Mahindi ni zao muhimu la chakula, na ni aina ya nafaka inayotumiwa kwa wingi kama chakula, hususani katika mataifa ya Afrika, lakini pia limekuwa likitumika katika nchi zilizopo kusini mwa jangwa la sahara.
Mahindi ni chakula cha matumizi ya nyumbani kwa idadi ya watu inayokadiriwa kuwa asilimia 50. Ni chanzo muhimu cha madini cha kuongeza nguvu mwilini, protini, madini ya chuma (iron) vitamini na madini mengine asilia.
Waafrika hutumia mahindi kwa milo kama vile kupika uji, makande, kuchemsha mabichi, kuchoma, ugali, pombe n.k.
Kila sehemu ya mmea wa mhindi una thamani kiuchumi: punje, majani, shina na magunzi huweza kutoa kiasi kikubwa cha bidhaa nyinginezo zilizo chakula na zisizokuwa chakula.
Vile vile mahindi ni chakula muhimu cha mifugo na huhifadhiwa kama silage.
Pia mabaki ya mimea na nafaka hutumika viwandani kutengeneza wanga na mafuta.
Mahindi ni mimea ambayo hustahimili mabadiliko ya hali ya hewa tofauti na huweza kumea katika maeneo mengi tofauti hapa nnchini. Kuna aina nyingi za mahindi yanayotofautiana katika muda wa kukomaa, mavuno na ustahimilivu wa hali ya hewa.
Ili kuwa na mazao mazuri baada ya kuotesha, ni lazima kufanyika kwa palizi kwa wakati sahihi na kwa usahihi pamoja na kudhibiti magonjwa na wadudu.
Udhibiti wa magugu/palizi
- Uthibiti wa magugu katika kilimo cha mahindi ni muhimu ili kupunguza kushindania maji, virutubisho na mwanga baina ya mahindi na magugu.
- Ni muhimu shamba la mahindi liwe safi bila magugu siku 40 za mwanzo baada ya mimea ya mahindi kuota.
- Matokeo ya utafiti yameonyesha kuwa kwa kawaida palizi 2 za mkono zinatosha katika maeneo ya chini, kati na nyanda za juu.
Hata hivyo mapendekezo ya muda, kati ya palizi ya kwanza na ya pili inatofautiana miongoni mwa maeneo.
Magonjwa ya mahindi na udhibiti wake
- a) Magonjwa ya majani
- Kuna magonjwa makuu matano ya majani yanayoshambulia mahindi Tanzania yanayoweza kupunguza mavuno kwa kiasi kikubwa.
- Magonjwa hayo matano ni aina mbili za kutu ya majani (rust), mbili za bakajani (Leaf blight and GLS) na ugonjwa wa milia (Viral diseases).
- Kati ya hayo hakuna hata moja linaloweza kudhibitiwa kwa madawa na faida ikapatikana.
- Njia pekee ni kupanda aina za mahindi ambazo zinavumilia au ni kinzani kwa magonjwa hayo.
Kutu ya majani
- Aina ya kwanza ya kutu ya majani ni kutu ya kawaida (Common rust) inayosababishwa na Puccinia sorghi.
Ni ugonjwa unaonekana maeneo yenye ubaridi wa nyanda za juu Tanzania, vivimbe vidogo vidogo hutokea pande zote za majani, huwa vya kahawia mwanzoni na baadaye hubadilika kuwa vyeusi vinapofunguka.
- Aina ya pili ya kutu ya majani, ni ile ya nyanda za chini inayosababishwa na Puccinia polysora. Inaonekana sana maeneo ya nyanda za chini Tanzania zenye unyevunyevu.
Vivimbe vidogo vya manjano hutokea pande zote za majani, kadri vinavyokomaa hubadilika na kuwa rangi ya kahawia nyeusi.
Bakajani
- Ugonjwa huu husababisha jani kuweka rangi ya kahawia.
- Hakuna viiniyoga (Spores) vinavyoonekana katika uso wa majani. Aina ya kwanza ya bakajani inasababishwa na Helminthosporium turcicum.
- Inaonekana zaidi maeneo ya juu ya Tanzania yenye ubaridi, makovu au madoamadoa hutokea kwanza katika majani ya chini yaliyokomaa.
- Kwa kadri mmea unavyokuwa makovu hayo hukua na yanakuwa mengi, madoa hayo ni marefu na yanapinda mwishoni. Makovu haya hatimaye huua jani lote.
