- Kilimo

Umuhimu wa mboga kiafya

Sambaza chapisho hili

Mboga ni mojawapo ya chakula bora kwani zikiliwa zenyewe kwa kuchanganya zina viini lishe tosha.

Hata hivyo, mboga zimegawanyika katika makundi kutokana na sehemu ya mmea iliyo muhimu katika chakula cha binadamu na viini lishe vipatikanavyo.

Sehemu za mmea wa mboga zinazotumika kama chakula ni pamoja na mizizi, shina, majani, matunda, maua na mbegu.

Kazi muhimu za mboga kwenye chakula

Mboga za mizizi ambazo ni pamoja na viazi mviringo, viazi, vitunguu maji, radishi, bitrut, vitunguu saumu, karoti nk.

Umuhimu wake

  • Zina viini lishe kama vile madini ya chuma na chokaa, vitamin A na C, wanga na karoti zina vitamin A nyingi kuliko zote.
  • Huongeza ladha na rangi na ni mlo kamili kwa binadamu.

Mboga za majani

Mboga za majani ni pamoja na kabichi, mnavu, mgagani, tembele, sukuma wiki, saladi, saro, chainizi nk.

Umuhimu wake

  • Mboga zote zenye rangi ya kijani kilichokoa zina viini lishe zaidi kuliko zilizo na rangi ya kijani kidogo.
  • Mboga za majani zina viini lishe kama vile vitamin A na C, protini, madini ya chokaa pamoja na madini ya chuma zinazoongeza rangi ya kupendeza na kupata kitoweo.

Mboga za matunda

Mboga za matunda ni kama vile, nyanya, matango, pilipili hoho, maboga, bamia, biringanya, ngogwe, maharagwe, kunde za maganda mabichi.

Umuhimu wake

  • Mboga hizi zina viini lishe ambavyo ni vitamin A na C, madini ya chuma pamoja na chokaa.
  • Mboga hizi pia zinaongeza ladha na rangi nzuri kwenye chakula, huvutia kula na huliwa kama kitoweo.

Mboga za matunda

Mboga za maua ni kama vile kauliflawa, maua ya maboga, maua ya milonge, brokoli nk.

Umuhimu wake

  • Mboga kama vile kauliflawa zina vitamin na protini kwa wingi.
  • Maua ya maboga pamoja na brokoli zina vitamin A na C kwa wingi.

Mboga za mbegu

Katika kundi hili, zinapatikana mboga kama vile maharage, njegere, kunde, choroko, mbegu za maboga.

Umuhimu wake

  • Mboga hizi zina viini lishe kama vile protini, vitamin A, B, D na K, madini ya chuma, wanga na mafuta kidogo.
  • Mboga hizi pia hutumika kama kitoweo na huongeza ladha katika chakula au mlo.

Mboga za shina

Mboga za shina ni pamoja na vitunguu maji, vitunguu saumu, seleri, liki

Umuhimu wake

  • Mboga hizi zina viini lishe kama vile vitamin A, B na C pamoja na madini kidogo.
  • Mboga hizi hutumika katika chakula ili kuleta ladha na hamu ya kula.

Maradhi ambayo unaweza kupata ukikosa kula mboga

Unapokosa kula mboga, maradhi mbalimbali huweza kushambulia mwili wako kama vile unyafuzi, nyogea, vidonda mdomoni na kwenye fizi, kupofuka macho, kukosa damu mwilini, matege na mifupa hafifu pamoja na tezi.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *