Maharagwe hushambuliwa na magonjwa kadhaa shambani, na pia huweza kuharibiwa na wadudu shambani ama wakati wa kuhifadhiwa.
Kutu ya Maharagwe
Ni ugonjwa unaosababishwa na ukungu na kwa kawaida hushambulia majani, shina na mifuko ya maharagwe. Dalili kuu za ugonjwa huu ni madoa yenye rangi ya kutu yenye unga ambao unaweza kuonekana kwenye majani, shina au vifuko vya mmea. Madoa yanaanza yakiwa madogo na hutoa unga ya rangi ya kahawia na kuongezeka kwa wingi na ukubwa na kuwa na unga nyeusi. Pia, madoa yanaweza kusababisha mashimo nyeusi kwenye mifuko ya maharagwe. Ugonjwa huu hudunisha mavuno ambayo mkulima atapata kwa hadi asilimia 30.
Kuthibiti
- Mkulima achague na kupanda mbegu safi ili kuzuia ukungu kuenea kutoka mmea mmoja hadi mwingine hasa wakati wa unyevu unyevu.
- Tumia mbegu inayostahimili ugonjwa huu kama vile Kabanima, Uyole 98, Ilomba, Lyamungu 90 au Selian 97.
- Panda maharagwe mwisho mwa msimu wa mvua kubwa ili kuepukana na unyevu mwingi unaoweza kusababisha ugonjwa kutokea au kusambaa kwa haraka.
- Unyevunyevu huweza kusambaza ukungu. Hivyo, mkulima anashauri kuwa makini shambani, hasa wakati wa palizi.
- Lima kwa kina cha sentimita 45 ili kuwezesha mabaki kuoza na kuzuia kuenea kwa ugonjwa toka msimu mmoja hadi mwingine.
- Ondoa shambani au zika ardhini mabaki ya mimea iliyoathirika.
- Funika mabaki ya mimea ardhini ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa
Virusi vya batobato la Maharagwe
Ili kudhibiti batobato;
Hakikisha mimea yako ni yenye nguvu na afya. Tumia mbinu hai za kuurutubisha udongo.
- Kama ugonjwa umezuka, safisha zana za shambani kama jembe baada ya matumizi
- Epuka kutembea ndani ya shamba / kugusa mimea iliyoambukizwa kisha kwenda kwenye mimea ambayo bado kuambukizwa.
- Dhibiti vidukari ndani ya shamba na mashamba mengine yanayozunguka hapo. Dhibiti vidukari kwa kutumia maji ya sabuni juu ya mimea na chini ya majani. Changanya gramu 8 za sabuni na lita 10 za maji na unyunyize kwenye mimea.
- Tembelea shamba lako mara kwa mara ili kujua kama kuna mashambulizi.
- Hakikisha shamba lako halina vidukari kwa sababu wanachangia kueneza ugonjwa huu.
- Ngoa na kuchoma au kuzika mimea yaliyoambukizwa.
Kuthibiti Halo blight
Mmea huwa na madoa madogo yaliyolowa maji (yanafanana na tundu za sindano) katika upande wa chini wa majani ambayo baadaye hugeuka rangi ya kahawia nyekundu na kukauka baada ya siku chache. Mara nyingi, t ishu zinazozunguka ile sehemu ya doa iliyokauka baadaye huwa rangi ya kijani cha ndimu na kufanya halo. Vitumba huwa na madoa ya mafuta-mafuta yaliyolowa maji, ambayo hutofautiana kwa ukubwa na yanaweza kufanya kingo za kahawia jinsi yanavyoendelea kukomaa. Hakuna mzunguko wa rangi ya kijani cha ndimu kwenye vidonda vilivyo katika vitumba, lakini nta nyeupe ya bakteria huonekana katikati mwa madoa wakati wa unyevu. Kwenye mashina ya maharagwe madoa ya kawaida ya mafutamafuta inaonekana, huku mbegu zinaoza au kuonekana zilizosinyaa na kuharibika rangi.
Njia za kudhibiti halo blight ni pamoja na;
- Panda mbegu safi.
- Ondoa mimea yaliyomea kwa kujitolea na mabaki ya mimea ili kupunguza vyanzo awali vya ugonjwa.
- Usiingie katika shamba wakati mimea ina unyevu ili usieneze ugonjwa.
- Safisha na uondoe bakteria kwenye vifaa ambavyo vimetumika katika shamba lililoambukizwa kabla kuenda kwenye mashamba ambayo hayana magonjwa.
- Fanya mzunguko wa mazao na nafaka kwa miaka 3 au zaidi.
Bakteria blight
Husababishwa na bakteria, na huwa na madoa juu ya majani, mashina na mifuko ya mbegu. Mbegu huambukizwa ndani na nje. Ugonjwa hupatikana kwa mbegu zilizoambukizwa, na huenea sana wakati kuna unyevu, hasa mvua nyingi, kupitia wadudu na hata upepo.
Ili kudhibiti ugonjwa huu;
- Hakikisha unatumia mbegu safi na zisizokuwa na ugonjwa.
- Fanya kilimo cha mzunguko, ukibadilisha maharagwe na mahindi au mazao mengine ya msimu.
- Usiingie au kufanya kazi shambani wakati kuna unyevu nyingi.
- Dumisha usafi shambani kwa kuondoa mabaki ya mimea na kufanya palizi wakati unaofaa.
Wadudu wanaoshambulia maharagwe
- Vidukari. Vidukari au wadudu mafuta ni wadudu wadogo, weusi hujitokeza wakati wowote katika hatua za ukuaji wa maharagwe. Hukaa chini ya majani na kubangua majani. Mara nyingi vidukari hujitokeza wakati wa kiangazi, hivyo mimea huonekana kama yamenyauka.
Ili kudhibiti vidukari;
- Tembelea shamba lako mara kwa mara, kisha uangalie chini ya majani ya mimea ili kuona kama kuna mashambulizi.
- Unaweza kunyunyiza sabuni ambayo hutoa koti la juu linalolinda ngozi ya vidukari. Tumia kiwango cha lita 20 ya maji kwa sabuni ya kipande ya urefu wa inchi moja/ nusu kidole au vijiko vya chai 10-15 vya sabuni ya maji).
- Nyunyiza mapema asubuhi au jioni ili dawa isikauke haraka. Kunyunyiza wakati wa baridi pia huzuia jua kuchoma majani.
Inzi weupe. Inzi weupe ufyonza maji kwenye majani ya mimea na hutoa mayai mengi ya rangi ya kahawia nyeupe. Wale ambao wamekomaa hukaa upande wa chini wa majani machanga. Wingu la wadudu hawa weupe zaidi ya 3-5 hutua tena mara tu baada ya mmea kutikiswa. Unaweza pia kuangalia rangi ya manjano kwenye majani ya mmea yaliyo chini ili kujua kama kuna mashambulizi.
Ili kudhibiti inzi weupe;
- Panda wakati wa mvua au muda mfupi baada ya mvua.
- Weka shamba safi bila ya kwekwe kwa kuwa zinaweza kuwa makazi mbadala ya inzi weupe.
- Panda mimea inayofukuza wadudu kama giligilani na marigold kuzunguka shamba.
- Hifadhi maadui wa asili, kwa mfano, nyigu vimelea kwa kuepuka kunyunyiza dawa wakati wa maua.
- Anza hatua za kudhibiti mara tu wadudu wanapoonekana kwenye mazao.
- Weka mitego ya njano yenye gundi ili kunasa inzi weupe waliokomaa. Kwa kawaida, mitego 4 kwa mita 300 mraba iwekwe sentimita 50 juu ya ardhi.
- Unaweza kutumia pilipili kuwafukuza na kuua inzi weupe. Changanya pilipili 30 zilizokatwakatwa kwenye lita 1 ya maji moto. Ziloweke kwa siku 1 kisha uzipunguze ukali kwa kuongeza lita 10 za maji. Nyunyiza kwenye mimea ukilenga upande wa chini wa majani.
Fukusi wa Maharagwe
Fukusi hushambulia Maharagwe yaliyovunwa na kuhifadhiwa. Hata hivyo, wanaweza kushambulia maharagwe yakiwa shambani. Wanapatikana ndani ya maharagwe na husababisha matundu kwenye mbegu. Mdudu huyu ni rangi ya nyekundu yenye kahawia. Mabuu hutoboa na kuingia ndani ya mbegu na kuanza uharibifu.
Ili kudhibiti fukusi;
- Tumia mbegu safi na ambazo hazijatobolewa.
- Panda maharagwe kwa mseto na mahindi ili kupunguza uzito wa mashambulizi.
- Vuna maharagwe mara tu yanapokomaa ili kupunguza hatari ya maambukizi makali.
- Kausha maharagwe iwe na unyevu wa asilimia 12 au chini zaidi kabla ya kuhifadhi.
- Dumisha usafi wa hali ya juu kwenye ghala au eneo la kuhifadhi.
- Hifadhi maharagwe kwenye chombo kisichoingiza hewa, kama vile mifuko ya plastiki au, mapipa.
- Unaweza pia kuchanganya maharagwe na mafuta ya mboga, unga wa mwarobaini au jivu kabla ya kuhifadhi. Hii itawazuia wadudu hawa kuzaliana.