Kabla ya kujifunza namna ya kusindika nanaa (mint), ni vyema tukaangalia kwa ufupi kuhusu zao hili na namna ya kuzalisha.
Nanaa ni zao la majani ambalo huzalishwa na kutumiwa kama kiungo. Zao hili la viungo ni muhimu kuoteshwa kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha na wenye pH kuanzia kiwango cha 6 hadi 7. Zao hili huoteshwa kwa kutumia mapandikizi au kwa kutumia miche na njia zote hufanya vizuri katika uzalishaji.
Uoteshaji wa nanaa
Hakikisha shamba la kupandia limelimwa na kutifuliwa vyema na wakati wa kuotesha hakikisha umeandaa mbolea ya samadi ili kuoteshea.
Zao hili huitaji nafasi ya mita tatu kati ya mche na mche na mita nne kati ya mstari na mstari.
Matunzo
Zao la nanaa linahitaji matunzo hasa palizi ili kuondoa magugu ambayo huota mara kwa mara kutokana na kuwa, huitaji maji kwa wingi hivyo ushawishi wa magugu kuota ni mkubwa.
Mavuno
Baada ya kuotesha, nanaa huchukua wiki tatu mpaka mwezi kuanza kuvunwa na uvunaji wake hufanyika kila wiki kwa kukata majani na kisha kuacha yachipue tena.
Namna ya kusindika/kukausha nanaa
Mmea wa nanaa unaweza kutumika ukiwa katika mfumo wa majani (kavu ama mbichi), nanaa ya unga na nanaa ya mafuta.
Mara nyingi zao hili limekuwa likivunwa na kuuzwa majani tu, jambo ambalo kama kutakuwa na mavuno mengi na uhitaji mdogo, ni vema kusindika ili kuborezha uhifadhi wake kwa muda mrefu.
Ili uweze kusindika na kuzalisha bidhaa bora itakayo hifadhiwa kwa muda mrefu, na kukidhi hata masoko ya kimataifa, ni lazima kufuata utaratibu mzuri. Hapa tutakuelekeza vifaa husika na utaratibu rahisi wa kusindika nanaa nyumbani kwako.
Vifaa
Wakati wa kusindika nanaa, unahitajika kuwa na vifaa ambavyo ni solar drier, maji safi na salama, chombo cha kuoshea, kinu pamoja na mtwangio au mashine ya kusaga na chekecheke.
Hatua
· Chukua majani ya nanaa uliyovuna kutoka shambani kisha chambua kuondoa takataka zingine kama magugu ambayo huenda yamevunwa pamoja na nanaa.
· Weka majani hayo kwenye chombo cha kusafishia, kidogo kidogo huku ukimwaga maji ili kuweza kuondoa mchanga ama udongo.
· Baada ya kusafisha weka kwenye solar drier yako kiasi kidogo ili ziweze kukauka kwa haraka.
· Acha kwa muda wa siku mbili hadi tano ili zikauke vizuri. Ukaukaji wa nanaa utategemea hali ya hewa ya wakati huo.
· Baada ya kukauka, chukua kiasi kidogo kidogo na kisha saga kwenye mashine au twanga kwenye kinu ili kupata unga kama wa majani ya chai.
· Baada ya kutwanga, chekecha ili kupata unga wa nanaa ulio laini na hapo inakua tayari kwa matumizi.
· Chukua unga wa nana weka kwenye chombo kisafi tayari kwa ajili ya kufungasha na kwenda sokoni.
· Chukua mifuko maalumu ulioandaa kwa ajili ya kufunga nanaa yako iliosagwa, na ukishafunga peleka moja kwa moja kuuza.
Matumizi ya nanaa
Nanaa iliyotwangwa hutumiwa kama kiungo cha chai, chemsha maji kisha weka kiasi kidogo cha nanaa kisha endelea kuchemsha kwa dakika kadhaa ili kupata maji yenye ladha nzuri ya nanaa. Kama wewe ni mtumiaji wa sukari unaweza kuongeza kiasi kidogo cha sukari kufuatana na uhitaji wako.
Faida ya nanaa mwilini
Nanaa ni moja kati ya mimea yenye faida katika mwili wa binadamu.
Zifuatazo ni baadhi ya faida za nanaa
· Hutumika kama kiungo katika vinywaji baridi kama vile juisi na smoothie.
· Hutumika kuweka harufu nzuri katika vyakula mbali mbali, hutumika pia kwenye madawa kama vile dawa za meno, dawa za kikohozi kwani husadikika kupambana na magonjwa mengi katika mwili wa binadamu.
· Nanaa huondoa harufu mbaya ya kinywa cha binadamu, unaweza kutafuna ama kunywa maji yaliochemshwa na nanaa.
· Inasadikika kuchangia katika kuondoa msongo wa mawazo kutokana na harufu nzuri na ladha ya kufurahisha.
· Husaidia kuuweka sawa mfumo wa umeng’enyaji chakula mwilini.
· Matumizi ya mara kwa mara husadikika kusaidia kuzuia kutokea kwa ugonjwa wa saratani.
Soko
Soko la nanaa linapatikana hasa kwenye mahoteli ya kitalii na kwenye maduka makubwa kama supermarket na pia hutafutwa kwa wingi na watu binafsi.
Kwa maelezo zaidi wasiliana na Mosses Anney kwa simu (+255 624 001 036)