- Kilimo

Msimu wa mavuno; Hakikisha umefuata kanuni sahihi za kuvuna na kuhifadhi nafaka

Sambaza chapisho hili

Nafaka mbalimbali ambayo ni mazao makuu ya chakula na kibiashara hapa nchini kama vile mahindi, maharage, mikunde mara nyingi wakulima hupoteza hasa wakati wa mavuno kutokana na uvunaji usiokidhi viwango pamoja na uhifadhi duni.

Ukiwa huu ni msimu wa mavuno katika maeneo mbalimbali nchini, Mkulima Mbunifu inatoa rai kwa wakulima kuhakikisha kuwa wanazingatia kanuni sahihi za mavuno ili waweze kupata mavuno bora na yanayokidhi chakula na soko kwa ujumla.

Katika kipindi hiki cha mavuno, wakulima hawana budi kuwa makini sana na kutambua ni kwa namna gani watavuna mazao yao na kuyahifadhi ili kuondokana na upotevu ambao mara nyingi huweza hata kufikia hadi asilimia 20 hadi 30 ya mavuno.

Nini husababisha upotevu wa mavuno

Mara nyingi upotevu hutokana na wakulima wengi kuyaacha sehemu ya mazao shambani kutokana na kushindwa kuyadhibiti na wakati mwingine kupotea njiani wakati wa kupeleka au wakati wa kuhifadhi.

Aidha, upotevu mwingine hutokea wakati wa kuhifadhi kulingana na aina ya vifaa vinavyotumika kuhifadhia kuwa na urahisi wa kuharibiwa na wadudu na mengine kuoza kutokana na unyevu.

Wakati mwingine wakulima huvuna mazao yakiwa bado hayajakomaa vizuri hivyo kukosa ujazo mzuri unaoshauriwa kitaalamu katika uhifadhi wa zao hili.

Maandalizi sahihi kabla ya kuvuna na kuhifadhi

Kabla ya kuvuna ni muhimu kuandaa vifaa vya kuvuna na kukagua shamba ili kujua kama mazao yamekomaa vizuri. Kwa kawaida kwa mfano kama ni mahindi hukomaa kati ya miezi 3 hadi 8 kutegemeana na aina na hali ya hewa. Unyevu katika punje huwa kati ya asilimia 23 hadi 28.

Dalili za mazao yaliyokomaa

  • Kama ni mahindi, rangi ya majani ya mmea wa mhindi na maganda ya gunzi hugeuka kutoka ukijani na kuwa ya kaki.
  • Sehemu iliyounganisha punje na gunzi huwa nyeusi na punje ya mhindi hung’ara.
  • Kama ni maharage, mmea au majani pamoja na podo huonekana kuwa ya kaki na ukibonyeza podo hupasuka
  • Punje ya maharage huwa imekolea rangi kabisa kulingana na aina ya maharage na hata punje uking’ata huelekea kuvunjika kwa urahisi

Matayarisho kabla ya kuvuna

Vifaa vya kuvunia na kubebea mazao kama vile vikapu, matenga, mapanga, magunia, mashine (combine harvest) kwa wakulima wenye mashamba makubwa.

Vyombo vya usafiri

Mkulima ni lazima kuandaa vyombo kwa ajili ya kusafirishia mazao kutoka shambani hadi nyumbani/ ghalani. Vyombo vya kusafirishia ni kama mikokoteni inayokokotwa na wanyamakazi au ya kusukumwa/ kuvutwa na mikono, matela ya trekta pamoja na magari.

Vifaa na sehemu ya kukaushia

Hivi ni pamoja na kichanja bora/ chekeche, mikeka, maturubai, sakafu safi, na ghala safi la kuhifadhia.

Kuvuna

Ni muhimu kuvuna mapema ili kuepuka upotevu wa mazao unaoweza kusababishwa na wadudu na wanyama waharibifu, moto, wezi na mvua.

Njia za kuvuna

Njia zinazotumika kuvuna mazao ni kwa kutumia mikono au mashine.

Kuvuna kwa mikono

Hii njia hutumiwa na wakulima ambao wana mashamba madogo na uwezo wao kupata mashine ni mdogo pia. Mashina ya mahindi yaliyokomaa hukatwa kwa panga, na kurundikwa mahali pamoja kisha magunzi ya mahindi huondolewa kwenye mashina kwa kutumia mikono.

Kwa maharage, mmea wa maharage hung’olewa kwa kutumia mikono, kisha hukusanywa katika turubai kwa ajili ya kupigapiga tayari kupata maharage.

