Mabaki ya mazao ndicho chakula halisi kinachotumika kwa malisho wakati wa kiangazi katika nchi za ukanda wa tropiki, ila ubora wake ni mdogo sana.
Ng’ombe wa maziwa huwa wanateseka kwa kutopatiwa chakula cha kutosha, na matokeo yake ni kuzalisha kiwango kidogo cha maziwa, uwezo mdogo wa kuzaliana, kuwa na uzito mdogo, ndama kufa au kuwa na umbo dogo na dhaifu, pamoja na kukuwa kwa shida.
Hali hii pia husababisha kipato kidogo kwa mfugaji na familia. Kutokuwa na chakula cha uhakika ni matokeo bayana ya malisho hafifu.
Matayarisho ya nyasi kavu
Majani yaliyokauka na aina nyingine ya malisho ni njia rahisi na nzuri ya kuhifadhi malisho.
Mahitaji: Safisha majani na yaache siku tatu kukiwa hakuna mvua kisha yahifadhi kwa ajili ya kulishia baadaye. Ukoka, ngano mwitu, majani ya tembo, mimea jamii ya mikunde na lablab inatengeneza malisho mazuri ya kiangazi yaani “hay”.
Malisho makavu yanaweza pia kuuzwa ili kuongeza kipato kwa mfugaji.
Namna ya kuandaa
- Kata majani mara tu yanapoanza kuchanua au kati ya wiki 4-6 toka ulipokata au kulisha mara ya mwisho.
- Ni vyema kukata nyakati za asubuhi siku unapohitaji kunyausha majani.
- Acha shina urefu wa sentimita 5 (inchi 2)
- Tandaza majani katika eneo unalotaka kukaushia majani yako na liwe eneo sahihi kwa kazi hiyo.
- Tumia reki kugeuza majani walau mara moja kwa siku kuepuka kuoza.
- Acha yakauke kwa siku mbili au tatu bila kunyeshewa.
- Majani yakishakauka yakusanye na hifadhi vizuri katika kivuli sehemu ambayo hayapati jua wala mvua.
- Hifadhi katika rundo au funga robota.
- Unaweza kutengeneza malisho ya kiangazi uliyoandaa kutokana na mchanganyiko wa nyasi na jamii ya mikunde yenye protini kama vile lucerner ili kuongeza ubora.
Kutengeneza robota
Njia rahisi ya kutengeneza robota ni kuwa na boksi la pembe nne lililo wazi upande wa juu na wa chini, ukubwa wa 3ft x 2ft na urefu 1.5 ft.
Weka majani yaliyokauka ndani yake na ukanyage juu yake (miguu iwe safi) mpaka itakapokuwa haliwezi kushindiliwa zaidi. Baada ya hapo funga majani yako na usukume kutoka ndani ya boksi.
Miti ya Malisho
Malisho yanayotokana na mimea jamii ya mikunde ina protini ya kutosha, inayoboresha uzalishaji wa maziwa.
Kwa kuwa ukuaji unapungua sana wakati wa kiangazi, majani yanakuwa hayana virutubisho vingi kama nyakati za mvua hasa yanapokuwa machanga.
MUHIMU: Kuwa makini usiwalishe ng’ombe majani mabichi zaidi ya kilo 12 kwa siku, au kilo 2 kwa mbuzi au kondoo, kwa kuwa majani mabichi yanakuwa na viini vinavyoingiliana na mmeng’enyo wa chakula. Mara zote changanya na majani makavu au majani vunde.
Ulishaji wa majani makavu: Usisahau maji
Kiwango cha majani makavu kiwe kidogo zaidi ya majani mabichi. Robota moja la kilo 15 la majani makavu ni sawa na kilo 75 za majani mabichi, na yanaweza kulishwa kwa ng’ombe anaetoa maziwa vizuri mara moja kwa siku.
Ikumbukwe pia kuwa usagaji wa chakula kikavu tumboni unahitaji kiwango kikubwa sana cha maji, vinginevyo itaathiri utoaji wa maziwa kutokana na kukosa maji ya kutosha.
Ukaushaji wa majani
Majani jamii ya mikunde yaliyokaushwa ni malisho mazuri wakati wa kiangazi yenye virutubisho vya protini. Kata majani wakati yakiwa yanapatikana kwa wingi hasa kipindi cha mvua. Yaanike katika eneo safi kwa siku tatu sawa na ulivyokausha malisho ya kiangazi. Majani hayo yanapokauka vizuri yanaweza kuhifadhiwa katika mifuko. Wape ng’ombe kati ya kilo 3-4 kwa siku na ½ kilo kwa mbuzi au kondoo.
Hesabu mifugo wadogo kama nusu ya mfugo mkubwa wa wastani.
Usisahau mifugo wadogo unapofanya hesabu ya kiasi cha malisho unachohitaji kuhifadhi kwa ajili ya kiangazi.
Mifugo wadogo pia wanahitaji virutubisho vya kutosha ili kuendeleza afya zao.
Malisho yanayolimwa
Nyasi ni chakula kikuu kwa wanyama wanaocheua. Ubora wa malisho unategemea yamevunwa yakiwa na umri gani. Malisho yanakuwa bora zaidi endapo yatavunwa yakiwa katika hatua za mwanzo za ukuaji kabla ya kuchanua, wakati ambao protini na virutubisho vingine vinakuwepo kwa wingi. Kuweka mbolea pia huongeza ubora wa malisho.
Matete
Matete ni aina moja wapo ya malisho yanayokatwa kwa ajili ya malisho, hasa kwa mifugo ya ndani. Matete yanapotunzwa vizuri na kukatwa mara kwa mara, yanakuwa na virutubisho vizuri kwa ng’ombe wa maziwa, na husaidia sana kunapokuwa na uhaba wa malisho hasa wakati wa kiangazi.
Malisho Mseto
Inashauriwa kupanda viazi vitamu au aina nyingine ya mimea jamii ya mikunde yenye virutubisho kwa wingi kama vile Desmodium au lusina. Panda katika mashimo au mistari ya matete ili kuongeza virutubisho na ubora wa malisho, pamoja na kusaidia kuzuia magugu.