- Kilimo

Benki za mbegu za asili zinazosimamiwa na jamii

Sambaza chapisho hili

Sekta ya kilimo nchini inachangia takribani asilimia 26 ya pato la taifa na kuajiri asilimia 75 ya idadi ya watu huku ikisaidia kuongeza mapato na kuboresha maisha.

Katika kuhakikisha wakulima wanaweza kuongeza uzalishaji mbegu na mavuno mengi, serikali kupitia waziri wa kilimo, Hussein Bashe wakati akiwasilisha bajeti ya wizara mwaka 2022- 2023 bungeni alisema, mikakati yao ni kuwa na benki ya mbegu ambayo itaweza kuchangia ongezeko la mbegu nchini.

Benki za mbegu za jamii ni nini

Benki za mbegu za jamii ni taasisi zisizo rasmi, zinazoongozwa na kusimamiwa na wakulima au serikali za mitaa, ambazo kazi za msingi ni kuhifadhi mbegu kwa ajili ya matumizi ya ndani.

Kwa sasa hapa nchini mwamko wa wanajamii kuanzisha na kusimamia benki za mbegu ni mdogo japo benki hizo zilikuwa zinapatikana katika maeneo machache ya Dodoma na Mbeya.

Benki hizo zilikuwa zikijulikana kwa majina kama, benki za jeni za jamii, nyumba za mbegu za wakulima, vibanda vya mbegu, vikundi vya kutunza mbegu, ushirika au mtandao wa kutunza mbegu, hifadhi ya mbegu za jamii, maktaba ya mbegu na benki ya mbegu za jamii.

Kuna umuhimu gani wa benki za mbegu zinazosimiwa na wakulima

  • Zina mbegu zinazovumilia na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
  • Zina mbegu ambazo huzalishwa kwa kuzingatia mbinu za ikolojia ya kilimo hai ambazo hutunza udongo na kuhifadhi mazingira na kujali afya ya mkulima na mlaji.
  • Hutunza aina mbalimbali za mbegu muhimu zilizopo na zinazoelekea kutoweka.
  • Husaidia kuwa na uhakika wa mbegu kwa jamii husika.
  • Kuna urahisi wa kubadilishana na kugawanya mbegu kwa wakulima.
  • Kuna urahisi wa kuongeza matumizi ya mbegu husika
  • Mbegu hizo zinaweza kuhifadhiwa kwa kiasi kidogo au kikubwa kulingana na hitaji na upatikanaji wake.

Hatua za kuanzisha na kusaidia benki za mbegu za jamii

  • Mchakato wa uchambuzi wa hali halisi ya mbegu

Hii hujumuisha mifumo ya mbegu, uchaguzi wa jamii na sehemu/eneo la kuanzishia benki ya mbegu.

  • Kuhamasisha na kuiandaa jamii

Wakulima wanaweza kuhamasishwa kushiriki katika shughuli za benki ya mbegu.

Pia vikundi vya wakulima vinaweza kuanzishwa na kuainisha mazao muhimu, na kukusanya mbegu kwa niaba ya jamii.

  • Hatua ya tatu ni kuchagua aina za mbegu

Aina hizi za mbegu ni kwa ajili ya kuhifadhi, ambapo kwa benki za mbegu za jamii huwa na lengo la kutunza mbegu za mazao muhimu. Ni muhimu wanajamii kutunza mbegu za mazao ya jadi yanayohusiana na utamaduni wa ndani na zenye uwezo wa kuhimili changamoto za magonjwa na mabadiliko ya tabianchi kama vile joto, ukame na mafuriko.

  • Kuchagua mbegu bora na safi

Kupata sampuli na kuchagua ambazo hazina magonjwa kwa kuchagua kutoka kwenye maeneo mbalimbali ya shamba, kwenye mimea na mashuke bora.

  • Kuweka miundombinu inayofaa ili kuweka mbegu katika hali ya usafi, afya na kuwa hai.

Miundombinu hiyo ni pamoja na rafu shelfu au makabati ya mbao na chuma, mzani wa kupimia mbegu, kaushio la jua, vifaa vya kuhifadhia mbegu vyenye ujazo tofauti, kifaa cha kupangia madaraja ya mbegu, nyaraka za kutunzia kumbukumbu, ubao wa matangazo na kipima joto na unyevu.

  • Kuingiza taarifa za mbegu kwenye daftari la kumbukumbu

Ni muhimu wakulima wakafundishwa kuweka taarifa za mbegu kwenye benki. Taarifa hizo ni pamoja na jina la mbegu la asili au la kisayansi, eneo au jamii ambayo mbegu imetoka au imekusanywa, na kiasi cha mbegu kilichokusanywa na jina la mkulima aliyetoa mbegu.

  • Uzalishaji endelevu wa mbegu

Katika hatua hii mbegu zinahuishwa kwa kuzipanda mara kwa mara. Benki za mbegu za jamii zinakuwa na kiasi kikubwa cha mbegu za asili, na pia zinahifadhi kiasi kidogo cha mbegu zilizoboreshwa. Uzalishaji wa huzingatia katika kuendleza mazao yasiyopewa kipaombele yenye afya, mazao yanayoelekea kupotea na mazao yenye uhitaji mkubwa kulingana na wanajamii.

Kwa maelezo zaidi wasiliana na Daud Ngosengwa Manongi mtalaamu wa Mbegu kutoka Mtandao wa Bayoanuai Tanzania (TABIO) 0769861063

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *