Uzalishaji wa mboga mara nyingi unahusisha matumizi ya viuatilifu vyenye kemikali. Baadhi ya wakulima hawawezi kumudu gharama kubwa za viuatilifu hivi, ambavyo visipotumika vizuri huweza kuleta madhara, kama kuharibu mazingira, mimea na kuathiri watumiaji wa mboga.
Njia asilia za kudhibiti visumbufu hutumia dawa zinazotokana na mimea ambayo hupatikana katika maeneo ya wakulima. Matumizi ya dawa hizi ni njia mojawapo ya kuepuka dawa za viwandani
ambazo huathiri udongo, mazingira na afya za watu na wanyama.
Madawa haya yasipotengenezwa vizuri na kutumiwa ipasavyo yanaweza yasifanye kazi ipasavyo na hivyo kuwa vigumu kuwashawishi wakulima kuzitumia.
Inashauriwa kutumia dawa hizi kama kinga kabla mashambulizi hayajashamiri kwani zinafanya kazi taratibu, hivyo ni vizuri kuzitumia kama kinga kuliko tiba.