Ufugaji wa kuku wa kienyeji chotara ni ufugaji ambao hujumuisha muunganiko au mchanganyiko wa aina mbili tofauti za kuku.
Kuku chotara wana faida nyingi sana kwa mkulima ikiwa ni pamoja na ustahimilivu wa magonjwa hivyo kupunguza gharama za kutibu.
Utagaji mkubwa wa mayai mengi mpaka kufikia 240 kwa mwaka kama ukiwalisha vizuri endapo watalishwa vizuri.
Halikadhalika, kuku hawa wanakua haraka na wana uwezo wa kufikisha mpaka kilo tatu(3), kwa muda wa miezi mitatu na hutumika kwa ajili ya kuku wa nyama au wa mayai.
Ufugaji rahisi wa kibiashara
Kama utahitaji kufuga kuku chotara kibiashara usimwachie kuku kuhatamia mayai kwani unampotezea muda wa kutaga.
Kusanya mayai na weka kwenye mashine ya kutotolea vifaranga.
Ukitaka kupata faida kubwa usinunue chakula bali tengeneza chakula cha kulishia kuku mwenyewa kwani bei za vyakula mara nyingi huwa juu sana.
Hatua za ufugaji
Ili kufanya ufugaji wenye ufanisi kwa kuku chotara hakikisha unafanya mambo yafuatayo;
- Andaa banda lako ambalo linafaa kwa matumizi ya ufugaji wa kuku (kulingana na wingi wa kuku unaohitajia kufuga), banda la kuku linatakiwa liwe linapitisha hewa ya kutosha.
- Tafuta kuku wa kienyeji matetea (majike) na jogoo la kisasa aina yoyote ile ambayo inafaa au unahitaji kisha wachanganye kuku wa kienyeji na jogoo wa kisasa katika banda moja.
- Hii itafanya uweze kupata mayai yenye mchanganyiko wa kuku.
- Wakati wa kutotolesha kutotolesha mayai ambayo umeyapata kutokana na mchanganyiko huo, unaweza kutumia mashine za kutotoleshea mayai au unaweza kuwatumia kuku wa kienyeji kuhatamia mayayi hayo.
- Baada ya wiki tatu, yaani siku 21 vifaranga watakuwa tayari kutotolewa kwa kutumia matetea ya kuku wa kienyeji au mashine ya kutotolesha vifaranga kwa ajili ya matunzo mpaka wakiwa wakubwa.
- Vifaranga vikishakuwa tayari chanjo muhimu inahitajika ili kuzuia vifo na milipuko ya magonjwa mbalimbali.
- Vifaranga kwa muda wa wiki tatu hadi nne wanahitaji joto la kutosha, kwa ajili ya ukuaji afya njema.
Utaratibu wa kinga za magonjwa kwenye kuku chotara
Siku | Aina ya chanjo |
Siku ya 1 | Mahepe (Mareks Disease) |
Siku ya 3 | Mdondo/Kideri(Newcastle disease) |
Siku ya 10 | Gumboro |
Siku ya 18 | Gumboro |
Siku ya 21 | Mdondo/Kideri(Newcastle disease) |
Siku ya 21 | Ndui ( Fowl pox) |
Wiki ya 12 | Homa ya matumbo (Fowl typhoid) |
Namna ya kufanya
- Siku ya kwanza hadi siku ya tatu vifaranga wapatiwe glukosi na siku ya 1 hadi ya 5 vifaranga wapewe vitamini.
- Usichanganye maji ya chanjo na vitamini au glukosi
- Chanjo ifanyike wakati wa jioni au asubuhi. Chanjo isifanyike wakati wa mchana kamwe.
- Hakikisha huchanji kuku wagonjwa bali wenye afya.
- Ukishachanja, maji na chanjo, kuku wanywe maji hayo kwa muda wa masaa mawili tu.
- Baada ya masaa mawili mwaga maji na osha vyombo vya maji na uweke maji safi yaliyochanganywa na vitamini.
- Tumia vyombo vya plastiki wakati wa kuchanganya na kuwapa kuku maji ya chanjo
- Wanyime kuku maji kwa masaa mawili kabla ya kuwapa kuku maji ya chanjo.
- Weka kumbukumbu za chanjo uliyotumia ikiwemo toleo la chanjo,(batch number).
- Vifaranga wapewe dawa ya kuzuia ugonjwa wa kuharisha damu (cocidiosis) kwa muda wa siku tatu mfululizo mara wafikishapo umri wa siku saba.
- Vifaranga wapewe dawa ya minyoo wafikishapo umri wa miezi miwili na baada ya hapo wapewe dawa ya minyoo kila baada ya miezi mitatu.