- Kilimo, Mifugo

Masomo kupitia jarida ni suluhisho la changamoto za wakulima

Sambaza chapisho hili

“Mimi ni mkulima na mfugaji, Ninazalisha kwa misingi ya kilimo ikolojia. Situmii pembejeo sumu za viwandani kuanzia ninapootesha zao husika au kuanza uzalishaji wa mifugo yangu mpaka ninapovuna, kuhifadhi na kuuza mazao yangu.

Ninafanya uzalishaji wa mazao ya aina mbalimbali kama vile ndizi, kahawa, njugu, maharage, mahindi, mbogamboga, na pia ninafanya ufugaji wa kuku pamoja na mbuzi.’’

Hayo ni maneo ya Bw. Deogratius Joseph (66) toka Kyaka, wilaya ya Misenyi mkoani Kagera, miongoni mwa wanufaika wa jarida la Mkulima Mbunifu kupitia FADECO radio.

Bw. Joseph anaeleza kuwa, tangu kuzaliwa kwake wamekuwa wakizalisha mazao mbalimbali ikiwemo mazao makuu ya ndizi na kahawa bila kutumia aina yeyote ya pembejeo zenye kemikali sumu za viwandani na wamekuwa wakipata faida kubwa kwani ardhi yao ina rutuba ya kutosha kuweza kuzalisha mazao yenye tija.

Hata hivyo, baada ya kuanza mji wake aliendeleza uzalishaji wa mazao mengine, pia kufanya ufugaji ambapo mpaka sasa anazalisha kwa misingi ya kilimo ikolojia kwenye eneo la ukubwa wa ekari 17.

Kwa nini Mkulima Mbunifu?

“Nilibahatika kupata nakala za jarida la Mkulima Mbunifu kupitia kwa rafiki yangu Bw. Joseph Sekiku, Mkurugenzi wa FADECO radio, na nilipopitia nakala ya kwanza niliipenda sana kutokana na taarifa za uzalishaji zilizochapishwa kwani zinalenga kwa asilimia kubwa kumsaidia mkulima wa chini kufanya kilimo kwa njia sahihi na rahisi jambo tunalolifanya hapa Kagera.

Nilifurahi sana kujua kuwa kumbe changamoto zinazotupa hasa za magonjwa ya mifugo tunaweza kupambana nayo kwa njia za kiasili yaani kwa kutengeneza dawa zinazotokana na malighafi zilizopo katika maeneo yetu, tukawapa kuku na wakapona.”

Uzalishaji kwa misingi ya kilimo ikolojia ukoje?

“Kutokana na kuwa ardhi yetu ina rutuba ya kutosha kulingana na njia ya uzalishaji tunayoifanya, tunapata mavuno mengi na hatujawahi kabisa kutumia sumu za kemikali katika maeneo yetu, hivyo uzalishaji huu ni faida kwa mkulima kwani gharama ni ya chini.”

Bw. Joseph anaongeza kuwa, wanapata chakula salama kwa ajili ya familia zao, pia kwa ajili ya kuuza na kujipatia fedha za kujikimu katika shughuli na miradi mingine ya kifamilia.

Vipi kuhusu soko?

“Soko la mazao yote ni kubwa na linapatikana kwa urahisi, bei ni nzuri na rafiki kwa mkulima. Kwa mfano, kuku wa kienyeji wanatafutwa sana na hawatoshelezi kabisa soko hata wana Kagera wote wakizalisha kuku bado soko ni kubwa sana. Kwa sasa, tetea anauzwa kati ya TSh 20,000/- hadi TSh 25,000/- huku jogoo akifikisha hadi TSh 30,000/-.”

Changamoto

Bw. Joseph anasema kuwa, changamoto wanayokumbana nayo ni ya magonjwa hasa ugonjwa wa kideri kwa kuku na kupe kwa mbuzi. Mwanzoni mifugo walikuwa wakiteketea kwa asilimia kubwa mpaka walipokutana na wataalamu waliowashauri kuwachanja mifugo kila mara lakini. Hata hivyo, kama Mkulima Mbunifu inaposhauri, kuna mbinu bora za asili za kupambana na magonjwa bila gharama kubwa na kwa ufanisi.

Wito kwa Mkulima Mbunifu

Jarida la Mkulima Mbunifu linatoa elimu muhimu sana kwa wakulima na wafugaji. Wakulima ambao hawapokei jarida hili wanakosa kitu kikubwa. Ni ombi langu MkM kuhakikisha wanatanua wigo wa kusambaza majarida haya kwa wakulima wengi zaidi nchini kwa manufaa ya uzalishaji wa leo na wa vizazi vijavyo.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *