Kilimo cha kiikolojia cha wakulima wadogo ni aina ya maisha yanayoichukulia dunia kwa heshima na kuithamini, na siyo kama kitu cha kunyonywa. Ni mfumo wa maisha unaonyesha kuwa upo uhusiano wa karibu kati ya binadamu na mazingira yanayowazunguka na hivyo mazingira hayo yasithaminishwe kwa pesa.
Mfumo huu unaoelewa kuwa matumizi mabaya ya mazingira na kuyafanya chanzo cha pesa kutaangamiza watu na dunia nzima.
Utamaduni wa kilimo hiki umejengwa katika msingi wa kubadilishana mbegu, kupeana maarifa, kupanda aina tofauti za mazao na kuweka mzunguko mzuri wa virutubisho kwa ajili ya kulinda rutuba na uhai wa ardhi ya kilimo.
Ni mfumo wa wakulima wadogo na hauwezi kuthaminishwa kwa pesa. Ni kwa njia hii ujuzi mpya wa kuzalisha mazao kwa namna inayoendana na tabianchi umebuniwa, na Kilimo cha Kiikolojia kimejengwa katika msingi huo.
Chakula lazima kilimwe kwa ajili ya binadamu, siyo kwa ajili ya faida. Wakulima wadogo wanaozingatia kilimo cha ekolojia huhimili na kupata nafuu haraka inapotokea kuna matatizo makubwa ya hali ya hewa kama vile ukame na mafuriko.
Kwa kutumia ujuzi asilia, mbegu za kienyeji, na kupanda aina tofauti za mazao, wakulima wanakuwa na uhakika wa kupata chakula bora kwa ajili yao na familia zao. Kwa kupata nafaka zinazoweza kuhifadhiwa kwa miaka mingi kama vile mtama, ulezi, uwele, inakuwa rahisi kwa mazao hayo kuhimili ukame. Kwa kuzingatia bayoanuwai, wakulima wanalinda udongo, wanatunza nyasi na miti inayotunza maji. Kwa kutumia mbolea inayotengenezwa shambani, wakulima wadogo hutunza virutubisho na kuendeleza uhifadhi wa rutuba.
Si hayo tu, bali pia kitendo cha kuzalisha kwa njia ya kienyeji badala ya kuzalisha kwa lengo la masoko ya kimataifa, wanatumia nishati kidogo na hivyo kuwa na kutoa hewa kidogo ya ukaa (kwa njia ya usafirishaji na ufungashaji wa mazao kwa ajili ya kupelekwa sokoni), na hivyo kufanikiwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Uzalishaji wa chakula kwa ajili ya kuuza nje huondoa rutuba ya ardhi kwa njia ya matumizi ya mbolea za kiwandani na viuatilifu ambavyo huharibu udongo na kuwafanya wakulima wawe watumwa wa kununua pembejeo hizo kutoka kwa makampuni makubwa ya pembejeo za kilimo.
Ni kwa njia hii, makampuni makubwa ya kilimo, yakiwa sehemu ya mfumo mzima wa chakula wa dunia nzima, husababisha mahitaji ya pembejeo zao, na kuwafanya wakulima wadogo waendelee kuingia gharama za kilimo. Lakini wakulima wadogo lazima walime kwa ajili ya kupata vyakula vyenye lishe bora na siyo kutengeneza mzunguko wa utegemezi.
Kilimo cha Kiikolojia cha wakulima wadogo hakipingani na teknolojia mpya. Kwa kweli, mkabala wa kilimo cha kiikolojia kinajikita katika sayansi, na kinatoa jukwaa mahususi kwa ajili ya maendeleo na kuhusisha teknolojia zenye tija. Lakini kilimo hiki kinapingana na teknolojia zinazotumika na mashirika shawishi kwa ajili ya kujimilikisha njia za uzalishaji wa chakula, ambazo zinakiuka uhuru na haki za wazalishaji na walaji, kwa maslahi binafsi.
Endapo teknolojia hizi zitachangia katika kutetea uhuru wa wakulima wadogo na uzalishaji wao, maeneo yao, utamaduni wao, na maisha yao, na kama inapigania haki za mazingira, na hivyo itaweza kuboresha maisha ya mkulima mdogo.
Kilimo cha kiekolojia cha wakulima wadogo, na misingi ya ujuzi wa kilimo hicho, ni mfumo unaonyesha kuwa upo uhusiano wa karibu na jamii na muunganiko wa kina na ardhi na ekolojia ya maeneo husika. Kilimo hiki kimeanza kutoa matokeo mazuri katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Hata hivyo, mafanikio yanakwamishwa na mfumo uliopo unaosisitiza mahitaji ya kupata faida inayotokana na kilimo cha mazao ya chakula.