Moja ya changamoto kubwa sana katika ufugaji wa samaki ni uchafukaji wa maji kwenye bwawa ambao hupelekea kutokukua vizuri kwa samaki na kutokuwa na mavuno kwa wakati.
Kama mkulima mbunifu ni vema sana kuwa mbunifu katika kutatua changamoto ambazo zinajitokeza katika mradi wako.
Ili maji yasichafuke kwa haraka ni vema sana mfugaji apandikize samaki kulingana na ukubwa wa bwawa lake kwa mfano; kama bwawa lako ni mita za mraba 200 ulipaswa kupandikiza samaki 2000 ni vema sana ukapandikiza kwa idadi hiyo.
Endapo idadi itazidi kuliko iliyohitajika hapo uchafukaji wa maji utatokea kwa haraka yaani inaweza kukulazimu kila baada ya siku tatu kupunguza na kubadilisha maji kwenye bwawa lako.
Nini cha kufanya ili bwawa liweze kuzalisha na kutunza samaki wengi
Ili bwawa lako liweze kupokea samaki wengi ni vema kuhakikisha unaweka miundo mbinu rafiki katika bwawa ili kuongeza hewa. Pia ikiwezekana weka na mifumo ya kuchuja maji kwenye bwawa.
Kwa kuweka mifumo ya uchujaji maji kwenye bwawa, kutamsaidia mfugaji kama alijenga bwawa la samaki 2000, kwa njia hii sasa anaweza kupandikiza mpaka samaki 4000 au 5000 katika bwawa hilo hilo. Kikubwa zaidi ni kuhakikisha hewa inaongezwa kwenye bwawa kulingana na uhitaji wa samaki wako na hii ni kwa kuweka mfumo huu wa uchujaji wa maji.
Kwa wafugaji wengi wakubwa hutumia sana mifumo hii kwa kuweka mashine kubwa za umeme ili kuchuja maji na kuongeza hewa kwenye bwawa.
Wafugaji wengi katika mfumo huu hupata ahueni ya ubadilishaji wa maji kwani mfumo husaidia ubadilishaji kutokuwa wa mara kwa mara na pia hupelekea samaki kukua vizuri sana kwa muda mfupi.
Ili kusaidia wafugaji wengine kuongeza ufanisi kwenye mabwawa yao mfumo huu rahisi ambao unatumia umeme kidogo hasa katika upande wa mashine ya kupandisha maji, unaweza kutumia hata kwa nishati ya jua. Mfumo ni mzuri kwa mfugaji kwani hupunguzia gharama ya maji na hata vifo vya samaki ambavyo hutokana uchafukaji wa maji.
Kazi kubwa ya mfumo ni kuchuja maji, kuongeza kiwango cha hewa kwenye bwawa na pia hupunguza kiwango cha rangi ya maji yaani ukijani wa kwenye maji hupungua hivyo kufanya maji kuwa katika hali inayotakiwa.
Mahitaji muhimu ili kufanikisha kujenga mfumo huu
Tofali
Kazi ya tofali ni kujenga vyumba vidogo vyenye urefu na upana wa mita moja na kina cha mita moja kutoka chini, hivyo kila chumba kitakuwa kinahifadhi lita 1000 za maji ambayo katika mfumo huu kutajengwa vyumba vitano na kila chumba kitakuwa na kazi yake.
Sementi, mchanga, kokoto, nondo na simenti ya maji
Kazi ya vifaa hivi vyote vitasaidia katika ujenzi na hivyo kufanya bwawa kuwa imara na la kudumu katika muda wote ambao mfumo unabidi ufanye kazi. Pia vinasaidia kuzuia maji yasiweze kutoka nje hivyo ni vyema mjenzi awe mzoefu na masula ya ujenzi.
Bomba ndogo za robo tatu
Kazi ya bomba hizi kuwekwa kila baada ya chumba ambacho hutumika kuchuja maji na kuyapeleka kwenye chumba kingine.
Mashine ndogo (motta)
Hii ni kwa ajili kuchukua maji kutoka ndani ya bwawa na kuleta kwenye vyumba ambavyo vimejengwa kwa ajili ya uchujaji wa maji. Mashine hii hutumia umeme mdogo wa majumbani.
Tajwa hapo juu ndiyo mahitaji ya msingi katika kujenga mfumo huu rahisi kwa ajili uchujaji wa maji na kuongeza hewa. Mfumo huu unatumia vitu ambavyo vipo katika mazingiira yetu bila kuhitaji matumizi yeyote ya kemikali kwani hufanywa kwa kuzingatia misingi sahihi ya kilimo hai. Maji haya ni salama pindi yanapohitajika kutumika kwenye kilimo.
Hatua za ujenzi wa mfumo huu
Kuna hatua muhimu ya kufuata kabla ya kuanza kujenga mfumo huu wa uchujaji wa maji katika bwawa;
- Anza kwa kupima ukubwa wa vizimba au vyumba kwa ajili ujenzi. Pima ukubwa kuanzia urefu mita moja hadi na moja na nusu na upana wa mita moja au moja na nusu.
Ukubwa wa vizimba unaweza kuongezeka endapo bwawa lako ni kubwa zaidi ya wastani wa kuanzia mita za mraba 300 ili kufanya kiwango cha maji kinachochujwa kuwa kikubwa.
Wastani wa maji yanayochujwa katika chumba kimoja ni kati lita 1000-3000, na upimaji huu pia ukizingatia idadi ya vyumba ambayo ni vyumba vitano vyote vikiwa na uwiano unaofanana.
Katika ujenzi huu hakikisha kuwa kina cha katika kila kisimba kinakuwa na urefu wa mita moja. Hakikisha vipimo vyako vinapimwa karibu kabisa na bwawa ili kufanya unyonyaji wa maji kirahisi. Hakikisha ujenzi wako unagusa ukuta wa bwawa kabisa, na vipimo viwe vimenyooka katika hali nzuri.
- Anza kujenga bwawa lako kwa kuweka kozi mbili au tatu za msingi ili kuongeza uimara wa vizimba vyako na changanya simenti na mchanga katika kiwango kizuri inavyoshauriwa kitaalamu katika ujenzi. Hakikisha pia kuwa tofali unazotumia ni imara na zenye ukubwa wa inchi 5 hadi 6.
- Anza kupandisha tofali kwenda juu kwa kujenga kozi 3 hadi 4 na tofali hizo zikiwa zimesimama vizuri katika hali ya mnyoofu kasha kamilisha ujenzi wa kujenga visimba kwa tofali katika kila sehemu.
- Anza kukata nondo zenye ukubwa wa mm 12, urefu wa nondo ndogo utaendana sanjari na kina cha kizimba chako ambacho wastani wake ni mita moja.
Weka nondo zako kila pembe ya mwisho ya kizimba chako, yaani kizimba kikiwa na kina cha urefu wa mita tano na upana wa mita moja. Mwanzo wa kupima weka nguzo na mwisho wa kupima weka nguzo na kufanya hivyo utakuwa umeongeza uimara.
Kama ujenzi wa vizimba ni vidogo sio muhimu sana kujenga kwa kutumia nondo au uwekaji wa nguzo katika ujenzi, matumizi ya nondo au kutumia nguzo ni kuongeza uimara wa mradi wako.
- Baada ya kukamilisha muundo wa ujenzi, anza kwa kuweka vipande vidogo vya bomba. Bomba hivi ziwe zenye ukubwa usiozidi nusu inchi na weka vipande visivyozidi kumi kwenye kila chumba kimoja.
Uwekaji wa bomba hizi zitakuwa kwenye hali ya mlalo ili maji yaweze kutiririka kwa urahisi zaidi. Bomba zitakazowekwa katika chumba cha kwanza zitakuwa juu kuliko zile bomba zitakazowekwa katika chumba cha tano au cha mwisho.
