Sera ya soko huria iliyoanza kutekelezwa toka miaka ya 1990 imefungua fursa kwa wawekezaji kuwekeza kwa wingi kwenye maeneo mbali mbali ya kibiashara.
Kwa muda mrefu, Kilimo kimewavuta wawekezaji ambao wamekuwa wakijishughulisha na mashamba makubwa ili kukidhi madhumuni ya biashara ya kuzalisha kwa wingi kupunguza gharama ya kuzalisha kwa kiasi kidogo. Pamoja na kutekelezwa kwa makubaliano baina ya wawekezaji na kijiji wanakofanya shughuli za kilimo, kumekuwa na manunguniko mengi kuhusu wawekezaji kuchukua maeneo makubwa na ardhi ikianza kupungua kutokana na kuongezeka kwa watu na wahamiaji hasa wafugaji.
Ili kupunguza manunguniko ya wakulima inabidi wakulima watayarishwe, ili waweze kuzungumza lugha ya biashara ambayo inalingana na ya wawekezaji.
Ni muhimu wakulima wakaelimishwa na kufahamu kwa undani kuhusu kilimo biashara. Hii itawasaidia wakulima kutimiza nia ya kufanya kilimo biashara na kupata kipato kikubwa. Ili kufikia lengo hilo inabidi wakulima wafanye mambo yafuatayo;
- Walime kwa kiasi cha kutosha.
- Wasindike wenyewe na kufungasha.
- Watafute soko na kuuza bidhaa zilizoongezwa thamani badala ya kuuza mali ghafi.
Mkulima anayeuza bidhaa zilizoongezewa thamani anakuwa na fursa ya kushiriki kupanga bei badala ya kupangiwa bei kitendo ambacho kinampa fursa ya kupata faida kubwa. Wawekezaji wanahamasishwa kuchukua mali ghafi kwa wakulima na kusindika kwa niaba ya wakulima na kuwaunganisha na masoko ya bidhaa wakitumia teknolojia za kisasa ambazo mkulima mdogo hawezi kuzipata kutokana na kuwa na mtaji midogo.
Kuna faida wakulima wadogo kujiunga na wawekezaji wanaofanya shughuli za kilimo kwa kiwango kikubwa. Moja wapo ya faida hizo ni pamoja na mkulima mdogo kuunganishwa na soko ambalo humpatia mkulima midogo faida.
Halikadhalika humuwezesha mkulima mdogo kuongeza uwezo wa kupanua shamba, kupata kipato kikubwa na kupunguza manunguniko. Mkulima ambaye anauza mazao yaliyoongezwa thamani anaweza kupanua kilimo chake na kuongeza idadi ya mazao ambayo anaweza kulima, kusindika na kuongezea thamani.
Vipi kuhusu wafugaji?
Wafugaji wanaweza kutumia eneo dogo la ardhi ikiwa wanafuga ndani badala ya kuchunga na kuwa na mkakati wa kutenga maeneo ambayo yataoteshwa malisho kwa ajili ya mifugo.
Kwa kufanya hivyo pia itapunguza migogoro ambayo inatokea kati ya wakulima na wafugaji kwa baadhi ya maeneo kwa sababu ya wafugaji kupenda kuchunga badala ya kufuga ndani.
Kwa kufanya ufugaji wa ndani, itawawezesha pia wafugaji kuuza mifugo iliyoongezwa thamani, kwa mfano kunenepesha mifugo na kuongeza tija ya kupunguza kiasi cha mifugo badala ya kuwa na mifugo mingi isiyokuwa na tija. Mfugaji anaweza kuwa na mifugo michache yenye faida.
Umuhimu wa maji katika mnyororo wa thamani
Kama wasemavyo maji ni uhai sio kwa binadamu peke yake, hata kwa wanyama na mimea pia. Kwa mkulima kutegemea mvua hawezi kuwa na kilimo cha kibiashara kwa kuwa hana uhakika mvua itanyesha lini, na kwa kiasi gani, ili atayarishe shamba kwa wakati na vile vile kuweka mbegu aridhini. Kutokuwa na uhakika wa mvua itanyesha lini mkulima hawezi kujua lini ajipange na palizi na vile vile kuwa na uhakika wa mvua ya kukuzia mazao. Mkulima hatakuwa na uhakikika kuwa mvua itakatika lini ili mazao yake yaliyo shambani yakauke tayari kwa kuvunwa. Ndio sababu mkulima anayetegemea maji ya mvua ni vigumu kuwa na kilimo cha kibiashara kwani hawezi kujua atavuna kiasi gani ili kumhakikishia mnunuaji upatikanaji wa mazao.
