Kumekuwa na maswali mengi kuhusu lishe hasa kutokana na janga la Covid-19. Maswali kama, je, tunapaswa kula nini kujenga na kudumisha mfumo wetu wa kinga ya mwili?
Watu wengi wangependa kujua jinsi wanavyoweza kutumia vyakula vinavyopatikana kwa urahisi shambani au sokoni kuhakikisha afya bora kwa familia zao.
Katika makala hii, tunaangazia mahitaji ya lishe ya makundi tofauti katika familia na jamii.
Ushauri wa lishe kwa watu wazima
Lishe sahihi na kunywa maji ya kutosha ni muhimu kwa afya ya binadamu. Watu wanaokula chakula kilichosawazishwa na kuwa na virutubisho muhimu huwa ya afya na kujenga kinga ya mwili na kupunguza uwezekano wa kupatwa na magonjwa sugu na ya kuambukiza.
Ni vyema kula chakula aina tofauti, chenye viungo tofauti-tofauti, ambavyo vimetoka shambani moja kwa moja na sio vilivyotengenezwa viwandani ili kupata virutubisho sahihi katika mwili.
Pia, epuka matumizi ya sukari, mafuta, na chumvi nyingi ili kupunguza hatari za kuwa na uzito kupita kiasi, magonjwa ya moyo, kiharusi, ugonjwa wa sukari na aina fulani za saratani.
Kula vyakula visivyotengenezwa viwandani
- Kula matunda, mboga-mboga, mikunde (maharagwe, kunde, soya, ndengu, njengere), karanga na nafaka nzima – ambayo haijakobolewa (mahindi, mtama, shayiri, ngano, mchele wa kahawia), mizizi kama vile viazi, nduma, au mihogo), na vyakula kutoka vyanzo vya wanyama (kuku, mbuzi, ng’ombe, samaki, mayai na maziwa).
- Viwango: Kila siku, kula: gramu 180 vya nafaka, vikombe viwili na nusu ya mboga, vikombe viwili vya matunda, gramu 160 ya nyama na maharagwe. Nyama nyekundu inaweza kuliwa mara 1-2 kwa wiki, na kuku mara 2-3 kwa wiki. Kula milo mikuu mitatu kwa siku (asubuhi, mchana na jioni) na milo midogo miwili (saa nne na saa kumi).
- Kwa vitafunio, chagua mboga mbichi na matunda freshi badala ya vyakula vyenye sukari, mafuta na chumvi nyingi.
- Usipike mboga na matunda kwa joto la juu na kwa muda mrefu kwani hii inasababisha upotezaji wa vitamini muhimu.
Kunywa maji ya kutosha kila siku
- Maji ni muhimu kwa maisha. Inasafirisha virutubishi na misombo katika damu, husawazisha joto la mwili wako, huondoa taka, na kusimamia viungo vya mwili.
- Kunywa vikombe 8 – 10 vya maji kila siku.
- Maji ni chaguo bora, lakini unaweza pia kunywa vinywaji vingine, matunda na mboga-mboga ambayo yana maji. Kwa mfano, juisi ya limau (iliyoingizwa kwenye maji na isiyotiliwa sukari), chai na kahawa (lakini kuwa mwangalifu usitumie kahawa / kafeini nyingi), na epuka juisi na vinywaji vilivyo na sukari nyingi.
Kula chumvi na sukari kidogo
- Wakati wa kupika na kuandaa chakula, punguza kiwango cha vitoweo vyenye madini mengi ya Sodiamu (mfano, sosi ya soya na sosi ya samaki).
- Punguza kiasi ya chumvi unayotumia kila siku. Isizidi gramu 5 (takriban kijiko kimoja cha chai), na utumie chumvi yenye Iodini au madini joto (Iodized).
- Epuka vyakula kama vitafunio vyenye chumvi na sukari nyingi.
- Punguza vinywaji kama soda, juisi za matunda zilizowekwa sukari nyingi
- Chagua matunda safi badala ya vitafunio vitamu kama vile keki na chokoleti.
- Unapotumia mboga mboga au matunda na mboga kavu, chagua aina isiyokuwa na chumvi na sukari nyingi iliyoongezwa.
Pombe na sigara
Unywaji na matumizi ya vileo kupita kiasi inaleta madhara katika mwili kwani hufanya mwili kupoteza maji mengi kwa njia ya mkojo, hufanya ngozi kuwa kavu, na mnywaji hawezi kifikiria na kufanya maamuzi ipasavyo.
Epuka uvutaji wa sigara (na kwa wale wanovuta, punguza). Sigara ina kemikali zinazochangia kuzorota kwa kinga ya mwili, madhara ya mapafu na magonjwa kama saratani na msukumo wa damu.