Mnamo tarehe 7 Machi, 2025 Wizara ya Afya kupitia mifumo yake ya ukusanyaji wa taarifa na ufuatiliaji wa magonjwa ilipokea taarifa za uwepo wa wahisiwa wenye dalili za vipele usoni, mikononi, miguuni na sehemu nyingine za mwili. Dalili hizi ziliambatana na homa, maumivu ya kichwa, vidonda kooni, maumivu ya viungo vya mwili ikiwemo misuli na mgongo. Kati ya wahisiwa hao mmoja ni dereva wa magari ya mizigo aliyetoka nchi jirani kwenda Dar es Salaam.
Baada ya kupokea taarifa za wahisiwa, sampuli zilichukuliwa na kupelekwa maabara ya Taifa kwa uchunguzi. Mnamo tarehe 9 Machi, 2025 uchunguzi wa kimaabara umethibitisha kuwa wahisiwa wawili (2) wana maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Mpox. Hivyo, hadi kufikia sasa jumla ya wahisiwa wawili (2) wamethibitika kuwa na ugonjwa wa Mpox nchini.
Wizara ya Afya, inawahakikishia wananchi kuwa Serikali imejipanga kudhibiti ugonjwa huu na hasa kutokana na uzoefu tulionao wa kudhibiti magonjwa ya mlipuko. Serikali inaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa katika ngazi zote, upimaji wa watu wanaoingia na kutoka kupitia mipaka ya nchi, kuimarisha utoaji wa elimu ya afya na kuhamasisha jamii ili kuwawezesha wananchi kuchukua hatua za kujikinga.
Kwa kuzingatia kuwa magonjwa mengi yanayosababishwa na virusi hayana tiba mahususi ila mgonjwa anahudumiwa kulingana na dalili alizonazo, Wizara inawasihi na kuwasisitiza wananchi wote kuzingatia na kutekeleza afua za kujikinga kama ifuatavyo:
- Kuwahi katika kituo cha huduma za afya kwa uchunguzi na matibabu unapoona mojawapo ya dalili za ugonjwa wa Mpox au piga simu nambari 199 bila malipo.
- Kuepuka kuchangia vitu kama nguo na matandiko ambavyo vimetumiwa na mtu mwenye dalili za Mpox.
- Kuepuka kugusana kwa kupeana mikono, kubusiana, kukumbatiana au kujamiiana na mtu mwenye dalili za Mpox.
- Kuepuka kugusa majimaji ya mwili ya mtu mwenye dalili za Mpox.
- Kuepuka kumuhudumia mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa wa Mpox bila kuchukua tahadhari.
- Watumishi wa afya kuzingatia kanuni za kujikinga na magonjwa wakati wote wanapowahudumia wagonjwa ikiwemo wenye dalili za vipele na homa.
- Kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono.
- Wizara ya Afya, itaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa ugonjwa huu, kadri taarifa za ufuatiliaji na uchunguzi zitakavyopatikana. Wizara inashauri wananchi kuendelea na shughuli za kila siku kwa kuzingatia tahadhari za kuzuia maambukizi ya ugonjwa huu.