- Mifugo

Njia bora ya kugawanya makundi ya nyuki wadogo

Sambaza chapisho hili

Nyuki wasiong’ata maarufu kama nyuki wadogo hufikia kiwango cha kuwa kundi kubwa lenye kuhitaji kuendelezwa kutoka katika mzinga mama na kuelekea katika mzinga mpya.

Zoezi la kugawanya makundi ya nyuki huhitaji utalaamu na uangalifu wa kutosha ili kusaidia ugawanyaji wa kundi kuwa wenye tija kwa mfugaji.

  • Kuna faida kubwa ya kugawanya makundi ya nyuki wasiong’ata Huongeza idadi ya nyuki katika manzuki
  • Husaidia kuongeza uwezo wa shughuli za uchavushaji katika mashamba
  • Hupunguza migogoro kati ya nyuki wa kundi moja
  • Huweza kumpatia kipato kizuri mfugaji wa nyuki kama sehemu ya biashara ya uuzaji wa makundi ya nyuki wasiong’ata.

Zifuatazo ni njia mbalimbali za kugawanya makundi ya nyuki wasiong’ata

  1. Kugawanya makundi kwa kutumia mianzi

Mwanzi utakaotumika hapa ni jamii ya mianzi yenye pingili nene na ndefu kiasi cha futi moja. Mianzi hii hupatikana sehemu za uwanda wa juu wa baridi wa kitropiki. Mwanzi huu utakatwa katika sehemu yake ya katikati na kugawanywa katikati, kisha kutolewa sehemu zote mbele na nyuma na kusafishwa vizuri.

 

 

 

 

Baada ya kusafisha, utakaushwa na kusafishwa tena na kupakwa gundi ngumu ya ulinzi (resini) kuzunguka mwanzi. Kisha utaunganiswa na mpira mweupe mwembamba wenye kipenyo cha milimita tatu kitakachounganishwa katika mzinga na kuunganishwa katika mwanzi.

Mzinga utaunganishwa na mpira huu, uwe ni mzinga wenye kundi lenye nyuki wengi na wenye afya wanaoonekana kuelekea kugawanyika. Baada ya siku 30 nyuki watakuwa tayari wameshaanza kugawanyika na kundi dogo litakuwa tayari limeshaanza kujenga katika mwanzi. Mfugaji atalichukua kundi lililoanza kukua vizuri katika mwanzi na kuliweka katika mzinga mpya.

  1. Kugawanya makundi kwa kutumia mizinga

Unaweza kutengeneza mzinga wenye sehemu tatu, sehemu ya chini ya kuingilia nyuki, sehemu ya katikakati ambapo ndipo nyumba inapokua na kuongezeka kila siku na sehemu ya juu ambapo ni ya kuhifadhi asali.

Muundo huu unaweza kukusaidia kwa namna hii; sehemu ya chini ya nyumba hupanuka na kuwa kubwa na kuifanya sehemu ya katikati kuwa na seli nyingi za mayai. Hivyo kuwa rahisi kuondoa sehemu ya katikati ya mzinga na kuweka kipande kingine kipya na kundi kuendelea kama kawaida.

Kisehemu kilichotolewa huunganishwa na mzinga mwingine na hiyvo kusaidia ukuaji endelevu wa makundi.

  1. Kugawanya makundi kwa njia ya muda

Hii ni njia rahisi na kwa asilimia 90% wafugaji wa nyuki wasiokua wakongwe wameitumia. Kwa kawaida nyuki huwa wachangamfu pale jua linapoanza kukolea wakati wa asubuhi na ifikapo mchana nyuki wengi wafanyakazi huwa wametoka katika mzinga na hapa ndio muda sahihi wa kugawanya makundi haya.

Mfugaji atalitoa kundi lake likiwa na nyumba yake kutoka katika mzinga mama na kuupeleka katika mzinga mpya. Kisha kuurejesha mzinga mama katika eneo husika huku ukiwa na gundi, vishikizio vya koloni na masega ya asali yakiwemo ndani.

Pindi nyuki wafanyakazi wanaporejea hukuta kuwa nyumba yao imeondololewa hapo ndipo malkia mpya hutafutwa na kuendeleza kundi, huanza kujenga upya na baada ya muda wa miezi miwili kundi huwa limerejea katika hali ya mwanzo

  1. Kugawanya makundi kwa njia ya T- PIPE

Mfugaji anaweza kununua pipe za maji za kawaida za plastiki za upana wa robo tatu kipenyo, na kuweka viungio vya kiwiko kisha kuunganisha katika pipe za maji na mdomo wa kuingilia nyuki katika mzinga.

 

 

 

 

Wakati wa kufanya hivyo hakikisha muunganisho huu unaleta alama ya T kisha unganisha katika mzinga mwingine. Unaotoa kundi mama, kadiri nyuki watakavyoendelea kuwepo katika mzinga. Kundi mama litagawanyika ikiwa tayari idadi ya nyuki imeongezeka, nafasi kupungua na uhitaji wa makazi mapya kuwepo, hiyvo kuhamisha himaya katika mzinga mpya.

Hii huweza kufanyika katika kipindi cha miezi miwili hadi mitano kulingana na uwezekano wa mgawanyo wa kundi. Njia hii ni rafiki sana kwani nyuki huweza kugawanywa pasipo kuharibu umbo la nyumba yao.

Kwa maelezo zaidi juu ya makala hii wasiliana na Daudi Ngosengwa Manongi simu namba 0769861063, Mtalaamu wa kilimo Ikolojia na Nyuki, Mradi wa wadudu wachavushaji.

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *