Huu ni ugonjwa unaosababishwa na viluwiluwi vinavyojulikana kitaalamu kwa jina la Coenurusis Cerebralis unaoshambulia mfumo wa fahamu wa kati (ubongo na uti wa mgongo) wa mbuzi na kondoo.
Chanzo cha viluwiluwi
Viluwiluwi vya ugonjwa huu vinatokana na minyoo aina ya tiniamaltisepts iliyopo katika utumbo wa mbwa au wanyama pori jamii ya mbwa. Mbwa anapojisaidia, hutoa kinyesi chenye mayai ya viluwiluwi na kuacha kwenye nyasi.
Chanzo cha ugonjwa kwa mbuzi na kondoo
- Mbuzi na kondoo hupata ugonjwa wa Coenurosis pale wanapokula nyasi zenye kinyesi cha mbwa kilicho na mayai au viluwiluwi hivyo.
Dalili
- Mbuzi au kondoo hupata kizunguzungu
- Kudhoofika kutokana na kushindwa kula
- Kung’ata meno na kutiririsha mate
- Mbuzi au kondoo kutembea kwa mwendo usio wa kawaida
- buzi au kondoo wanaweza kupata upofu kwa kutokuona
Sampuli ya kupima kama ni ugonjwa wa Coenurosis
Ni vigumu kutambua kama mbuzi au kondoo wameathiriwa na ugonjwa huu kwa kuangalia baadhi ya daliali, ni vyema kuchukua sampuli (kichwa cha mnyama au uti wa mgongo) kwa ajili ya kupima.
Magonjwa yenye dalili zinazofanana na ugonjwa huu
Mbuzi na Kondoo wanaweza kupatwa na magonjwa mengine yenye dalili zinazofanana na za ugonjwa huu. Magonjwa hayo ni pamoja na;
- Kichaa cha mbwa (mbuzi au kondoo anapong’atwa na mbwa mwenye kichaa.
- Mbuzi au kondoo kuwa na jipu kwenye ubongo
- Listeriosis (ugonjwa unaosababishwa na ulaji wa chakula chenye bakteria aina ya Listeria Monocytogenes
- Kuwa na vijidudu kwenye ubongo viitwavyo Oestrus Ovis
Namna ya kudhibiti
- Mbwa wapewe chanjo na dawa za minyoo kila wakati ili kudhibiti uzalishaji wa wadudu hawa.
- Mbwa wote wanaozurura wadhibitiwe kwani mbwa hao mara nyingi hawapati dawa wala chanjo.
- Mbwa wasilishwe nyama ya mbuzi au kondoo aliyekufa kwa ugonjwa huu ili kuzuia mbwa hawa kuendelea kuzalisha viluwiluwi vya ugonjwa huu.
- Mfugaji ahakikishe hachungi wala kulisha mbuzi na kondoo nyasi zilizotoka kwenye eneo lenye kinyesi cha mbwa ili kulinda kutokula mayai au viluwiluwi vya ugonjwa wa Coenurosis.
Nini kifanyike ikitokea mbuzi au kondoo wamepata ugonjwa huu
Upasuaji ufanyike kwa kutumia wataalamu ambao watapasua ubongo au uti wa mgongo na kutoa viluwiluwi hivyo.
Muhimu
Wafugaji wahakikishe wanawapa mbwa dawa za minyoo inayoendana na aina ya minyoo (minyoo hii ni aina ya kamba) kila baada ya miezi mitatu. Dawa hizo ni Niclosamide au praziquantel.