Kuvuna kwa mashine

Njia hii hutumiwa na wakulima wenye uwezo na mashamba yao ni makubwa. Kama ni mahndi, mashine hukata mashina ya mahindi yaliyokauka, kuyamenya na kupukuchuwa kwa wakati mmoja.

Kusafirisha

Mazao husafirishwa kutoka shambani hadi sehemu ya kukaushia kwa kutumia, matoroli, kubeba kichwani, kutumia baiskeli, kutumia wanyamakazi kama punda, kutumia mikokoteni ya wanyamakazi, kutumia mateka ya trekta pamoja na magari.

Kukausha

Ili kupunguza upotevu na kudumisha ubora, ni muhimu kuzingatia njia bora za kukausha mazao.

Hatua ya kwanza

Huu ni ukaushaji wa awali ambao hufanyika mara tu mahindi yanapotolewa shambani. Ukaushaji huu hufanyika kwa kuyaweka magunzi ya mahindi juu ya turubai, kichanja, sakafu, au kribu. Lengo la kukausha magunzi ni kupunguza unyevu na kurahisisha upukuchuaji.

Pia, kama ni maharage, mara baada ya kung’oa hukusanywa na kutandazwa juu ya turubai ili kukausha mapodo vizuri na baada ya kukauka hupigwa kwa kutumia mti.

Upukuchuaji/upigaji

Kabla ya kuanza kupukuchua au kipigapiga, ni muhimu kuchunguza na kutoa mazao ambayo tayari yameshaanza kuoza au kuwa na wadudu.

Mahindi yanaweza kupukuchuliwa kwa kutumia mikono, mashine, kichanja maalum, au kutumia magunia kisha kupiga. Vivyo hivyo kwa maharage, unaweza kupukuchua kwa kupigapiga ikiwa juu ya turubai kisha kuondoa taka baada ya kumaliza.

Kupepeta na kupembua

Kazi ya kupepeta hufanyika ili kuondoa takataka kama vile majani, mapodo, magunzi, mawe, wadudu, punje zilizooza, kuharibika au kupasuka. Kazi hii inaweza kufanyika kwa kutumia mikono, chekeche, mashine.

Hatua ya pili

Hatua hii hujumuisha ukaushaji wa punje hadi kufikia unyevu unaokubalika kwa kuhifadhi salama. Iwapo kiwango kitakuwa chini ya hapo, basi mazao hushambuliwa kwa urahisi sana na vimelea vya ukungu, na kusababisha kuoza.

Ukaushaji huu hufanyika kwa kusambaza punje za mazao kwenye sehemu yeyote iliyo safi ili kuhakikisha kuwa punje hizo zinakauka bila kuingiliwa na uchafu tena.

Jinsi ya kutambua punje zilizokauka

Utambuzi huu unaweza kufanyika kwa kupima unyevu kwa njia kuu nne ambazo ni:

  • Kung’ata punje: Huwa magumu na hukatika kwa mlio mkali.
  • Kumimina kwenye chombo au sakafu: Hutoa mlio mkali kama wa kuumiza sikio.
  • Kutumia chumvi: Changanya punje na chumvi kiasi kisha mimina kwenye jagi la kioo, na kama chumvi itang’ang’ania kwenye punje basi hazijakauka.
  • Kutumia kipima unyevu: Kuonyesha unyevu wa asilima 13.5.

Kutayarisha mahindi kabla ya kuyahifadhi

Kabla ya kuweka mazao kwenye vifungashio au kuhifadhi ghalani, inabidi kuchukua tahadhari ya kuzuia uharibifu utokanao na wadudu au wanyama kama panya ndani ya ghala.

Hakikisha ghala la kuhifadhia ni safi, lisilovuja na ikibidi changanya mazao na viuwadudu salama. Viuwadudu hivyo vinaweza kuwa ni vile vya asili vinavyotokana na mimea kwa mfano muwarobaini au pareto.

Aidha ni muhimu kutenga kiasi cha mahindi yatakayotumika kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu baada ya kuvuna. Hii ni kwasababu katika kipindi hiki, mashambulizi ya wadudu huwa ni ya kiwango cha chini sana.

Ghala bora la kuhifadhia mahindi

Ghala bora ni chombo chochote kile au jengo lolote lililo imara na lenye sifa zifuatazo;

  • Liwe na uwezo wa kuzuia wadudu, panya, mvua na unyevu kutoka chini.
  • Liwe na nafasi ya kutosha kuweka mazao, kukagua na kutoa.
  • Liwe na uwezo wa kuhifadhi mazao yaliyokusudiwa.

Mahindi au maharage na nafaka zingine yaweza kuhifadhiwa kwenye silo, bini, mapipa maaulumu ya kuhifadhiwa au mifuko maalumu ya kuhifadhia nafaka.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *