Malengo ya kilimo ni kuzalisha chakula na bidhaa zingine ili kutosheleza mahitaji ya kaya, jamii na nchi kwa ujumla. Kufuatana na hilo, ni vyema kuhakikisha kwamba wakulima wanazalisha chakula chenye virutubisho, safi na salama kwa walaji na wote wanaotumia bidhaa zinazotokana na kilimo. Kilimo pia huchangia ajira na ustawi wa kichumi katika ngazi mbali mbali. Hivyo, tunapopanua kilimo, tunachangia malengo ya maendeleo ya nchi, kanda na bara letu la Afrika ambalo linaendelea kukua.
Kuna mifumo mbali mbali ya uzalishaji inayotumiwa na wakulima, na kila mfumo una faida na changamoto. Jarida hili linasisitiza matumizi ya mbinu za kiikolojia ambazo zinaambatana na utunzi wa mazingira, na huchangia kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayotishia msingi wa maliasili katika sehemu kubwa ya ulimwengu hasa nchi zinazoendelea. Tunapotunza mazingira tunahakikisha uendelevu, yaani tunaendelea kuzalisha kwa viwango vya juu sana na kwa vizazi vya baadaye.
Kilimo ikolojia ni kilimo endelevu kinachofanya kazi kupitia mahusiano kati ya mimea, wanyama, watu na mazingira yao na michakato inayofanyika katika mahusiano hayo. Wakulima wanatumia rasilimali asili ili kufanya uzalishaji. Hivyo, kilimo ikolojia mara nyingi ni kilimo kinachotumia kiasi kidogo cha pembejeo za nje ama kemikali zinazonunuliwa madukani.
Kilimo ikolojia inalenga kudumisha na kubadilisha mahusiano ya kijamii, kuwawezesha wakulima, kuongeza uzalishaji na kupendelea minyororo mifupi ya thamani. Inaruhusu wakulima kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, matumizi endelevu na kuhifadhi maliasili na bayoanuwai. Yaani, wakulima wanazalisha mazao ya chakula na ya thamani ya juu ili kukidhi mahitaji ya lishe, kupata hela kutokana na mauzo, na wanafanya hivi wakilinda mazingira.
Wakulima wengi wanaendelea kukumbatia kilimo hai na kuchuma faida zinazotokana na mbinu hii ya kilimo. Kupitia kwa masimulizi yao, tunajifunza na kuona vile hata sisi tunaweza kuboresha uzalishaji, michakato mbalimbali katika kilimo na namna tunaweza kuongeza mapato yanayotokana na kilimo.
Kama kawaida, tunaendelea kuwashauri wakulima kufanya majaribio katika eneo dogo, kuona matokeo kabla ya kuongeza eneo la uzalishaji.
Pia, ni muhimu kuelewa soko kabla ya kuzalisha, hii ikiwa ni pamoja na kujua ni mazao gani yanayotumika na kuhitajika na watu wengi au ni zao gani linaloweza kupata soko ili usizalishe kisha ukashindwa kuuza. Hii itakuletea hasara badala ya faida ambayo kila mkulima anatafuta.
Hata hivyo, kuongeza uelewa na uzoefu, tembelea na kushirikishana na wakulima wengine hasa wale wanaozalisha kwa kiwango cha juu ili uweze kujifunza na kupanua uzalishaji wako. Makundi ya wakulima yanachangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza elimu na kubadilishana mawazo kwa wakulima wenye nia ya kuongeza uzalishaji na mapato yao.
Ni jukumu lako wewe mkulima kuboresha zaidi idadi na hali ya biashara yako ya kilimo. Haijalishi kiasi cha shamba lako, liwe dogo au kubwa, unaweza kufanya kilimo hai. Ni mfumo unaoweza kutumiwa na kila mkulima.
Hivyo, kaa chonjo na uwe mbunifu kila wakati. Karibu na tuhamasike pamoja.