Mara nyingi wakulima wa mbogamboga na matunda wanapata hasara kutokana
na ukosefu wa soko la uhakika. Wakulima wengi wamezoea kuuza mbogamboga na matunda yakiwa ghafi kutoka shambani. Hii ni changamoto wakati mavuno ni mengi na wanunuzi ni wachache. Ili kuepuka hali hii, uhifadhi wa mbogamboga na matunda ni ya manufaa hasa wakati uhitaji ni mkubwa na pia kudumisha lishe bora.
Wakati wa masika, hupatikana aina mbalimbali za mbogamboga ya majani kama vile sukuma wiki, mchicha, managu, kunde, spinach na mengine mashambani na pia sokoni. Matunda ya msimu yanafurika soko na hupatikana kwa wingi mashambani. Mbogamboga na matunda ni vyanzo vya virutubisho muhimu kwa ukuaji wa vikundi mbalimbali vya binadamu. Virutubisho hivi husaidia kujenga na kudumisha kinga ya mwili na kupigana na magonjwa mbalimbali.
Mazao ya mbogamboga na matunda upoteza ubora wake mara tu baada ya kuvunwa, na uanza kunyauka na mengine kuoza baada ya muda mfupi. Hii ni kutokana na uwepo wa vimelea na bakteria zinazosababisha kuoza. Vimelea hivi hupatikana kwa maji chafu, miko michafu, vifaa vichafu vinavyotumika, matunda yaliyoiva zaidi na yaliyoharibika, mavuno kuwekwa katika maeneo yenye kiyesi cha wanyama, kuingiliwa na wadudu na hata panya. Hivyo, usafi ni muhimu sana wakati mkulima anafanya shughuli ya uvunaji.
Hata hivyo, mkulima lazima kuwa makini ni wakati gani anavuna mazao yake kwani mambo ya kimazingira huchangia pakubwa kwa uharibifu wa mazao. Haya ni pamoja na joto, unyevu na miale ya jua. Kuhifadhi mbogamboga na matunda katika eneo baridi inayaruhusu kuwa katika hali nzuri kwa muda mrefu.
Kukausha mboga na matunda inapunguza uzito na ukubwa wake, hivyo kurahisisha usafirishaji na uhifadhi, na kuepusha uharibifu na upotevu. Unapoweza kusafirisha bidhaa mingi kwa wakati mmoja, unapunguza gharama na kuongeza faida baada ya mauzo. Kukausha na kuhifadhi mbogamboga na matunda ina faida kubwa kibiashara kwani ni cha kipato kwani bidhaa huwa kidogo sokoni na uhitaji ni mkubwa. Zaidi, uhifadhi huu inatoa lishe bora kwa familia wakati wote wa mwaka hata wakati ambapo mazao hayo hayapo shambani.
Mbinu za uhifadhi
Kuna njia mbalimbali za kutayarisha mbogamboga na matunda kwa ajili ya uhifadhi na pia ikiwa ni njia ya kuongeza dhamani yake kwa soko au mauzo ya aina yoyote. Njia rahisi ya kuhifadhi na inayoweza kutumika na mkulima bila gharama kubwa ni kukausha. Mboga inapokaushwa, inapunguza kiasi ya maji na kuwezesha mboga kuwa bora kwa matumizi kwa muda mrefu. Ili kuhakikisha ubora wa bidhaa; zingatia usafi muda wote kwa kutumia maji safi, usafi wa watu wanaofanya shughuli hii, usafi ya maeneo na vyombo kama vile kikaushio. Unaweza kuosha vyombo na kikaushio kwa kutumia maji safi yenye chumvi ili kuua bakteria.
Kukausha mbogamboga ya majani
Mbogamboga jamii ya majani ni kama vile spinach, majani ya malenge, kunde, mboga za kienyeji na kadhalika.
- Chagua majani mabichi, laini na yenye rangi nzuri ya kijani kibichi. Hakikisha unatoa majani yaliyonyauka, kukwaruzika au yaliyokauka.
- Tayarisha mboga ya kutosha kwa uhifadhi kwa wakati mmoja. Usivune mboga kisha uyaache hadi siku inayofuata, ubora wake utapungua na kupoteza virutubisho.
- Osha majani kwa maji safi kisha ondoa sehemu ngumu kwenye majani na kuchambua ili kuondoa nyuzinyuzi.
- Unaweza kukatakata mboga vipande vidogo-vidogo, ila hakikisha kuwa unaosha mboga kabla ya kuchambua au kukata ili kuepuka kupoteza vitamin muhimu.
- Tumbukiza mboga kwenye maji ya yaliyochemka na yaliyotiliwa chumvi. Yaache kwenye maji kwa dakika 1 hadi 1½ na uhakikishe majani yote yamefunikwa na maji. Unaweza pia kutumia maji vuguvugu kwa dakiki 3-5. Ondoa mboga na kuweka kwenye maji ya baridi kwa dakika 1 ili kuzia kuendele kuiva
- Chuja maji kwenye mboga na kuweka katika trei au gunia safi ili kuepuka kuingiliwa na uchafu.
- Kausha mboga ikauke vizuri, ila yasipigwe moja kwa moja na miale ya jua. Geuza mboga kila baada ya masaa matatu ili majani yote yakauke vizuri.
- Hifadhi mboga yako kwenye mifuko safi yasioweza kuingiza hewa.
Unapotayarisha mbogamboga yaliyokaushwa kwa ulaji, yaloweshe kwenye maji kwa saa 1 hadi 2 ili kurudisha unyevu. Usimwage maji unayotumia kulowesha mboga, ila weka kando na kutumia kupika mboga hayo ili kuepuka kupoteza virutubisho.
Kukausha matunda
Matunda yanayofaa kwa uhifadhi huu ni kama maembe. Andaa kiasi cha matunda unachohitaji na matunda hayo yawe yameiva vizuri na yasiwe yameoza.
- Osha matunda vizuri kwenye maji safi ukitumia sabuni au maji yenye limau.
- Menya na kukatakata vipande yenye upana wa milimita 6 hadi 8.
- Loweka kwenye maji, limau na sukari kwa dakika 15-20. Tumia mililita 50 ya jisi ya limau kwa gramu 60 ya sukari kwenye lita 1 ya maji (50mls: 60g: 1ltrs).
- Ondoa matunda kisha uyaweke kwenye trei au chombo cha chuma kisichoshika kutu. Unaweza kupaka trei mafuta kidogo. Funika ukitumia neti na uyaweke nje ili yakauke, ila yasipigwe moja kwa moja na miale ya jua. Yakaushe kwenye kivuli au chombo cha kukaushia.
- Gueza baada kila baada ya masaa 3. Matunda yako yatakuwa yamekauka vizuri baada ya siku 2-5 kulingana na hali ya hewa.
- Kausha vipande vya matunda hadi yanaweza kuvunjika kwa urahisi, kisha hifadhi kwenye mifuko na kwenye eneo baridi.
- Bidhaa hii itakuwa na ubora mzuri na kutumika hadi miezi 12.
Kukausha ndizi iliyoiva
Ukaushaji wa ndizi husaidia kuongeza ubora, thamani, matumizi ya baadaye kama chakula, pamoja na kusubiri soko yenye bei ya juu.
- Hakikisha unatumia ndizi iliyokomaa na kuiva vizuri. Osha kwa kutumia maji safi ili kuondoa uchafu.
- Menya ndizi kwa uangalifu na kuondoa nyuzi na sehemu zilizopondeka, kisha kata vipande kiasi cha sentimita 0.5 hadi 1 kila kipande ili kurahisisha ukaukaji na kuwa na umbo nzuri baada ya kukauka.
- Unaweza kulowesha ndizi kwenye maji ya limau (kipimo mililita 100 juisi ya limau, gramu 60 ya sukari na lita 1 ya maji) kwa dakika 10-15.
- Weka kwenye chombo chenye maji safi, ili kuzuia kiasi ya sukari kwenye ndizi kupanda na kusababisha ndizi kupoteza rangi yake ya asili.
- Baada ya kukata kiasi cha ndizi unachotaka kuhifadhi, panga vizuri kwenye kikaushio cha jua (solar drier). Gueza baada kila baada ya masaa 3 kulingana na kiasi ya joto.
- Ndizi huchukua muda wa siku 5 kukauka vizuri wakati wa msimu wa jua na siku zaidi wakati wa mvua na mawingu mengi.
- Bidhaa hii itakuwa na ubora mzuri na kutumika hadi miezi 6.
Ndizi iliyohifadhiwa kwa njia hii huweza kutumiwa kama kitafunio pamoja na vinywaji vya aina mbalimbali kama vile kahawa, juisi au chai. Kwa kawaida, mbogamboga na matunda yaliokaushwa huweza kuuzwa rejareja (kwa majirani na soko la karibu) au kwenye maduka makubwa ya vyakula.