Maziwa ni sehemu ya mlo kamili wenye virutubisho vya kutosha au viini lishe sawia vinavyohitajika katika mwili wa binadamu.
Katika toleo lililopita, tulizungumzia kwa ufupi sana kuhusu usafi wa maziwa na mada hii tutaikamilisha kwa kueleza kwa undani vipengele kadhaa vinavyohusiana na usafi wa maziwa.
Maziwa ni nini
Maziwa ni maji meupe yenye viini lishe yanayokamuliwa kutoka kwenye mifugo mbalimbali ikiwamo ng’ombe, mbuzi.
Maziwa haya ni muhimu sana kwa binadamu yeyote na ndiyo maana madaktari hushauri watoto wachanga kunyonya miezi sita bila kuanzishiwa chakula kingine.
Hii inaonyesha ni kwa jinsi gani maziwa yana ubora katika kuujenga mwili, na kuulinda dhidi ya magonjwa mbalimbali pamoja na kuimarisha mifupa na meno.
Virutubisho vinavyopatikana katika maziwa
Maziwa yana virutubisho mbalimbali kama vile, mafuta asilimia 4% ambayo husaidia kuutia mwili joto.
Aidha, yana protini asilimia 3.8% ambayo husaidia kuujenga mwili pamoja na sukari asilimia 5% ambayo husaidia kuongeza nguvu mwilini.
Maziwa pia yana maji asilimia 86% ambayo husaidia kusafirisha viini lishe ndani ya mwili pamoja na madini asilimia 2% ambayo husaidia kujenga na kuimarisha mifupa na meno.
Faida ya maziwa kiuchumi
Maziwa ya wanyama hususani ng’ombe ni moja ya zao la mifugo ambao linaweza kumpatia kipato mfugaji kwa mwaka mzima.
Mfugaji akitumia zao hili vizuri linaweza kumuinua sana kiuchumi pale ambapo atakuwa anazalisha kwa wingi na kwa usafi na kuuza kwa wahitaji.
Aidha, maziwa yanapopatikana kwa wingi, yanaongeza kiwango cha upatikanaji wa maziwa kwa ajili ya kusindika na hivyo mfugaji kuendelea kukuza pato lake.
Vyanzo vya uchafuzi wa maziwa
Maziwa yanaweza kuwa machafu kutokana na mambo mbalimbali kama vile ng’ombe wagonjwa, kinyesi cha mifugo, vyombo au mashine ya kukamulia isiyosafishwa kwa ubora.
Pili, maziwa yanaweza kuwa machafu pale mkamuaji anapokuwa katika hali ya uchafu (nguo zake, mikono) pamoja na matumizi ya kemikali au madawa ya kutibia mifugo.
Usafi wa maziwa
Ili kuzingatia usafi wa maziwa, ni bora kuzingatia vitu mbalimbali kama vile, ng’ombe mwenyewe awe anatunzwa katika mazingira masafi yasiyo na wadudu kama mbung’o.
Banda analoishi liwe safi na lisafishwe mara kwa mara.
Aidha, sehemu ya kukamulia iwe safi, mkamuaji awe msafi aliyevalia vizuri pasipokuwa na nguo zenye mikanda inayoning’inia kwani inaweza kuingia katika chombo cha kukamulia.
Vyombo vya kukamulia na vya kuhifadhia maziwa viwe visafi vilivyosafishwa kwa maji safi na salama.
Utunzaji na uhifadhi wa maziwa
Maziwa yatokayo katika kiwele cha ng’ombe asiye na ugonjwa wowote ni safi na ni salama kwa matumizi.
Ndani ya maziwa pia kuna bakteria wenye manufaa na ili kuhifadhi maziwa kwa muda mrefu ni muhimu yahifadhiwe sehemu safi na yenye ubaridi ili kuzuia bakteria hawa wasiongezeke.
Inashauriwa maziwa yahifadhiwe kwenye ubaridi wa nyuzi joto 5 za sentigredi ili yaweze kuhifadhika kwa muda mrefu.
Kama hakuna vifaa vya kutunza baridi, inafaa maziwa hayo yafike sokoni ndani ya saa tatu tangu kukamuliwa ili yaweze kutumika na kulinda ubora wake.
Soko la maziwa
Hapa nchini, soko la maziwa lipo hasa ukizingatia kuwa, kwasasa Tanzania imebarikiwa kuwa na wasindikaji wengi wadogo, wa kati na hata viwanda vikubwa ambao wote hawa wanategemea kusindika maziwa kutoka kwa mfugaji.
Ili kuweza kuliteka soko la maziwa, ni vyema kama mfugaji kukamua, na kutunza maziwa katika ubora unaohitajika ili uweze kufikisha sokoni yakiwa safi na yenye ubora wake.