Mbegu
Kwa matokeo mazuri ikiwemo ukuaji mzuri wa mbogamboga na mavuno mengi mkulima anashauriwa kutumia mbegu bora zilizothibitishwa. Mbegu hizo huwa na sifa zifuatazao:
- Hutoa mavuno mengi ya kiwango bora.
- Zina uwezo mkubwa wa kuota.
- Huhimili baadhi ya wadudu na magonjwa.
- Hukua kwa haraka, kwa usawa na ni imara.
Ikolojia ya Eneo
Eneo linalofaa kwa uzalishaji wa mbogamboga za majani lisiwe kwenye mwinuko mkali kwa sababu kuna uwezekano mkubwa wa kutokea mmomonyoko wa udongo na kuondoa rutuba na hivyo kusababisha mavuno hafifu.
Endapo sehemu itakuwa na mwinuko, mkulima anashauriwa kutengeneza makinga maji ili kuzuia mmomonyoko. Vilevile lisiwe mahali penye kivuli kikubwa kwani itasababisha mbogamboga kutokupata mwanga wa jua wa kutosha na kushindwa kutengeneza chakula hivyo kuwa dhaifu.
Udongo
Mbogamboga za majani hustawi kwenye udongo wenye rutuba na wenye uwezo wa kupitisha maji kwa urahisi.
Utafiti wa udongo
Kabla ya kuanza uzalishaji ni vema mkulima afanye utafiti wa hali ya udongo wa eneo analotaka kuzalisha mbogamboga. Kupima udongo itamsaidia mkulima kujua afya ya udongo kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na virutubishi vilivyopo ndani ya udongo, hali ya uchachu (ph) ya udongo kwa sababu upungufu au wingi wa uchachu huathiri ukuaji wa mmea, na mazao yatakayofanya vyema kwenye shamba.
Maji
Mbogamboga za majani huhitaji maji ya kutosha ili kuwezesha mmea kufyonza virutubishi kutoka kwenye udongo na kuvisafirisha kwenda sehemu mbalimbali za mmea. Chanzo cha maji kinapaswa kuwa cha uhakika na cha kudumu endapo uzalishaji utakuwa endelevu. Maji yanayofaa kwa uzalishaji wa mbogamboga ni yale yasiyo na vichafuzi vinavyoweza kuleta athari kwa afya ya binadamu. Vichafuzi hivi ni kama uwepo wa metali, mabaki ya viuatilifu, na maji yenye vimelea vyenye maambukizi ya magonjwa. Zaidi, maji yasiwe na chumvi nyingi kwani huathiri ukuaji wa mimea.