Ugonjwa wa milia
- Ugonjwa huu husababishwa na virusi. Panzi mdogo wa kijani aitwae Cicadulina Spp. ndiye anayesambaza virusi kutoka mmea mmoja kwenda mwingine.
- Ugonjwa unatambulika kwa mistari ya weupe yenye njano kwenye majani, kadri mmea unavyokua majani mapya huonesha zaidi na zaidi ugonjwa huu.
- Kama ugonjwa ukitokea mapema katika maisha ya mmea, mmea hudumaa na hautatoa mhindi wa kawaida. Ugonjwa wa milia unaonekana sana mikoa ya Morogoro, Arusha, Mwanza, Shinyanga na Kagera na wilaya za Rungwe na Sumbawanga.
- Matumizi ya madawa kudhibiti mdudu anayesambaza ugonjwa huu hayana tija.
- b) Magonjwa ya mhindi (gunzi)
- Magonjwa matatu yanayojulikana sana ya mhindi (gunzi) ni Gibberella Spp, Fusanium Spp na Diplodia Spp. Magonjwa haya yanashambulia mbegu na gunzi.
- Yaweza kutokea wakati mhindi unakua, lakini mara nyingi hutokea wakati wa kukomaa.
- Ndege, wadudu na wanyama huharibu maganda ya mahindi na ugonjwa huingia kwenye mhindi kama mashambulizi ya pili, na kusababisha ugonjwa.
- Iwapo mahindi yataanguka magonjwa hutoka kwenye udongo. Magonjwa ya magunzi (mahindi) yanatokea kwa wingi katika maeneo yenye mvua nyingi,
- Mahindi yote yenye ugonjwa na maganda yaangaliwe kwa kuchomwa au kufukiwa kina kirefu, ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa kwa msimu unaofuata.
Wadudu waharibifu wa shambani na udhibiti wake
Kwa uzalishaji mzuri wa mahindi ni muhimu kuwatambua wadudu waharibifu madhara yanayosababishwa na jinsi ya kuwadhibiti Bungua (Stalk borer).
Uharibifu ufanywao na bungua wa mahindi si rahisi kuwaona mwanzoni na wakati uharibifu mkubwa utakapokuwa umeonekana mimea mingi tayari huwa imekufa na mingine kuharibiwa kwa kiwango cha kutoweza kuinusuru.
Aina tatu kuu za bungua wa shina Tanzania ni i) Chilo patellus, ii) Busseola fusca na iii) Sesania calamistis.
Chilo Partellus
- Bungua wa shina mwenye madoadoa, anapatikana Tanzania sehemu za joto za ukanda wa chini, Chilo huanza kushambulia mara tu majani yanapoanza kutokea
- Nondo mdogo wa kahawia anataga mayai kwenye uso wa jani na kiwavi anakwenda ndani ya jani lililo mviringo katikati ya mahindi na kila jani jipya.
- Matundu madogo madogo hutobolewa kwenye jani na kawaida huwa hayaonekani matundu huwa yamezagaa kwenye jani, hakuna mpangilio wapi yatatokea kwa kawaida tundu moja linamaanisha kuwa kiwavi mmoja.
- Matundu huonekana kama vile yametobolewa kwa pini ndogo kupitiliza kwenye jani.
Bussoela fusca
- Uharibifu wa Busseola ni rahisi kuonekana. Nondo hutaga mayai nje ya jani kwenye shina na kiwavi anatoboa majani yaliyo pamoja na kuingia ndani ya shina.
- Hili likitokea matundu mengi huonekana katika mstari wakati jani likichomoza
Sescania Calamistis
- Bungua wa tatu ni s-calamistis au bungua wa rangi ya pinki kama ilivyo kwa chilo na uharibifu wa mwanzo wa mdudu huyu haudhibitiki kirahisi. Madhara yanayosababishwa ni kama ya Chilo na Busseola kuingia katikati ya shina na kuharibu sehemu inayokua.
- Aina zote tatu za bungua huuwa sehemu inayokuwa ya mahindi ukiwa mchanga na mashambulizi ya baadaye hudhoofisha shina na kufanya kuanguka baadaye katika msimu.
MUHIMU:
Ni muhimu kwa mkulima kuhakikisha anafanya usafi wa shamba kuondoa magugu na masalia yatakayopelekea wadudu na magonjwa kupata njia ya kuzaliana na kuambukizana kwani vyanzo vingi vya magonjwa na wadudu ni mazingira rafiki.
Makala hii imenakiliwa kutoka katika kitabu cha mwongozo wa kilimo cha mahindi kilichoandikwa na Zabron M. Msengi & Kheri M. Kitenge.