Katika hali hii uwezekano wa kutumia mbegu bora, mbolea sahihi unakuwa wa mashaka kwani mkulima hana uhakika na uzalishaji katika aina ya kilimo anachofanya. Kilimo cha umwagiliaji kinachotokana na maji yaliyovunwa au yaliyojengewa kutoka kwenye vyanzo vya maji au kwa kutumia maji yaliyo chini ya ardhi ni muhimu katika kufanikisha kilimo cha kibiashara.
Tanzania imejaliwa kuwa na vyanzo vya maji vya kutosha kinachotakiwa ni mipango mizuri ya uvunaji na matumizi ya maji hayo.
Licha ya kuwa bado hatujafanya bidii kubwa kujenga utaratibu wa kuvuna maji na kuyatumia kwa njia sahihi bado tunatumia asilimia 21% pekee ya miundo mbinu ya umwagiliaji iliyopo. Mbinu za kilimo biashara kwenye mnyororo wa ongezeko la thamani itafanya gharama za maji ziwe miongoni mwa gharama ambazo lazima zibebwe na mlaji na zitajumuishwa kwenye gharama ya kuuza bidhaa.
Ili kuwa na matumizi mazuri ya maji ni lazima jamii iwe na mpango wa usimamizi, wa kutunza vyanzo vya maji matunzo ya miundo mbinu na ugawaji wa maji usiokuwa na upendeleo. Lazima maji yawe na gharama na kila mtumiaji maji awe anatambua kuwa kila atakapotumia maji kwa kasi fulani itabidi alipe.
Changamoto katika mnyororo wa thamani
Tumeshuhudia namna ambavyo mabadiliko ya hali ya hewa yalivyopelekea hasara katika kilimo na ufugaji. Ili kuhakikisha upatikanaji wa maji ya kutosha kwa ajili ya umwagiliaji iko haja ya kuwa na mabwawa ambayo yatahakikisha upatikani wa maji kwenye msimu wa kilimo.
Hii ina maana vyombo vya fedha vikishirikiana na sekta binafsi kuna uwezekano wa kuvuna maji ya mvua ambayo yanaweza kuuzwa kama bidhaa nyingine. Wakulima hawatakuwa na matatizo ya kununua maji kwa ajili ya kilimo ali mradi gharama za maji zinaweza kubebeka kwenye bei ya bidhaa kwenye soko.
Faida ya kuuza bidhaa zilizoongezwa thamani, ni kubwa na gharama zote zile kutoka kuzalisha, kusindika na kuuza zinaweza kubebwa na bei ya mazao.
Katika mkakati wa kuvuna maji ya mvua na kuuza kuna haja ya sekta binafsi kufanya utafiti na kuandika mpango biashara utakaoonesha
kiuhalisia gharama zote za kujenga miundo mbinu, mkakati wa kuuza bidhaa ya maji, ukusanyaji wa mapato na vihatarishi vya aina yoyote ambavyo vinaweza kuwa ni kikwazo kwa biashara kufanikiwa.
Ili kukabiliana na hali ya hewa isiyotabirika kuna ulazima wa kuangalia uwezekano wa kujenga visima virefu ambavyo vinatoa maji kwenye mito mikubwa, ambayo iko chini ya ardhi ambavyo inaaminika kuwa si rahisi kukauka. Mikakati ni pamoja na kujenga mitaro ya kuhamisha maji yaliyozidi kwenye mashamba.
Kuwa na bima ni kati ya mikakati ingawa bima ni suluhu ya mwisho kwani madhumuni ya biashara ya kilimo ni kuzalisha, kusindika na kuuza. Kutokuwa na mazao ya kutosha hata kama bima inaweza kutumika kupunguza madhara ya hasara bado ni tatizo ikiwa hali ya hewa itazuia upatikanaji wa mazao. Mkakati mahususi wa kukabiliana na upatikanaji wa uhakika wa maji utachangia kwa kiwango kikubwa sera ya kilimo chenye tija.
Kwa maelezo zaidi juu ya mnyororo wa ongezeko la thamani, unaweza kuwasiliana na Herment A. Mrema kutoka Africa Rural Development Support Initiative (ARUDESI) kwa simu +255 752 110 290, +255 687 003 367, Barua pepe: machomingi@yahoo.com