Augustino Olturia: Mfugaji wa ng’ombe wa maziwa
“Nimefanya shughuli za kilimo na ufugaji toka mwaka 1984. Sikuwa nimefahamu kuwa naweza kuwalisha ng’ombe wangu kwa kipimo na nikapata mafanikio mpaka niliposoma jarida la Mkulima Mbunifu.”
Ni maneno ya Mkulima msomaji wa jarida la Mkulima Mbunifu Bw. Agustino Olturia kutoka Kijiji cha Oloigeruno Mkoani Arusha.
Bwana Agustiono anasema kuwa jarida la Mkulima Mbunifu limemsaidia kuboresha ufugaji wake kwani amebadili anavyowatunaza ng’ombe wake; alikuwa akiwalisha ng’ombe wake katika hali ya kawaida tu lakini toka alipojifunza kufuata vipimo vilivyopendekezwa ameona mabadiliko kwa ng’ombe wake jambo linalomuongezea faida zaidi.
Mbali na ufugaji anafanya kilimo cha mboga mboga kama kabichi, nyanya, vitunguu na kale. Anasema kilimo kinalipa sana kwa mtu anayefanya kwa umakini, japo tatizo mara nyingine linakuwa ni soko.
Mkulima huyu kwa kudhihirisha hilo anasema ameweza kuwasomesha watoto wake watano katika ngazi ya sekondari hadi chuo kikuu. Kwa uzoefu wake anasema zao la nyanya na kabichi linalipa zaidi.
Anashauri wakulima wenzake kujiunga kwenye vikundi na kuomba kupatiwa jarida la Mkulima Mbunifu ili waweze kufaidika kama yeye na wenzake.