Ikiwa wewe siyo mfugaji wa ng’ombe na unahitaji kufanya hivyo ila unaogopa kulingana na habari toka kwa wafugaji wengine, hebu soma baadhi ya taarifa hizi huenda zikakushawishi kufanya mradi huu kwa furaha na kwa ufanisi zaidi.
- Unaweza kuanzisha mradi wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa ukiwa na eneo dogo. Unachotakiwa ni kuwa na sehemu inayotosheleza kuwafugia idadi ya ng’ombe ulionao.
- Aina nzuri ya ng’ombe ambae analishwa vizuri, anaweza kuzalisha kiasi cha 50 – 60 za maziwa kwa siku.
- Ng’ombe wa maziwa anaweza kula zaidi ya kilo 25 za sileji kila siku.
- Sileji hutengenezwa kwa ajili ya kuhifadhi malisho na kutumika wakati ambao ni vigumu kupata majani mabichi. Kamwe isitumike kama mbadala wa virutubisho kwa ajili ya mifugo.
- Usinunue ng’ombe kutoka kwenye sehemu yenye baridi kali, ukawapeleka sehemu yenye joto kali na ukategemea kuwa utapata kiasi sawa cha maziwa. Mfano, ng’ombe ambae anafugwa Arusha hawezi kupelekwa Dar Es Salaam akazalisha kiwango sawa cha maziwa na alipokuwa Arusha.
- Endapo umejenga banda zuri na kununua aina nzuri ya ng’ombe, lakini ukawa hauna malisho mazuri na ya kutosha, usitegemee kuwa na mafanikio mazuri.
- Ng’ombe ni kama binadamu; kwa kadri utakavyomuhudumia vizuri ndivyo nae atakavyokupatia faida zaidi. Wekeza kwenye kuwahudumia ng’ombe ili waongeze uzalishaji wa maziwa zaidi.
- Huhitaji kwenda chuoni au kuajiri mtaalamu wa mifugo ili kufuga, unachohitaji ni kuwa na hari ya kufuga, kutafuta taarifa sahihi juu ya ufugaji na kujifunza kutoka kwa wafugaji ambao wamepata mafanikio.
Maoni kupitia Facebook