Suala la afya bora ni suala la muhimu katika maisha ya kila mmoja wetu na jamii kwa ujumla. Bila afya hakuna furaha, amani wala shughuli yoyote ile ya maendeleo. Afya ndio msingi wa maisha yetu ya kila siku. Siku hizi si ajabu sana kusikia au hata kushuhudia watu wengi wakisumbuliwa na matatizo mengi ya kiafya, suala hili linachangiwa na mambo mengi ikiwemo hali ya mazingira au tabia za watu.
Upuuzaji wa matumizi ya matunda na mboga mboga unachangia kwa kiasi kikubwa matatizo mengi ya kiafya.
Matunda ni moja ya sehemu ya chakula muhimu kwa binadamu kutokana na faida lukuki.
Kuna sababu kadhaa za kwa nini watu hawatumii matunda mara kwa mara, baadhi ya hizo ni kutokujua faida ya matunda kiafya, ukosefu wa uwezo wa kumudu gharama za kula matunda mara kwa mara. Ikiwa wewe ni miongoni mwa watu wanaoshindwa kutumia matunda Mkulima Mbunifu inakusisitiza ujitahidi kuzalisha matunda ya asili nyumbani kwako.
Kila tunda lina viini lishe muhimu kwa afya ya binadamu navyo hutofautiana kutoka tunda moja hadi lingine.
Hata hivyo kwa ujumla wake matunda husaidia kuboresha afya ya mwili kwa kujenga kinga madhubuti dhidi ya magonjwa, vitamin C kutoka kwenye matunda inasaidia ukuaji na utengenezaji wa tishu za mwili, kutengeneza chembe hai nyekundu za damu na faida nyingine kadha wa kadha.
Tengeneza mazoea ya kula matunda kila siku, ili kujenga afya bora.