- Malizia ujenzi wako kwa kupiga plasta kwenye kila kizimba na hakikisha unaweka uwiano mzuri wa simenti na mchanga ili kufanya maji yakae zaidi kwenye kila kizimba.
Weka simenti ya maji (waterproof cement) na mwagilia maji kwa muda wa siku mbili ili kufanya uimara wa visimba vyako. Kwa kufanya hivyo, ujenzi kamili wa vizimba kwa ajili ya mfumo wa uchujaji wa maji utakuwa umekamilika na tayari kwa ajili ya kuanza kufanya kazi.
Kazi ya kila chumba katika mfumo huu wa uchujaji wa maji
Kazi ya chumba cha kwanza
Chumba hiki huwekwa mawe makubwa /sponchi za godoro kulingana upatikanaji wake kirahisi, kazi kuu ya chumba hiki nikuchuja uchafu ambayo unaonekana kirahisi,kama vile vinyesi vya samaki, mabaki ya chakula na uchafu mwingine ambao uliingia kwenye bwawa hivyo uchafu wote utabaki kwenye hayo mawe au sponchi.
Chumba cha pili
Mawe ya wastani uchuja uchafu ambao utakuwa umepita kutoka chumba cha kwanza hivyo hapa huacha kabisa aina zote za uchafu na kufanya maji kubaki bila kinyesi au mabaki ya chakula mengine.
Chumba cha tatu
Chumba huwekwa majani aina ya Lettus ambayo huota za sana kwenye mazingira yetu hususani kwenye mabwawa kandokando ya ziwa au mito.
Kazi ya majani ni kufyonza baadhi za kemikali ambazo zipo ndani ya maji kama vile ammonia, carbon na aina nyingine za kemikali ambazo zinapatikana kwenye maji.
Majani hutumia mizizi yake kufyonza kemikali hizo na kutumia kama sehemu yake yakujitengenezea chakula, hivyo kitendo cha maji kupita katika chumba hiki hupunguza sana kiwango cha kemikali hususani ammonia ambayo hutokana na kinyesi cha samaki mwenyewe.
Majani haya hatushauri yapandwe ndani ya bwawa licha ya kuwa na kazi nzuri ya uchujaji wa uchafu kupitia mizizi yake kutokana na mimea nyakati za usiku huitaji hewa ya oksijeni hivyo kuleta ushindani wa hewa nyakati za usiku na matokea yake hupelekea vifo kwa samaki.
Sifa ya majani haya pia ni kuzaliana kwa wingi pindi unapopandikiza kwenye bwawa hivyo kufanya ongezeko la jamii kuwa nyingi zaidi na kuleta ufanisi wa kazi ya uchujaji mzuri wa maji
Chumba cha nne
Huwekwa mkaa au activated carbon ambayo ni malighafi yanayopatikana kirahisi. Kazi kuu ya malighafi hizi ni kupunguza kwa kuua kiwango cha ukijani uliopo kwenye maji, na fahamu kuwa mkaa hutoa carbon ambayo husaidia kuua kiwango cha ukijani kwenye maji.
Chumba cha tano na cha mwisho
Huwekwa mchanga na kokoto ndogo ndogo ambayo hatua hii ya mwisho ndiyo hukamilisha uchujaji wa maji na kurudisha tena kwenye bwawa. Aidha, kitendo cha maji kudondoka tu husaidia kuongeza hewa kwenye bwawa kwa njia ya mawimbi.
Nini cha kufanya ili mfumo huu ufanye kazi kwa ufanisi
Katika hatua zote hizi ni muhimu sana kuwasiliana na mtaalamu katika kila hatua kwa ushauri ili kufahamu ukubwa wa bwawa lako na kama litahitaji ukubwa zaidi ili mfumo huu uwe na matokeo chanya kama vile tunavyotarajia.
Aidha, ni vyema sana wafugaji wakaanza kuboresha mabwawa yao kwa kuweka mfumo huu ambao utawasaidia kuongeza idadi ya samaki kwenye bwawa na kupunguza gharama za matumizi ya maji ya mara kwa mara.