- Kilimo, Usindikaji

Usindikaji wa mafuta ya parachichi nyumbani

Sambaza chapisho hili

Unaweza kusindika na kukamua mafuta ya parachichi nyumbani

Parachichi ni moja ya zao la matunda ambalo liko katika kundi la mmea wenye ghala mbili, yaani tunda lake hulizunguka peke linalokuwa ndani. Kitalaamu parachichi huitwa Persea Americana na huweza kusindikwa na kupata mafuta.

Namna ya kusindika parachichi kupata mafuta

Kuna njia mbalimbali za kutengeneza mafuta kutokana na parachichi lakini mkulima anaweza kutumia njia rahisi ya kukausha parachichi kwenye oven na kisha kukamua kupata mafuta au kukausha parachichi kwenye mwanga na kisha kukamua kupata mafuta.

  1. Kusindika parachichi kwa kutumia oven kupata mafuta

Vifaa: Hii ni pamoja na oven, kisu kikali kisichoshika kutu, beseni, kitambaa cheupe cha pamba, bakuli, kijiko

Malighafi: Parachichi, maji

Namna ya kusindika

  • Chukua na chagua kiasi/idadi ya parachichi (yenye ubora na yaliyokomaa) unayotaka kusindika kupata mafuta kisha vundika mpaka yaive. Unaweza pia ukanunua parachichi yaliyoiva moja kwa moja sokoni.
  • Kama umevundika au kununua hakikisha yameiva vizuri tayari kwa ajili ya kukamua mafuta.
  • Chukua maji na weka kwenye beseni kwa ajili ya kusafisha parachichi.
  • Safisha parachichi vizuri kisha chukua kisu na kata kupata vipande viwili kisha toa kokwa.
  • Chukua kijiko, na na anza kutoa chakula kilicho ndani ya ganda la parachichi kwenye vipande ulivyokata na weka kwenye bakuli kubwa, pondaponda kupata rojo kisha weka kwenye sinia la oven.
  • Tandaza rojo lako kwenye sinia la oven kwa wembamba, inategemea na ukubwa wa sinia lako. (Unaweza kukausha mara nyingi kulingana na wingi wa parachichi ulizonazo).
  • Weka sinia kwenye oven na oka kwa muda wa dakika mpaka 15 kwa joto la sentigredi 100.
  • Toa rojo hilo na changanya vizuri hapohapo kwenye sinia kisha tandaza na rudishia tena kwenye oven.
  • Oka kwa muda wa dakika 10 kwa nyuzi joto 75 kisha epua na koroga tena.
  • Rudia mara 3 au nne mpaka pale utakapoona rojo limebadilika rangi na haishiki tena kwenye kijiko au sinia la oven, lakini pia umeanza kuona mafuta yanatoka.
  • Acha lipoe kisha chota kidogokidogo na weka kwenye kitambaa kisha anza kukamulia mafuta kwenye bakuli mpaka utakapoona mafuta hayatoki tena bali machicha tu yamebaki.
  • Tayari utapata mafuta safi na salama kwa matumizi mbalimbali.

  1. Kusindika parachichi kwa kutumia mwanga kupata mafuta

Usindikaji huu ni mrahisi sana na wenyewe utasindika parachichi kiasi unachotaka

Vifaa: Hii ni pamoja na kisu kali kisichoshika kutu, beseni, kitambaa cheupe, bakuli, kijiko

Malighafi: Parachichi, maji

Namna ya kusindika

  • Chukua na chagua kiasi/idadi ya parachichi (yenye ubora na yaliyokomaa) unayotaka kusindika kupata mafuta kisha vundika mpaka yaive. Unaweza pia ukanunua parachichi yaliyoiva tayari.
  • Kama umevundika, hakikisha yameiva vizuri tayari kwa ajili ya kukamua mafuta.
  • Chukua maji na weka kwenye beseni kwa ajili ya kusafishia parachichi.
  • Safisha parachichi vizuri kisha chukua kisu na kata kupata vipande viwili kisha toa kokwa.
  • Chukua kijiko, na na anza kutoa chakula kilicho ndani ya ganda la parachichi kwenye vipande ulivyokata na weka kwenye sinia.
  • Tandaza vizuri kwa wembamba kwenye sinia na hakikisha rojo limechanganyika na kupondeka vyema.
  • Weka sinia lako mahala pakavu na penye mwanga kisha kila baada ya masaa mawili au zaidi (kulingana na hali ya hewa ya eneo husika) koroga na tandaza kwa upya.
  • Endelea na zoezi la kukoroga, kutandaza na kuacha mpaka pale utakapoona rojo limekauka, limebadili rangi kuwa ya kahawai na limeanza kutoa mafuta na halishiki tena kwenye kijiko.
  • Chukua bakuli, na kitambaa safi cheupe kisha anza kukamua mafuta kidogokidogo mpaka utakapomaliza rojo lote.
  • Baada ya hapo, mafuta yako yapo tayari kwa matumizi.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *