Chakula na lishe ni muhimu kwa afya ya binadamu, hasa wakulima wanaotumia nguvu kazi nyingi shambani. Wakati mwingi wakulima wanazalisha na kuuza, wanasahau kwamba pia wao wanahitaji lishe bora ili kuwa na nguvu ya kuendelea kufanya kazi na kuhakikisha usalama wa chakula.
Ili kuwa na lishe bora tunapaswa kula mlo kamili na wa kutosha. Unapotafuta na kutayarisha chakula, zingatia makundi sita ya chakula ikiambatana na mazoezi ya mwili ambayo ni msingi wa afya njema. Makundi haya ni; nafaka na mizizi yenye wanga, vyakula jamii ya mikunde, vyakula asili nyama, mbogamboga, matunda na mafuta.
Chakula cha nafaka ni chanzo cha wanga na nguvu mwilini. Vyakula asili ya nyama husaidia kujenga mwili kwa uwepo wa protini. Hii ni pamoja na vyakula jamii ya mikunde ambayo huwa ni chanzo cha protini ambayo hujenga mwili. Mbogamboga na matunda huwa na vitamin na madini ambayo hujenga kinga ya mwili dhidi ya magonjwa. Nayo mafuta huipa mwili joto.
Zingatia haya
Punguza kiasi ya mafuta kwenye chakula. Ingawa mafuta muhimu mwilini, yana yanahitajika kwa kiasi kidogo tu. Zaidi, tumia mafuta yatokanayo na mimea ikilinganishwa na mafuta inayotokana na mifugo.
Ongeza matunda na mbogamboga kwa wingi. Hivi ni vyakula vyenye nyuzinyuzi ambayo husaidia katika usagaji wa chakula tumboni.
Tumia chumvi iliyoongezwa madini joto (iodine), na utumie kwenye kupika vyakula kwa kiasi kidogo. Epuka kutoongeza chumvi ya ziada mezani wakati wa kula, ingawa inaongeza ladha kwa chakula, ukifanya hivi, utakula chumvi nyingi kupita kiasi.
Sawa na chumvi, matumizi ya sukari yawe kwa kiasi kidogo. Punguza kula bidhaa zinazowekwa sukari, kwa mfano, biskuti, visheti, kashata, keki, pipi, chokoleti, jamu, na kadhalika. Vyakula aina tofauti huwa na sukari. Hivyo, tumia sukari ya dukani kwa kiasi kidogo. Unaweza kutumia asali kama mbdala ya sukari, pia, kwa kiasi kidogo.
Hata hivyo, uaji bora unatakiwa kuzingatia mahitaji ya mwili kulingana na umri, kazi ama shughuli anazofanya mtu, na pia hali ya afya ya mtu.
Watoto
Watoto chini ya miezi sita wapewe maziwa ya mama pekee, pasipo kutumia chakula kingine.
Watoto wenye umwri wa miezi sita hadi miaka miwili wapewe maziwa ya mama na chakula mchanganyiko cha nyongeza. Chakula hiki kitengenezwe kwa kutumia vyakula asili. Iwapo mtoto hanyonyi maziwa ya mama, anahitaji kupewa maziwa (baada ya mwaka mmoja) mengine (kama ya ng’ombe) angalau nusu lita kwa siku na chakula mchanganyiko.
Watoto wenye miaka miwili mpaka mitano wale angalau milo mitano kwa siku (kwa viwango vidogo-vidogo) na maziwa yaendelee kuwa sehemu ya mlo wa mtoto.
Watoto wa miaka sita hadi tisa wapewe milo kamili mitatu na vitafunwa mara mbili au tatu kwa siku. Vitafunwa hivi visiwe na sukari au mafuta mengi.
Vijana
Vijana (wavulana na wasichana) wanahitaji virutubishi kwa wingi zaidi kwani wanakua haraka, hivyo ni muhimu kuongeza kiasi cha chakula. Wasichana wanahitaji madini chuma kwa wingi kwa sababu hupoteza damu wakati wa hedhi, hivyo wale vyakula vyenye madini chuma (iron), asidi ya foliki na vitamini C kwa wingi ili kutengeneza chembe chembe za damu kwa wingi Inashauriwa pia watumie chumvi yenye madini joto (iodine).
Wazee
Wanahitaji mlo kamili midogo-midogo mara nyingi kwa siku. Wale vyakula laini vyenye virutubishi kwa wingina vyakula vyenye madini ya chokaa (Calcium) kwa wingi kama maziwa na dagaa. Waongeze ulaji wa vyakula vyenye nyuzi-nyuzi ili kusaidia mfumo wa usagaji wa chakula.
Mwanamke mjamzito
Mwanamke mjamzito anahitaji kuongeza chakula kukidhi mahitaji yake binafsi na ya mtoto aliye tumboni. Vinginevyo anaweza kupatwa na matatizo ya kiafya. Anapaswa kutumia vidonge vya madini chuma (iron), vidonge vya asidi ya foliki, vidonge vya kutibu minyoo, dawa za kuzuia malaria na alale ndani ya vyandarua vilivyowekwa viuatilifu ili kijikinga dhidi ya mbu na malaria. Vyote hivyo ili kuzuia upungufu wa damu. Pia, atumie chumvi yenye madini joto (iodine).
Mbinu asili
Wakati chakula kiko shambani ni muhimu sana kwa mkulima kutumia mbinu sahihi za kiasili ili kulinda afya ya kilichozalishwa na kutunza rutuba ya udongo. Hii ni pamoja na matumizi sahihi ya mbolea asili, madawa ya wadudu na dawa ya kukuzia (booster). Kumbuka kuwa bidhaa inayotoka shambani ikiwa na vimelea vya sumu vitaadhiri usalama wa mtumiaji na kupunguza ubora wa chakula.
Wakati wa kuanda vyakula inabidi tuwe na umaakini ili tulinde ubora wa chakula husika. Hakikisha unaosha mboga za majani na kuacha zitoke maji kabla ya kukata. Pika mboga za majani kwa muda mfupi, na endapo utahitaji kuchemsha mboga,