasi cha mavuno. Lengo ni kujua umegharamia pesa kiasi gani kwa gunia moja au kilo moja au kwa tunda moja ulilovuna. Hii ndiyo thamani ya mazao yako.
Ikiwa gharama za uzalishaji ni kubwa basi mazao yako yanathamani kubwa na hivyo basi ili upate faida ni lazima uuze kwa bei kubwa kuliko thamani yake.
Panga bei ya mazao yenye faida
Baada ya kujua thamani ya gunia moja au kilo moja au tunda moja, hatua nyingine ambayo ndio muhimu zaidi ni kupanga bei sahihi yenye faida utakayouzia mazao yako. Hapa tunahitaji kupanga bei ya mazao kwa kipimo husika yaani bei ya gunia moja au kilo moja au tunda moja. Bei yenye faida kwako ni ile itakayorudisha gharama zote ulizotumia katika uzalishaji wako.
Ikiwa bei uliyopanga kuuza mazao yako ni ndogo kuliko inayotembea sokoni kwa wakati huo unaweza kuuza au kuangalia namna nyingine ya kuongeza faida zaidi. Ukiona bei ya sokoni ni ndogo kuliko ile uliyopanga kuuzia mazao yako, fanya moja kati ya yafuatayo:
- Kwa mazao yanayohifadhika basi yahifadhi kwa muda ili kupisha hali mbaya ya soko. Hakikisha kuwa mazao yako yanahifadhika na una miundombinu ya kuhifadhia kwa angalau miezi mitatu hadi sita.
- Kumbuka kuwa unapoamua kuhifadhi unaongeza gharama za ulinzi na za kuhifadhi hivyo utakapotaka kuuza itabidi uzitilie maanani gharama hizi. Kwa maana nyingine ni kwamba unaongeza gharama za uzalishaji kwa hiyo utatakiwa kuongeza ile bei ya kuuzia.
- Na kwa mazao yasiyohifadhika kama mboga mboga na matunda, epuka hasara na uuze kurudisha gharama. Hii inamaanisha uza mapema kadri uwezavyo, kwani kuchelewesha kuna hasara Zaidi,
ANGALIZO: Katika mradi wowote wa kilimo biashara utakao ufanya jitahidi kupunguza gharama za uzalishaji ili ujiongezee nafasi ya kupata faida kubwa zaidi. Punguza gharama zote zisizo za lazima, lakini usijisahau kiasi cha kuathiri ubora na wingi wa mavuno.
Hili chapisho limenifundisha mm kama mkulima mdogo, asanteh mungu awabaliki sana. Na mtoe chapisho nyingi zaidi.
Asante sana kwa mrejesho wako, tunashukuru pia kwa pongezi. Karibu na tunaendelea kuchapisha machapisho mengine ya jarida letu