- Mifugo

Ulishaji wa majani machanga ni hatari kwa afya ya mifugo

Sambaza chapisho hili

Mabadiliko ya hali ya hewa ni jambo muhimu sana katika maisha yetu ya kila siku, hata katika ufugaji mabadiliko haya ya hewa yanaweza kuleta athari katika mifugo yetu.

Ukame wa muda mrefu unasababisha kupungua au kuisha kwa malisho ya wanyama.

Majani machanga ni yapi

Majani machanga ni yale yanayo chipua baada tu ya mvua kunyesha. Majani haya ni hatari sana kwa afya ya mifugo hasa ikiwa mifugo ilikuwa inachungwa kwenye malisho makavu yenye kiwango kidogo cha protini kwa muda mrefu na ghafla kuchungwa kwenye majani machanga yenye kiwango kikubwa cha protini.

Ulishaji wa mifugo kwenye majani haya machanga unaweza kuleta madhara kwa haraka katika mfumo wa upumuaji wa wanyama na hatimaye kusababisha vifo.

Hivyo, ni lazima kuchukua tahadhari kwa kipindi hicho kuchunga mifugo katika majani machanga kwani mbuzi na ng’ombe huathirika zaidi.

Nini kinaleta madhara katika mfumo wa upumuaji

Wanyama wakichungwa kwenye majani makavu muda mrefu sehemu ya kwanza ya tumbo yaani utumbo mkubwa (rumen) linakuwa limezoe uchakataji wa chakula kikavu chenye protini kiasi kidogo.

Ghafla mnyama anapoanza kuchungwa kwenye malisho yenye majani machanga (lush green pasture) yenye kiwango kikubwa cha protini basi bakteria wa tumbo kubwa wanachakata majani machanga kwa haraka mno na kuzalisha amino acid tryptophan ambayo inazalisha kemikali ambayo ni sumu.

Sumu hii inasafirishwa kutoka tumboni kwenda kwenye mapafu kwa njia ya damu na inakwenda kuharibu seli za ndani ya mapafu.

Dalili kwa mnyama aliyeathirika

Dalili zinaonekana ndani ya siku 4 hadi 10 mara tu baada ya mnyama kubadilishiwa malisho kutoka majani makavu yenye kiwango kidogo cha protini na ghafla kuanza kulishwa majani machanga yenye protini kwa kiwango kikubwa.

Dalili hizi zinazoweza kuonekana ni kama hizi;

  • Mnyama kukosa nguvu ya kutembea, na kupumua wakati mdomo wake ukiwa wazi.
  • Mnyama kunyoosha kichwa na shingo juu ili kuweza kusaidia hewa ipite kwa urahisi.
  • Mnyama kupumua kwa haraka na kwa shida.
  • Mnyama kutoa mapovu mdomoni na puani.
  • Mnyama kudondoka chini na kufa.

Mnyama akishakufa na mzoga wake ukipasuliwa yafuatayo yanaweza kuonekana;

  • Mapafu kuonekana kjaa maji na mapovu.
  • Moyo wa mnyama utaonekana kuvilia damu.
  • Figo pamoja na bandama kuvilia damu pia.
  • Chakula kilichopo kwenye tumbo la kitabu kuwa kikavu.

Utajuaje kwamba mifugo yako imeathirika na tatizo hili

  • Utaona kundi kubwa la mbuzi au ng’ombe wakubwa watakuwa wamepata tatizo la kupumua kwa shida ndani ya wiki mbili baada ya kutoka kwenye ukame wa muda mrefu na kuanza kuwachunga kwenye majani machanga.
  • Asilimia 50 ya wanyama waliopo kwenye zizi kama wameugua basi kuna uwezekano wa asilimia 30 ya Wanyama kufa.

Utazuiaje Ugonjwa huu usitokee

Uzuiaji wa ugonjwa huu ni kufanya mabadiliko kutoka kuchunga mifugo kwenye majani makavu kwenda kwenye majani machanga.

Njia hizi zinaweza kutumika;

  • Wanyama wachungwe kwenye maeneo yenye majani yaliyokomaa kwa siku 10 za mwanzo baada ya majani machanga kuchipua mpaka hapo yatakapokomaa.
  • Wanyama wanaweza kuchungwa kwa masaa machache yaani 2 hadi 3 kwa siku na kwa wiki mbili za mwanzo mara baada ya majani machanga kuchipua.

Tiba

  • Kwa wanyama walioathirika sana huwa hawaponi kwa matibabu yoyote na wanakufa ndani ya siku moja au mbili mara baada ya kuugua.
  • Wanyama walioathirika kidogo wanaweza kupatiwa matibabu ambayo yatapunguza makali ya dalili za ugonjwa.

Muhimu

Hakikisha unakuwa makini sana kipindi chote cha mabadiliko ya hali ya hewa na ufugaji kwa ujumla.

Kwa maelezo Zaidi wasiliana na Afisa mifugo Bi. Adelina Mkumbukwa kwa simu namba 0755 719338 au barua pepe adelinamkuu@yahoo.com

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *