Kila mwaka, watoto wengi chini ya miaka 5 nchini Tanzania hufa kwa sababu ya chakula duni na kisichotosha. Watoto hawa hawapati chakula chenye vitamini, madini ya iodini na chuma ambayo yanahitajika kwa afya na ukuaji mzuri. Hali hii inasababisha utapiamlo.
Utapiamlo unamaanisha upungufu, kupita kiasi, au kukosa usawa katika ulaji wa vyakula na virutubishi muhimu mwilini.
Aina mbali mbali za utapiamlo
Utapiamlo unajitokeza katika makundi tatu
(i) Kupoteza nyama na misuli mwilini (uzito mdogo, kudumaa) na kuwa na uzani wa chini (uzani wa chini-kwa-umri). Kawaida hii husababishwa na kukosa chakula cha kutosha au kuugua kwa muda mrefu kama vile kuhara. Kudumaa ni sugu, kwa hivyo kuna matokeo ya muda mrefu yasiyoweza kurekebishwa.
(ii) Utapiamlo unaohusiana na virutubishi, ambavyo ni pamoja na ukosefu wa vitamini na madini muhimu) au virutubishi kuzidi mahitaji.
Aina hizi mbili za utapiamlo hufanya watoto wawe katika hatari zaidi ya magonjwa na kifo.
(iii) Uzito kupita kiasi, unene kupita kiasi na magonjwa yasiyoweza kuambukizwa yanayohusiana na lishe (kama ugonjwa wa kisukari, ugonjwa wa moyo, na saratani zingine).
Inakadiriwa kwamba zaidi ya watoto milioni 2.7 wa Tanzania walio chini ya umri wa miaka 5 wanadumaa na zaidi ya 600,000 wana shida ya utapiamlo mkali.
Ingawa kuna tofauti kubwa katika hali ya lishe ya watoto chini ya miaka 5, maeneo na mikoa yenye umasikini mkubwa, hali mbaya ya uchumi, afya duni ya mama, yanachangia asilimia kubwa ya utapiamlo, hii ina maanisha kwamba familia zinashindwa kutosheleza mahitaji ya lishe kwa watoto.
Zalisha mazao ya chakula kwa matumizi ya nyumbani
Kuna haja ya kuzalisha vyakula vyenye virutubishi muhimu kwa watoto ikiwa ni pamoja na vyakula vya kuipa mwili nguvu, vyakula vya kujenga mwili, vitamin na madini.
Chakula cha mboga-mboga ni chanzo cha vitamin na madini yanayowezesha mwili kujenga kinga dhidi ya magonjwa. Upatikanaji na uwepo wa mboga kwenye chakula cha familia unategemea uwezo wa kuzalisha mboga nyumbani au kununua sokoni.
Kuanzisha shamba la jikoni hapo nyumbani inakupa nafasi ya kuzalisha chakula hasa mboga-mboga kwa matumizi ya nyumbani kwani unakua na uhakika pia wa njia ya uzalishaji kwani mboga nyingine zimezalishwa kwa madawa ya kemikali ambayo ni hatari kwa afya ya binadamu.
Ikiwa una eneo dogo, unaweza kutengeneza bustani la gunia, yaani sack garden.
Pia ni vema kuchanganya mboga inayokua kwa muda mfupi kama spinach, kabeji, mboga za kienyeji, maharagwe, mchicha, na kadhalika na yale mazao yanayochukuwa muda mrefu kama viazi vitamu, ndizi na kadhalika. Mchanganyiko huu unakuhakikishia virutubishi tofauti katika mlo.
Kula vyakula aina tofauti
Watoto wenye umri wa miezi 6 na zaidi, wapewe chakula cha ziada tofauti-tofauti kwa viwango vidogo mwanzoni na kuongeza kadri wanapokua. Vyakula hivi ni pamoja na protini (nyama, maharagwe, samaki, mayai n.k) na vyakula vya nguvu (nafaka – mahindi, mtama, mahindi, mchele), mboga na matunda.
Upungufu wa virutubisho unashughulikiwa vizuri kupitia mikakati kama bustani za nyumbani na bidhaa ya mifugo wadogo kama kuku wa mayai na mbuzi kwa maziwa.
Matumizi ya vyakula vya asili kama vile mboga kwenye milo yote kwa viwango vidogo na za mara kwa mara zinaweza kupunguza utapiamlo.
Zingatia lishe
Kwa sababu lishe ni muhimu katika ukuaji wa jumla wa mwili na akili kwa watoto, kuna haja ya kuzingatia hasa miaka miwili ya kwanza ya maisha ya mtoto ili kuzuia athari za utapiamlo.
Hii inahitaji kushughulika na vihatarishi kuanzia chakula duni, magonjwa hadi upatikanaji duni wa maji safi ya kunywa na usafi wa mazingira.