Maparachichi ni moja ya zao la matunda ambalo hulimwa kwa wingi katika mikoa ya Mbeya, Kilimanjaro, Morogoro, Kigoma, Kagera, Arusha na Tanga. Zao hili ni muhimu sana katika lishe kwani lina mafuta na protini kwa wingi kuliko matunda yote yanayolimwa nchini.

Kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji kila wakati, ambapo mara nyingine husababisha kushuka kwa bei ya matunda haya sokoni, ni vyema wakulima wakajifunza kusindika maparachichi kupata saladi (guacamole) na kupunguza hasara ambazo husababishwa na kushuka kwa bei sokoni.
Vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya kusindika maparachichi kupata (guacamole) saladi.
Mashine ya kusaga rojo, bakuli la kuoshea maparachichi, kisu kikali kisichoshika kutu, chupa za kufungashia zenye mifuniko imara na lebo.
Malighafi
Maparachichi mawili, kitunguu maji kimoja, pilipili kali moja, juisi ya limao kidogo, giligilani ya majani 25, chumvi na pilipili manga kidogo, maji safi na salama pamoja na nyanya moja kubwa.
Jinsi ya kutengeneza
- Menya kitunguu kisha katakata pamoja na pilipili kali.
- Osha maparachichi na giligilani.
- Saga giligilani kwenye mashine ya kusaga.
- Ongeza maparachichi, juisi ya limao, nyanya, pilipili, kitunguu maji, chumvi na pilipili manga.
- Saga hadi mchanganyiko uwiane sawa kisha fungasha kwenye chupa za kioo.
- Weka lebo na hifadhi mahali penye baridi.
Matumizi Guakamole hutumika kama sosi baridi pamoja na vitafunwa kama mkate au pamoja na mboga za majani. Hutumika pia kama mchanganyiko wa matunda.
Hutumika katika hali ya kusindikwa. Bidhaa inayotokana na parachichi ni saladi ambayo hutumika pamoja na chipsi au chakula chochote kilichotengenezwa kutokana na nafaka.
Viamabaupishi vinavyopatikana kwenye gramu 100 za maparachichi.
Maji gramu 75, Mafuta gramu 21.8, Wanga gramu 6, Nguvu kilokari 875, Kalsiamu miligramu 10, Fosiforasi miligramu 34, Vitamini A I.U 800, Vitamini C miligramu 15




