- Mimea

Mchicha: Zao la muda mfupi lenye faida

Sambaza chapisho hili

Wakati wakulima wakijikita kwa kiasi kikubwa kwenye mazao mengi ya bustani kama vile nyanya, karoti,kabichi na mengine mengi, hawana budi pia kuweka mkazo katika zao la mchichi ambalo huvunwa kwa muda mfupi (wiki 3 – 5) na lenye pato kubwa katika masoko makubwa. 

Halikadhalika, mkulima hawezi kuwa na gharama kubwa kwenye kilimo cha mchicha hasa kwa kuwa ni zao la muda mfupi, hivyo suala la wadudu na magonjwa siyo tatizo kubwa.

Aina za mchicha 

Mchicha upo wa aina mbalimbali na huweza kutofautishwa kutokana na majani, umbo lake pamoja na rangi ya majani.

  • Aina ya kwanza ni zile zenye majani makubwa ya kijani na yenye kimo cha mita 2 hadi 2.5 na ambayo huzaa majani mengi na yenye ladha ya utamu.
  • Aina ya pili ni zile zenye majani ya ukubwa wa kati, kimo kifupi cha mita 1.5 na yenye kuzaa majani mengi sana.
  • Aina nyingine ya mchicha ni ile yenye miiba na mashina, yenye majani na maua ya rangi ya zambarau au nyekundu.

Kusia 

Mkulima anunue aina ya mbegu anayohitaji kupanda na kusia kulingana na aina ya mavuno anayopendelea kwa ajili ya soko.

Usiaji/upandaji wa kutawanya kwa uvunaji wa kung’oa 

Njia hii ya kusia mchicha ni rahisi na ya haraka sana. Mkulima atahitajika kuandaa shamba lake vizuri kwa kuchanganya udongo na samadi au mboji kiasi cha kilogramu 2 kwa mita moja ya mraba.

Kwa majira ya kiangazi wakati ambapo kuna uhaba wa maji, mkulima aandae matuta yaliyo chini ya ardhi (sunken) au bapa na matuta yaliyoinuka toka kwenye usawa wa ardhi kwa wakati wa mvua.

Mkulima achukue mbegu za mchicha na kuchanganya na mchanga kwa (mbegu ni ndogo sana) katika uwiano wa moja kwa tatu (1: mbegu na 3: mchanga) ili kurahisisha usiaji na uotaji ulio katika mpangilio mzuri.

Baada ya hapo, mbegu hiyo ifukiwe kwa tabaka la udongo kwa sentimeta 0.5 hadi 1.0 kisha kunyunyiziwa maji kiasi kidogo ili kuweka unyevu.

Palizi 

Miche inapoota, mkulima afanye palizi walau mara 1 kwa juma ili kuondoa ushindani wa magugu na mchicha pamoja na kuepuka mchanganyiko wa magugu wakati wa kuvuna.

Aidha, mimea ipunguzwe kwa umbali wa sentimeta 5 toka mmea na mmea ili kupata mimea bora, imara na yenye afya. Katika upandaji huu, mkulima huweza kuvuna mchicha baada ya wiki 3 toka kusia hadi 5 ikiwa ni kwa kutegemea aina ya mchicha uliosiwa.

Usiaji wa muda mrefu katika mistari kwa uvunaji wa kuchuma 

Mkulima achague mbegu anayohitaji kupanda na kuandaa vitalu kisha kuchanganya mbegu na mchanga na kusia kwa umbali wa sentimeta 20 hadi 30 kutoka mstari na mstari. Shamba liandaliwe kwa kulimwa vizuri na kuchanganywa udongo na samadi au mboji iliyoiva kwa uwiano wa kilogramu 2 hadi 5 kwa mita moja ya mraba.

Baada ya majuma 3, miche ing’olewe na kuhamishiwa kwenye shamba lililoandaliwa na kuoteshwa kwa nafasi ya sentimeta 10 hadi 15 kutoka mmea hadi mmea.

Palizi

Usafi wa shamba yaani palizi ifanyike kila wiki mara 1 ili kuondoa magugu yanayotafuta virutubisho kwa ushindani pamoja na mchicha. 

Uvunaji

Mchicha uvunwe baada ya wiki ya 5 hadi 7 toka kupandwa na kuendelea hadi miezi 4. Mimea ya zamani inaweza kukatwa karibu na usawa wa ardhi na kuchipua.

Wadudu na magonjwa 

Zao la mchicha haliathiriwi sana na magonjwa wala wadudu kama mazao mengine ya bustani. Wadudu kama vidukari na utitiri huweza kuathiri zao hili hasa zile zilizozeeka na kwa baadhi ya aina ya mchicha huweza kuathiriwa na virusi.

Masoko 

Uvunaji wa ung’oaji mmea mzima na uuzaji unafanyika kwenye masoko ya kawaida kwenye miji mikubwa na midogo. Aidha, bei ya uuzaji wa mafungu ya mchicha hapa Tanzania huwa ni shilingi 100 hadi 200 lakini bei huwa juu kwenye masoko makubwa.

Uzalishaji wa mbegu

Kwa uzalishaji wa mbegu za aina zote za mchicha, inashauriwa kupanda kwa nafasi ya sentimeta 60 toka mstari hadi mstari na sentimeta 25 tika mche na mche.

Mbegu zikishakoomaa huvunwa na kukaushwa kisha kupigapiga ili kutoa mbegu.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

6 maoni juu ya “Mchicha: Zao la muda mfupi lenye faida

    1. Habari,

      Karibu Mkulima Mbunifu na asante kwa kuendelea kufuatilia na kusoma makala mbalimbali za jarida hili.

      Karibu sana

  1. Je,mchicha huitaji dawa ipi nzuri na yenye kukuza kwa haraka kati ya kemikali na asili?na kikawaida mchicha huvunwa mara ngapi hadi kufa

    1. Habari,
      Dawa inayotakiwa ni dawa za asili pekee. Uvunaji wake hutegemea unavuna kwa namna gani na aina gani ya mchicha, kama ni uvunaji wa kung’oa ukishang’oa ndiyo imeisha kama ni wa kuchuma unaweza kuchuma mpaka mara tatu au nne kulingana na utunzaji wako.

  2. kwema humu mi nashida katika ushauri nina eneo dogo nafanya project ya kilimo ila tatizo ni maji ya magaidi mboga mboga zinakauka nikilimaa

    1. Habari, pole sana kwa changamoto hiyo
      Tafadhali wasiliana na mtaalamu Bi. Lucy mvungi kwa namba 0755 565 621 kwa ushauri zaidi wa nini kifanyike

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *