Tarehe 2 na 3 Septemba 2026, Dar es Salaam itakuwa kitovu cha kilimo cha Afrika.
Kila mwaka, wakulima, wafanyabiashara, wawekezaji, na wataalamu wa kilimo kutoka nchi mbalimbali wanakutana katika mkutano mmoja mkubwa kuzungumza biashara, kujifunza, na kuunda ushirikiano. Mwaka huu, mkutano huo unafika nyumbani kwetu, hapa Tanzania.
Tarehe 2 na 3 Septemba 2026, Dar es Salaam itaandaa toleo la 10 la Africa Agri Expo (AAE 2026), ukifanyika pamoja na Expo ya 3 ya Future Food, Livestock and Poultry (FLIP 2026). Ni mara ya kwanza kwa tukio hili kubwa kufanyika Tanzania, na ni fursa ya kipekee kwa wakulima na wadau wa kilimo wa Tanzania kushiriki moja kwa moja na dunia nzima.

Sasa Ndio Wakati wa Afrika
Afrika inamiliki zaidi ya asilimia 60 ya ardhi yenye rutuba duniani ambayo bado haijatumika kwa uzalishaji wenye tija. Idadi ya watu barani Afrika inakadiriwa kuongezeka maradufu ifikapo mwaka 2050, na soko lake la chakula ni mojawapo ya yanayokua kwa kasi zaidi duniani. Mahitaji ya chakula yanazidi, na fursa za biashara zinazidi kuwa kubwa. Kwa kweli, Afrika si soko la kesho, ni soko la leo na linafaa kuwafaidi Wakulima wadogo.
Tanzania, hasa, inajitokeza kama nguzo ya kilimo Afrika Mashariki. Ardhi yake yenye rutuba, bandari yake ya kimkakati, na serikali inayowekeza kikamilifu katika miundombinu ya kilimo vinafanya Dar es Salaam kuwa lango bora kwa biashara zinazotaka kuingia au kupanua masoko yao Afrika Mashariki na Kati. Kwa mujibu wa Tahir Abdul Bari, Mkurugenzi Mtendaji wa TAB Group, ‘Afrika si soko la kesho, ni soko la leo. Biashara zinazojenga mahusiano hapa sasa ndizo zitakazoongoza biashara ya chakula duniani katika miaka kumi ijayo.”
Tutarajie nini?
Kwa siku mbili, wageni watakuwa na nafasi ya kuona pembejeo mpya za kilimo, teknolojia za kisasa za kulimia, vifaa vya usindikaji na uhifadhi wa mazao, na suluhisho za changamoto zinazowapata mifugo na kuku, yote haya mahali pamoja. Pia, kutakuwa na vikao vya majadiliano kuhusu masuala yanayoathiri kilimo cha Afrika, yakiwa pamoja na mabadiliko ya tabianchi, masoko, fedha za kuwekeza kilimo, na jinsi vijana wanavyoweza kushiriki katika kuijenga sekta hii.
Washiriki wanatarajiwa kutoka nchi zaidi ya 35, wakiwemo watengenezaji wa pembejeo, wasambazaji, watunga sera, na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa. Kwa mkulima wa Tanzania, hii ni fursa adimu ya kuwafikia watarajiwa hao bila kusafiri mbali.
Kufanya maonesho ama kudhamini
Kama wewe ni mfanyabiashara anayetaka kuonyesha bidhaa zako, mdhamini anayetaka kuongoza mazungumzo, mzungumzaji mwenye ujuzi wa kushiriki, au mgeni anayetaka kujifunza na kuunda mitandao, nafasi yako ipo. Wasiliana na waandalizi kwa anuani: agri.expo@tab-global.com
MkM itakuwepo
Mkulima Mbunifu utashiriki katika AAE 2026. Tutakuwa na kibanda kitakachoonesha jinsi MkM inavyofanya kazi — jarida, moduli za mafunzo, na wakulima mabalozi – na jinsi maarifa ya kilimo endelevu yanavyofika kwa mkulima wa kawaida shambani. Karibu , ututembele na ujifunze!
Kumbuka
- Tarehe: 2–3 Septemba 2026
- Mahali: Dar es Salaam, Tanzania
- Maelezo zaidi: africa-agriexpo.com
- Barua pepe: agri.expo@tab-global. com




